KOCHA wa maafande wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesema licha ya mwenendo mzuri wa timu hiyo kwa sasa ila anataka kufikia rekodi ya msimu uliopita na kuandika nyingine mpya, baada ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo alisema ushindi huo wa mabao 3-0 dhidi ya Mbuni ni muhimu kwa timu hiyo japo malengo yao ni kuhakikisha wanaivuka rekodi ya msimu uliopita, licha ya kukiri ushindani mkubwa wa wapinzani wao hasa kwa hatua inayofuata ya robo fainali.
“Kadri unavyozidi kusonga mbele ndivyo ambavyo ushindani pia unazidi kuongezeka kwa sababu unakutana na timu bora pia, tumepata ushindi mzuri wa kutufikisha hatua ya robo fainali, ila malengo yetu kiujumla ni hadi fainali,” alisema Ally.
Kikosi hicho kimekata tiketi ya kufuzu hatua ya robo fainali, baada ya kushinda mabao 3-0 dhidi ya Mbuni FC ya Arusha, inayoshiriki Ligi ya Championship, katika mechi ya hatua ya 16 bora iliyopigwa juzi Ijumaa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar.
Katika mechi hiyo, mashujaa wa maafande hao walioipeleka hatua ya robo fainali ni mshambuliaji Edward Songo aliyefunga mabao mawili ya dakika ya 4 na 51, huku lingine likifungwa na Anuary Kilemile dakika 61.
Timu hiyo msimu huu ilianza hatua ya 64 kwa kuwachapa mabingwa wa Ligi Kuu Bara mwaka 1982, Pan Africans FC, mabao 7-0, huku 32 bora, ikaichapa Hausung FC ya Njombe mabao 2-0, kisha 16 bora ikaifunga Mbuni mabao 3-0 na kutinga robo fainali.
Msimu uliopita wa 2024-2025, timu hiyo ilifika hatua ya nusu fainali ikichapwa mabao 2-0 dhidi ya Yanga, iliyotinga fainali na kutwaa taji hilo baada ya kuichapa Singida Black Stars, mabao 2-0.