Dar es Salaam. Wakati mabilioni ya fedha yakitumika kila mwaka katika matengenezo ya barabara, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imebaini kukosekana kwa mfumo madhubuti wa kupanga na kusimamia matengenezo hayo.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi wa ufanisi ya mwaka wa fedha 2024/25, imesababisha barabara kuharibika bila kufanyiwa matengenezo kwa wakati.
Hata hivyo, taarifa ya Mapato na Matumizi ya Mfuko wa Barabara mwaka 2023 ilionyesha Serikali hutumia Sh1 trilioni kila mwaka kwa matengenezo ya miundombinu hiyo.
Katika ripoti hiyo ya CAG, imebainika kuwapo kwa udhaifu katika mfumo wa usimamizi na matengenezo ya barabara nchini, hali inayochangia kuendelea kuharibika kwa miundombinu hiyo licha ya kuwepo kwa rasilimali na mipango ya utekelezaji.
Ukaguzi huo uliofanyika katika sekta ya barabara, umeonesha hakuna mfumo madhubuti unaotumika kubaini, kupanga na kutekeleza mahitaji ya matengenezo ya barabara kwa wakati na kwa ufanisi.
“Hali hii imekuwa ikisababisha barabara nyingi kuharibika mapema, huku gharama za ukarabati zikiendelea kuongezeka,” imeeleza ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imeeleza taasisi zinazohusika na usimamizi wa barabara zimekuwa zikitekeleza matengenezo bila kuwa na mfumo wa uhakika wa kutambua kwa usahihi kiwango cha uharibifu na vipaumbele vinavyotakiwa kushughulikiwa.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya barabara zimekuwa zikifanyiwa matengenezo yasiyoendana na hali halisi ya uharibifu, huku nyingine zikichelewa kufanyiwa matengenezo hadi kufikia hatua ya kuhitaji ukarabati mkubwa.
Aidha, ukaguzi umebaini kukosekana kwa mfumo wa kisasa wa ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu za barabara kumeathiri uwezo wa mamlaka husika kupanga kwa usahihi matengenezo ya miundombinu hiyo.
Badala yake, uamuzi umekuwa ukifanyika kwa kutumia taarifa zisizo kamili au zisizo sahihi, jambo linalochangia matumizi yasiyo na tija ya fedha za umma.
Katika tathmini ya utekelezaji wa mipango ya matengenezo ya barabara, ripoti imeonesha kumekuwapo na utekelezaji usioridhisha wa kazi zilizopangwa, hali inayotokana na udhaifu katika usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya miradi.
Baadhi ya miradi imekuwa ikichelewa kukamilika, huku mingine ikitekelezwa chini ya viwango vinavyotakiwa.
Vilevile, ukaguzi umeonesha kuwa hakuna uratibu wa kutosha kati ya taasisi mbalimbali zinazohusika na sekta ya barabara, jambo linalosababisha kuwepo kwa mwingiliano wa majukumu pamoja na matumizi yasiyo na ufanisi ya rasilimali.
“Hali hii imekuwa ikichangia kushindwa kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa katika mipango ya maendeleo ya miundombinu,” imeeleza ripoti hiyo.
Ripoti hiyo pia, imebainisha baadhi ya barabara zimeendelea kuharibika kutokana na kutofanyika kwa matengenezo ya mara kwa mara, jambo ambalo lingeweza kupunguza kasi ya uharibifu na gharama za ukarabati mkubwa.
“Kukosekana kwa mpango thabiti wa matengenezo endelevu kumeonekana kuwa chanzo kikubwa cha changamoto hiyo,” imeeleza ripoti hiyo.
Kwa upande wa matumizi ya fedha, ukaguzi umeonesha kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara hazitumiki kwa ufanisi kutokana na kukosekana kwa mfumo unaoongoza matumizi hayo kwa kuzingatia mahitaji halisi.
Hali hiyo, ripoti imeonyesha imekuwa ikisababisha baadhi ya maeneo kupata matengenezo yasiyo ya kipaumbele, huku maeneo yenye uhitaji mkubwa yakiachwa bila kushughulikiwa kwa wakati.
Matokeo ya ukaguzi yanaonesha wazi, kukosekana kwa mfumo madhubuti wa usimamizi wa matengenezo ya barabara kumechangia kudorora kwa ubora wa miundombinu hiyo nchini.
“Barabara nyingi zimeendelea kuwa katika hali mbaya, hali inayosababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara pamoja na kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii,” imeeleza ripoti hiyo.
Ili kuboresha hali ya barabara nchini, ripoti inapendekeza kuwepo kwa mfumo wa uhakika wa kutambua mahitaji ya matengenezo, kupanga vipaumbele kwa usahihi na kuimarisha usimamizi na uratibu wa taasisi zote zinazohusika na sekta hiyo.
“Bila hatua hizo, juhudi za kuboresha miundombinu ya barabara zitaendelea kukumbwa na changamoto na kushindwa kuleta matokeo yaliyokusudiwa.”
