Azam yalia na pointi 20 ikiweka rekodi Ligi Kuu

MSIMU huu wa Ligi Kuu Bara 2025/26, takwimu za mechi za ugenini kwa vigogo wa ligi hiyo, Simba, Yanga na Azam zinaonyesha mabadiliko makubwa ya viwango tofauti na msimu uliopita na walikuwa wakitesa tu.

Takwimu zinaonyesha Simba ambayo ipo nafasi ya pili Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi  36, hadi sasa imecheza jumla ya mechi tisa ugenini, ikishinda nne dhidi ya JKT Tanzania (1-2), KMC (0-2), Tanzania Prisons (0-2) na Singida Black Stars kwa mabao 1-2, sare tano na hawajapoteza hata moja.

Asilimia yao ya ushindi ni 44.4 lakini kinachovutia zaidi ni mechi hizo tano ambazo imetoa sare ugenini nne hawakufunga bao ambazo ni dhidi ya Dodoma Jiji (0-0), Azam (0-0), TRA United (0-0) na Yanga (0-0). 

Yanga ambayo inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 44, imeshinda mechi tano kati ya tisa ugenini, ikitoa sare nne bila kipigo chochote.

Ushindi wao mkubwa umejumuisha matokeo dhidi ya Singida Black Stars kwa mabao 0-3  na Pamba  kwa mabao 0-3, pia wamekumbana na michezo migumu ya sare ambayo hawakupata bao dhidi ya Azam 0-0, Mbeya City 0-0 na TRA (0-0).

Azam inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 34 imekuwa na changamoto zaidi kuliko wapinzani wao, wakishinda mechi nne kati ya 10 za ugenini, sare sita, hawajapoteza, , lakini kwa jumla wametoka sare mechi 10, ambazo ni rekodi kwao. 

Ingawa wameonyesha uimara wa kutopoteza mechi, kiwango chao cha kushinda kimeshuka ugenini hadi asilimia 40 huku sare hizo zikiwa dhidi ya JKT Tanzania (1-1), Namungo (1-1), Pamba Jiji (2-2),Tanzania Prisons (0-0), Mashujaa (0-0) na Mbeya City (0-0).

Ukilinganisha takwimu hizi, inaonekana wazi kuwa hakuna timu inayotawala ugenini kwa kiwango kikubwa kama ilivyokuwa misimu iliyopita. Michezo ya ugenini imegeuka kuwa kaa la moto kwa vigogo hao.

Msimu wa 2024/25, hali ilikuwa tofauti kabisa, ambapo Yanga na Simba walikuwa na kiwango cha juu sana ugenini. Yanga walikuwa na asilimia 88.9 ya ushindi ugenini, kipindi kama hiki wakishinda mechi nane kati ya tisa huku Simba pia wakifikia asilimia 88.9 sawa na watani zao.

Azam FC nao walikuwa na msimu mzuri, wakishinda kwa asilimia 70 ya mechi zao za ugenini saba kati ya 10, hali ambayo ni bora zaidi kuliko msimu wa sasa ambapo wameshuka hadi asilimia 40 ya ushindi.

Kwa ujumla, msimu wa 2025/26 unaonyesha wazi kushuka kwa kiwango cha ushindi ugenini kwa timu zote tatu kubwa, hasa Simba na Yanga ambao walikuwa wakitawala. Hii inaweza kuchochewa na ongezeko la ushindani wa ligi, ubora wa timu ndogo kupanda kama inavyoelezwa na kocha wa zamani wa Yanga, Azam na Singida United, Hans van der Pluijm.

“Soka la Afrika Mashariki linazidi kuwa na ushindani mkubwa, timu ndogo zimepiga hatua kubwa kimfumo na kiufundi, hivyo hakuna tena mechi rahisi ugenini kama ilivyokuwa zamani,” alisema kocha huyo.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, Azam FC wanaonekana kuwa waathirika wakubwa wa mabadiliko haya, kwani ingawa hawapotezi mechi yoyote hadi sasa wakiwa chini ya Florent Ibenge, wamechemka katika mechi nyingi za ugenini.

Yanga bado wanaongoza kwa ubora katika mechi za ugenini msimu huu kwa asilimia 55.6 ya ushindi wameshuka kwa asilimia 33.3, wakifuatiwa na Simba SC wenye 44.4 wameshuka kwa asilimia 44.5 huku Azam FC wakibaki nyuma kwa 40 nao wameshuka kwa asilimia 30.