WhatsApp inavyozika vikao vya sherehe

Dar es Salaam. Mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano yanaanza kubadili kwa kasi namna jamii inavyoshiriki katika shughuli za kijamii huku makundi ya mitandao ya kijamii, hasa WhatsApp, yakitajwa kuchukua nafasi ya vikao vilivyokuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya harusi na shughuli nyingine za kifamilia.

Kwa miaka mingi katika jamii nyingi za Tanzania, vikao vya harusi vilikuwa zaidi ya mikutano ya kupanga sherehe bali sehemu muhimu ya kujenga mshikamano wa familia na jamii.

Katika vikao hivyo, ndugu, marafiki na majirani walikutana mara kwa mara kujadili maandalizi ya harusi, kutoa ushauri kwa maharusi na kuchangia gharama za shughuli hiyo muhimu ya kijamii.

Mbali na kupanga maandalizi, vikao hivyo pia vilikuwa fursa ya kuimarisha mahusiano ya kifamilia na kijamii, mara nyingi mikutano hiyo iligeuka kuwa sehemu ya kujenga urafiki, kubadilishana mawazo na hata kusuluhisha migogoro iliyokuwa ikiibuka kati ya wanafamilia au wanajamii.

Hata hivyo, hali hiyo sasa inaonekana kubadilika kadiri teknolojia ya mawasiliano inavyozidi kushika kasi, badala ya kukutana ana kwa ana, wengi wanachagua kujadili mambo kupitia makundi ya WhatsApp, hali inayorahisisha mawasiliano lakini pia kuibua mjadala kuhusu kupungua kwa utamaduni wa kukutana uso kwa uso.

Wachambuzi wa masuala ya jamii wameitafsiri hali hiyo kama ishara ya mabadiliko makubwa ya utamaduni wa kijamii, huku baadhi ya wazee wakilalamika kuwa utamaduni wa kukutana, kushauriana na kushirikiana uso kwa uso unapotea taratibu.

Mkazi wa Kinondoni, Mzee Paulo Mwakalinga (63), anakumbuka enzi ambazo vikao vya harusi vilikuwa tukio muhimu la kijamii.

Amesema vikao hivyo vilikuwa zaidi ya mikutano ya kupanga sherehe, bali pia sehemu ya kujenga mshikamano wa jami, marafiki na ndugu walikutana mara kwa mara kujadili maandalizi, kutoa ushauri kwa maharusi na kuchangia gharama za harusi.

“Zamani ukiitwa kwenye kikao cha harusi ulikuwa lazima uhudhurie. Watu walikutana, walijadili na hata kula pamoja. Ilikuwa njia ya kuimarisha uhusiano wa jamii,” amesema.

Ameongeza vikao hivyo vilikuwa na nidhamu maalumu, kuanzia kuchangia fedha, kushauri maharusi hadi kupanga majukumu ya siku ya harusi.

“Watu walikuwa wanachangia mawazo, wengine walikuwa wanajitolea kusaidia kazi mbalimbali. Ilikuwa ni ushirikiano wa kweli. Lakini sasa, anasema, hali imebadilika kwa kiasi kikubwa.

“Leo hii watu wanategemea WhatsApp. Unatuma ujumbe tu, lakini ile roho ya kukutana na kujadiliana inapotea. Watu wanadhani kuandika ujumbe kwenye simu ni sawa na kuhudhuria kikao, lakini si kweli, kuna mambo mengi yanapotea,” amesema.

Kwa upande wake, Teckla Shija amesema vikao vya maandalizi ya harusi vilikuwa pia nafasi ya kutoa ushauri kwa wanandoa.

“Katika vikao hivyo kulikuwa na wazee waliokuwa wanawashauri maharusi kuhusu maisha ya ndoa. Lakini sasa ushauri huo unapotea kwa sababu watu hawakutani tena.

Wakati mwingine vikao hivi vilikuwa sehemu ya kufundisha vijana heshima, uwajibikaji na ushirikiano,” amesema Teckla.

Mhadhiri wa sosholojia wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk Joanita Mushi amesema kupungua kwa vikao vya ana kwa ana ni sehemu ya mabadiliko ya kijamii yanayoletwa na teknolojia na mabadiliko ya maisha ya mijini.

Amesema hali hiyo imefanya mikutano ya ana kwa ana kuwa changamoto.

“Katika jamii za zamani, watu waliishi karibu zaidi na walikuwa na muda wa kushirikiana. Lakini katika miji ya sasa watu wana shughuli nyingi na umbali wa makazi ni mkubwa. Ndiyo maana watu wanachagua njia rahisi zaidi kama makundi ya WhatsApp,” amesema Dk Joanita.

Hata hivyo, mtaalamu huyo ameonya jamii inapaswa kutafuta uwiano kati ya teknolojia na utamaduni.

“Teknolojia ni muhimu, lakini haipaswi kuua kabisa utamaduni wa kukutana na kushirikiana ana kwa ana. Mnapokutana kuna namna mnashirikishana na kubadilishana mawazo kwa ukaribu Zaidi, tofauti na ikifanyika kwa njia ya teknolojia,” amesema Dk Joanita.

Salma Mussa na mchumba wake Ibrahim Makame, waliotarajia kufunga ndoa Februari mwaka huu, changamoto ya vikao vya harusi kwao ilikuwa kubwa kuliko walivyotarajia.

Salma amesema walipoanzisha kikao cha harusi walitarajia watu watakuwa wanakutana mara kwa mara kupanga mambo mbalimbali ya sherehe yao.

“Tulikuwa na zaidi ya wajumbe 25 kwenye kamati. Lakini kila tulipopanga kikao watu walikuwa wanatoa visingizio. Wengine walikuwa wanasema wako kazini, wengine wanasema wapo mbali,” amesema Salma.

Hatimaye waliamua kuanzisha kundi la WhatsApp ili kurahisisha mawasiliano.

“Baada ya kuanzisha kundi, watu wakaanza kuchangia mawazo humo humo. Lakini ukweli ni kwamba mijadala mingi ilikuwa haimaliziki vizuri kwa sababu watu wanajibu kwa vipindi tofauti,” amesema.

Kwa upande wake Ibrahim amesema wakati mwingine uamuzi muhimu ulikwama kwa sababu baadhi ya wajumbe hawakuwa wanashiriki kikamilifu kwenye majadiliano ya mtandaoni.

“Kuna watu wanaweza kusoma ujumbe lakini wasijibu. Halafu baadaye wanauliza tena jambo lile lile,” amesema Ibrahim.

Simulizi inayoendana na hiyo imetolewa na Neema Kikoti mkazi wa Mbagala Kichemchem ambaye ameeleza namna matarajio yake ya kuwaona watu wake wa karibu wakishiriki kwenye harusi yake yalivyoyeyuka.

“Siku ya kikao cha kwanza, viti vilivyopangwa zaidi ya 30 vilibaki vitupu. Nilitarajia kuona marafiki na ndugu wakija kama nilivyoona kwa harusi za wengine zamani. Lakini watu watano tu ndio walifika.

“Wengi waliishia kuandika kwenye kundi la WhatsApp la harusi yao wakisema wako kazini au wanasafiri, huku wengine wakiahidi kutuma mchango wao kupitia simu. Mwisho wa siku tulijikuta tunapanga mambo mengi sisi wenyewe na watu wachache waliokuja. Ilikuwa tofauti kabisa na tulivyotarajia,” amesema Neema.

Ukuaji wa teknolojia wachochea

Wataalamu wamesema moja ya sababu kubwa ya mabadiliko hayo ni kasi ya maisha ya sasa pamoja na maendeleo ya teknolojia.

Mwanasaikolojia na mshauri wa masuala ya familia, Agnes Lema amesema mitandao ya kijamii imebadilisha namna watu wanavyowasiliana na kushirikiana.

“Teknolojia imeleta urahisi mkubwa katika mawasiliano. Watu wanaweza kujadili mambo bila kukutana ana kwa ana. Hii imewafanya wengi kuona vikao vya ana kwa ana havina umuhimu sana,” amesema Agnes.

Hata hivyo ametahadharisha mabadiliko hayo yanaweza kuwa na athari za kijamii akieleza kuwa mawasiliano ya ana kwa ana yana faida nyingi, ikiwemo kujenga uhusiano wa karibu, kuelewana vizuri na hata kupunguza migogoro ambao ambayo ni magumu kuyapata kwenye mawasiliano ya mtandaoni.

Changamoto za makundi sogozi

Licha ya urahisi wake, baadhi ya wanajamii wanasema makundi sogozi kama WhatsApp nayo yana changamoto zake.

Asha Mohamed, ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa kamati ya harusi ya rafiki yake, amesema mara nyingi mijadala ya mtandaoni hukosa umakini.

“Unakuta watu wanaanza kujadili suala la harusi, ghafla mtu anatumia picha au utani ambao hauhusiani na mada. Mwisho wa siku mjadala unapotea,” amesema.

Amesema pia kuna wakati baadhi ya wajumbe wanashindwa kutoa maoni yao kwa sababu hawapendi kujadili mambo kwa maandishi.

“Wapo watu wanaweza kuzungumza vizuri sana kwenye kikao, lakini kwenye WhatsApp hawajisikii huru kuandika na inaweza kutokea pia mtu akawa na mawazo lakini hana huo muda wa kuandika,” amesema Asha.

Wataalamu wameshauri jamii inapaswa kutumia teknolojia kwa busara bila kuacha kabisa utamaduni wa kukutana.

Dk Lema amesema makundi ya WhatsApp yanaweza kuwa nyenzo ya kusaidia mawasiliano, lakini yasichukue nafasi ya mikutano yote.

“Ni vizuri kuwa na mchanganyiko. Baadhi ya mambo yanaweza kujadiliwa mtandaoni, lakini maamuzi muhimu yafanywe kwenye vikao vya ana kwa ana,” amesema.

Kwa upande wa Salma na Ibrahim, licha ya changamoto walizokutana nazo, harusi yao hatimaye ilifanikiwa kufanyika.

“Tungetamani watu wangekuwa wanahudhuria vikao kama zamani. Kuna furaha ya pekee kukutana na kupanga mambo pamoja,” amesema Salma.