DC Arusha aonya matumizi mabaya ya magari ya Serikali

Arusha. Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amewataka watumishi wa umma kuhakikisha wanatumia ipasavyo magari ya Serikali yaliyotolewa kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, akionya dhidi ya matumizi binafsi yasiyo na tija.

Mkude ametoa maagizo hayo leo Jumatatu, Aprili 13, 2026 wakati akizungumza katika hafla ya kukabidhi vitendea kazi mbalimbali ikiwemo magari mapya, ambapo mkoa huo umepokea malori yenye kreni mbili, magari aina ya Land Cruiser manne na bajaji tano kwa ajili ya shughuli za huduma kwa wateja, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Arusha.

Amesema Serikali imetumia fedha nyingi kununua magari hayo, hivyo ni wajibu wa watumishi kuyatumia kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Niwasihi twende tukafanye kazi kwa bidii. Haya magari tuliyopatiwa katika mkoa wetu na kugawanywa katika wilaya zake yatumike ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa. Tusiyatumie kwa mambo ya kibinafsi yasiyoleta tija,” amesema.

Amesema kwa sasa Serikali imepiga hatua kubwa katika kusambaza umeme nchini, akibainisha kuwa zamani huduma hiyo ilikuwa ikipatikana katika taasisi chache za umma na maeneo ya mijini pekee, hali ambayo imebadilika kwa sasa.

“Tumetoka mbali sana. Zamani umeme ulikuwa unapatikana mikoani na kwenye taasisi chache za umma, lakini sasa umefika hadi wilayani, vijijini na vitongoji. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma hii muhimu,” amesema.

Mkude amewataka watumishi wa Tanesco kuongeza bidii na kuimarisha usimamizi wa miradi ya umeme ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati huku akipongeza utendaji wa shirika hilo kwa sasa.

Awali, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Arusha, Mhandisi Kisika Kisika amesema hali ya upatikanaji wa umeme mkoani humo ni shwari huku akieleza kuwa miundombinu imeimarika na maboresho yanaendelea kufanyika mara kwa mara.

Amesema kuwa Mkoa wa Arusha una vituo vikubwa vitatu vinavyosaidia kusambaza umeme, na  changamoto zilizopo ni ndogo na za kawaida.

“Kuna utulivu mkubwa wa umeme. Miundombinu yetu iko vizuri na tunaendelea na maboresho ya hapa na pale ili kuhakikisha huduma inazidi kuwa bora,” amesema.

Amesema vijiji vyote 368 vya mkoa huo vina huduma ya umeme na vitongoji 945 kati ya 1,505 vina huduma hiyo muhimu.

“Tumepokea miradi mingi ya Rea na katika mwaka huu wa fedha tumetengewa Sh19.5 bilioni kwa ajili ya kupeleka umeme katika vitongoji 127, ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali kuhakikisha vitongoji vyote vinapata umeme ifikapo mwaka 2030,” amesema.

Amesema mkoa huo wenye wateja 318,863 wa makundi mbalimbali ya watumiaji, umejipanga kusimamia miradi hiyo kikamilifu na kuhakikisha wananchi wanahudumiwa kwa ukaribu, huku malalamiko yote yakishughulikiwa kwa wakati.

Awali, Meneja wa Huduma za Usalama anayesimamia kitengo cha usafirishaji makao makuu ya shirika hilo, Lenin Kiobya amesema Serikali imenunua magari 556 kwa ajili ya kuboresha huduma za umeme nchi nzima katika mwaka wa fedha 2025/26.

Amesema kati ya magari hayo, malori 215 yenye uzito wa tani saba na 10 yamepangwa kusambazwa, ambapo tayari 61 yamefika na mengine yanaendelea kuwasili kwa awamu.

“Wiki ijayo tunatarajia kupokea magari mengine 61 ili kuendelea kuimarisha huduma zetu. Serikali pia imetenga zaidi ya Sh200 bilioni kwa mwaka ujao kwa ajili ya kuongeza vitendea kazi hivi,” amesema.