Azam FC yarudi kwa beki Mkongo

KUNA taarifa za Azam FC kufanya mazungumzo ya kumsajili beki wa kulia wa  Al-Hilal Omdurman, Steven Ebuela aliyezaliwa Machi 07, 2001 (umri wa miaka 25) ili kuongeza nguvu msimu ujao wa 2026/27.

Azam ambayo kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa imeshinda michezo nane, imetoka sare kumi na haijapoteza mchezo wowote ikiwa bado kwenye mbio za ubingwa wa ligi.

Azam ilianza kuhitaji huduma ya Ebuela katika usajili wa dirisha kubwa la msimu huu, lakini ilishindikana kwa sasa mazungumzo yanaendelea vizuri na kuna uwezekano mkubwa akajiunga na klabu hiyo.

Chanzo cha taarifa hiyo kilisema kocha wa timu hiyo, Florent Ibenge ndiye aliyependekeza asajiliwe Ebuela aliyejiunga na Al-Hilal Januari 21, 2023 na mkataba wake unaonyeshwa utamalizika Juni 30, 2027.

“Lazima mwisho wa msimu wataongezwa wachezaji wapya na kupunguza kulingana na ripoti ambayo kocha atatupatia, ili kuhakikisha tunakuwa na kikosi imara chenye ushindani,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Ebuela ni beki mwenye kasi, tunaamini akijiunga na klabu yetu kama tutalifanikisha hilo, atakuja kuongeza nguvu kwani msimu ujao tutahitaji kufanya vizuri zaidi kimataifa na Ligi Kuu Bara, hivyo lazima tutahitaji wachezaji wenye uwezo wa juu.”

Endapo Ebuela akijiunga na Azam msimu ujao atakutana na ushindani wa namba dhidi ya Nathaniel Chilambo anacheza beki ya kulia na kushoto anaingia na kutoka, huku panga pangua ni Lusajo Mwaikenda ambaye hadi sasa ana bao moja na asisti mbili na msimu uliyopita alikuwa na asisti tatu.