Hatua kwa hatua filamu ya Chobwedo ilivyoanza Yanga, ikaishia Simba

KUNA filamu moja ya usajili imeripotiwa kufanyika na timu kongwe za hapa nchini, Simba na Yanga inayomhusu winga wa TRA United, Ramadhan Salum Chobwedo.

Winga huyo ambaye kwa siku za karibuni amekuwa midomoni mwa wafuatiliaji wengi wa Ligi Kuu Bara kutokana na kiwango chake bora uwanjani alichokionyesha dhidi ya wakongwe hao,

imeripotiwa Simba imemalizana naye wakati Yanga ilipokuwa kwenye hesabu za kumsajili kwa ajili ya msimu ujao.

Mwanaspoti liliwahi kuandika jina la winga huyo wa zamani wa KenGold, limefika mezani mwa mabosi wa Yanga na linajadiliwa na kama mambo yangeenda vizuri, basi angemwaga wino katika kikosi hicho.

Inaelezwa baada ya Simba kupata taarifa watani zao wa jadi Yanga wana mpango wa kumchukua nyota huyo, waliingilia dili haraka na kufanya mchakato wa kuipata saini yake.

Taarifa kutoka Simba zililiambia Mwanaspoti, klabu hiyo inadaiwa kufanya haraka kumsajili Chobwedo baada ya kuwa na uhitaji na winga mzawa kwa ajili ya msimu ujao.

“Simba imekamilisha usajili wa Chobwedo kwa mkataba wa miaka miwili kwani moja kati ya mipango iliyopo msimu ujao ni kuongeza nguvu eneo la mbele ikiwemo winga, ndipo Chobwedo akaonekana ni mtu sahihi kwa wachezaji wazawa kwani hivi sasa hakuna mzawa ambaye amepenya kikosini kwa upande huo,” kilisema chanzo hicho.

Awali Yanga iliripotiwa kuwa ya kwanza kuulizia huduma ya Chobwedo, ilidaiwa mabosi wa klabu hiyo walikutana mezani na kuanza kumjadili winga huyo.

Katika majadiliano hayo, Mwanaspoti lilijuzwa kulikuwa na mvutano wa pande mbili, wapo waliokuwa wakikubaliana wamsajili, wengine wakihitaji kumuona zaidi kwani hawataki kufanya mambo kwa haraka kisha wakaja kujutia.

“Dili la Chobwedo kwenda Yanga lilikuwa na mvutano, wapo mabosi walioona kiwango chake kinahitaji muda zaidi kuangaliwa kabla ya kufanya uamuzi wa kumsajili, wengine wakitaka asajiliwe fasta, hapo ndipo kukawa na mgawanyiko.

“Licha ya kwamba amekuwa midomoni mwa wengi kutokana na aina yake ya uchezaji ambao imewavutia baadhi ya viongozi, lakini mvutano huo ndiyo uliofanya uamuzi kuchelewa kufanyika,” kilisema chanzo kutoka Yanga.

Mwanzoni wakati Chobwedo anahusishwa na Yanga, Mwanaspoti lilimtafuta winga huyo kuhitaji kufahamu ukweli wa kinachoendelea na amesema hajafanya mazungumzo na mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, lakini timu yoyote itakayohitaji huduma yake, anaweza kufanya nayo majadiliano kupitia wasimamizi wake.

“Kuhusu kutakiwa na Yanga mimi sijazungumza nao, kwa sasa ni mchezaji wa TRA, hivyo siwezi kuzungumzia klabu nyingine, halafu timu zinamchukua mchezaji baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu, huwezi kusema wanakuchukua kisa nimecheza mechi mbili mfululizo, kiukweli binafsi najiona bado nina safari ndefu ya kupambana,” amesema Chobwedo.

Chobwedo ambaye huu ni msimu wake wa kwanza kuitumikia TRA United baada ya kusaini mwaka mmoja akitokea KenGold, mkataba wake kikosini hapo unamalizika mwisho wa msimu huu, hadi sasa amefunga bao moja na asisti moja Ligi Kuu Bara.

Tangu kuondoka kwa Kibu Denis aliyeuzwa Januari mwaka huu kwenda Al-Nasr ya Libya, hakuna winga mzawa Simba anayecheza kikosi cha kwanza. Wakati Kibu akiondoka, Saleh Karabaka anacheza JKT Tanzania kwa mkopo tangu mwanzoni mwa msimu huu.

Winga mzawa aliyebaki Simba ni Ladaki Chasambi aliyeshindwa kupenya mbele ya wageni Libasse Gueye, Anicet Oura na Elie Mpanzu.