Dar es Salaam. Halmashauri tano na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), zimebainika kutumia magari ya Serikali yaliyosajiliwa kwa namba binafsi, jambo ambalo ni kinyume na matakwa yaliyowekwa ya utambuzi na udhibiti wa mali za umma.
Hayo yamebainika katika Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Tamisemi, Sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kwa mwaka fedha 2024/25, iliyowasilishwa bungeni Aprili 10, 2026.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa Kanuni ya 3(3) ya Kanuni za Fedha za Umma (Usimamizi wa Mali za Umma) za mwaka 2024 inamtaka Ofisa Masuuli kuhakikisha kila mali ya umma inayopatikana inatambuliwa kwa namba au msimbo wa utambulisho wa kipekee, kama inavyoweza kuainishwa na sheria yoyote iliyoandikwa au katika mfumo uliowekwa kwenye nyongeza ya kwanza.
Pia, Kanuni ya 18(1) ya Kanuni za Usalama Barabarani (Usajili wa Vyombo vya Moto) za mwaka 2001 inataka namba ya usajili kwa vyombo vyote vya moto isipokuwa vile vinavyomilikiwa na Serikali, Jeshi la Ulinzi Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mashirika ya kimataifa, ofisi za kidiplomasia au kibalozi itanguliwe na herufi ‘T’ ikifuatiwa na tarakimu na herufi kuanzia ‘101 AAA’ hadi ‘999 ZZZ’.
“Taasisi sita zilikuwa na jumla ya magari 21 yenye namba binafsi za usajili badala ya namba za usajili za Serikali. Utaratibu huu hauendani na matakwa yaliyowekwa ya utambuzi na udhibiti wa mali za umma,” imeeleza ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imezitaja halmashauri za Jiji la Dar es Salaam, Wilaya ya Kibaha, Mwanga, Manispaa ya Lindi na Manyara kuwa ndizo zilizobainika.
Ripoti hiyo imebainisha tatizo hili linatokana na kutozingatia matakwa ya kikanuni, uangalizi hafifu wa maofisa husika, na mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti isiyo na tija, jambo lililosababisha kushindwa kuhakikisha kuwa mali mpya au zilizohamishwa zinasajiliwa mara moja kama mali za Serikali.
“Matumizi ya namba binafsi kwenye magari ya Serikali na pikipiki yanadhoofisha uzingatiaji wa sheria, kudhoofisha utambuzi na udhibiti wa mali. Hali hii huongeza hatari ya matumizi mabaya, ubadhirifu, au upotevu wa mali za umma na kudhoofisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa mali za Serikali,”amesema CAG.
“Napendekeza Tamisemi ihakikishe magari yote na pikipiki zote, ziwe mpya au zilizohamishwa kutoka taasisi au maeneo mengine, zinasajiliwa ipasavyo na kwa wakati kwa kuzingatia matakwa ya sheria, kanuni na taratibu husika za usajili,” imeelekeza ripoti hiyo.
Pia, ripoti hiyo imependekeza hatua za haraka za kurekebisha zichukuliwe ili kurasimisha usajili wa magari na pikipiki yaliyobainishwa, na kuimarisha mifumo ya udhibiti ili kuzuia kujirudia kwa tatizo hilo siku zijazo.
