Azania benki yaja na huduma mpya malipo ya kidijitali

Dar es Salaam. Katika kuendeleza mkakati wa kuboresha huduma za kifedha kupitia teknolojia, Benki ya Azania imezindua rasmi huduma mpya ya malipo ya kidijitali ijulikanayo kama ‘Azania Lipa’ kuleta urahisi zaidi kwa wateja.

Huduma hiyo ni mfumo wa kisasa unaowawezesha wateja kufanya malipo kwa urahisi kupitia QR code, namba ya malipo (till number), pamoja na kutumia simu za mkononi kupitia Mobile Banking au USSD. Mfumo huu umeundwa kuunganisha huduma za benki, mitandao ya simu na wafanyabiashara katika jukwaa moja lenye ufanisi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Kitengo cha Ubunifu na Mikakati, Jackson Lohay, amesema uzinduzi wa ‘Azania Lipa’ ni hatua muhimu katika safari ya mabadiliko ya kidijitali ya benki hiyo.

“Kwa miaka kadhaa sasa, Benki ya Azania imewekeza katika kujenga mfumo imara wa huduma za kidijitali ikiwemo Mobile Banking, Internet Banking, WhatsApp Banking pamoja na mtandao wa Azania Wakala. Azania Lipa inakuja kuongeza thamani katika huduma hizi kwa kurahisisha zaidi malipo kwa wateja na wafanyabiashara,” amesema.

Ameongeza huduma hiyo inalenga kuongeza ujumuishwaji wa kifedha, kusaidia ukuaji wa biashara na kupunguza matumizi ya fedha taslimu katika miamala ya kila siku.

Kwa upande wa wafanyabiashara, ‘Azania Lipa’ inatoa suluhisho salama na rahisi la kupokea malipo, kupunguza hatari ya kubeba fedha taslimu na kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa biashara.

Aidha, huduma hiyo haina gharama za usajili, inafanya kazi na mitandao yote ya simu pamoja na benki mbalimbali, na haina makato kwa wateja wa Benki ya Azania.

Benki hiyo imewahimiza wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla kuanza kutumia ‘Azania Lipa’ ili kufurahia urahisi, usalama na ufanisi wa huduma hiyo mpya.

Uzinduzi wa ‘Azania Lipa’ unaendelea kudhihirisha dhamira ya Benki ya Azania ya kuwa mstari wa mbele katika utoaji wa suluhisho bunifu za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wateja na kuchangia maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.