Mahakama yatupilia mbali rufaa ya kifo wauaji wa dereva bodaboda

Arusha. Mahakama ya Rufani imetupilia mbali rufaa ya Nathanael Matei na Martin Tiophil waliokuwa wakipinga adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kutiwa hatiani kwa kumuua Haji Hussein na kuiba pikipiki yake.

Uamuzi huo ulitolewa Aprili 10, 2026 na majaji Lugano Mwandambo, Abraham Mwampashi na Lameck Mlacha, baada ya mahakama kujiridhisha kuwa ushahidi wa kimazingira uliowasilishwa ulikuwa wa kutosha kuwaunganisha moja kwa moja na tukio hilo la mauaji.

Awali, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliwatia hatiani washtakiwa hao kwa kosa la mauaji yaliyotokea Oktoba 11, 2020 katika kijiji cha Kiru Ndogo wilayani Babati, mkoani Manyara. Ilielezwa kuwa siku ya tukio walikodisha usafiri wa bodaboda na baadaye kumuua dereva huyo kwa kumnyonga, kisha kuutelekeza mwili wake msituni katika eneo la Kiru Hill.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, warufani walikuwa watu wa mwisho kuonekana na marehemu akiwa hai. Aidha, baada ya kukamatwa, waliwaongoza polisi hadi mahali ulipokuwa mwili wa marehemu, ambao ulikutwa ukiwa umeoza, ukiwa umefungwa mikono na kuwa na alama za kunyongwa shingoni.

Ripoti ya daktari ilithibitisha kuwa chanzo cha kifo kilikuwa ni kukosa hewa, hali iliyothibitisha kuwa marehemu aliuawa kwa kunyongwa. Pia ushahidi ulionesha kuwa warufani walihusika na kuichukua pikipiki ya marehemu na baadaye kuwapa watu wengine.

Katika rufaa yao, walidai kuwa ushahidi uliotumika ulikuwa dhaifu, wenye kukinzana na haukuweza kuthibitisha hatia yao bila shaka yoyote. Pia walipinga uhalali wa maungamo yaliyotumika dhidi yao wakidai yalipatikana kinyume cha sheria na kwa njia ya kulazimishwa.

Mahakama ya Rufani ilikubaliana kwa sehemu na hoja hizo, ikibaini kuwa baadhi ya maelezo ya maungamo hayakukidhi matakwa ya kisheria na hivyo hayakuwa na uzito wa ushahidi. Hata hivyo, mahakama ilisisitiza kuwa hata baada ya kuyaondoa, bado kulikuwa na ushahidi wa kutosha wa kimazingira uliowaunganisha warufani na tukio hilo.

Majaji walieleza kuwa ushahidi wa kimazingira unaweza kuthibitisha hatia endapo utaonyesha mnyororo usiovunjika wa matukio unaoelekeza kwa washtakiwa bila kuacha shaka yoyote. Katika kesi hii, walibaini kuwa mazingira yoteikiwa ni pamoja na kuwa watu wa mwisho kuonekana na marehemu, kuongoza polisi hadi mwili ulipokuwa, na kuhusishwa na pikipiki ya marehemu, mambo yalitosha kuthibitisha hatia yao.

Kutokana na tathmini hiyo, Mahakama ya Rufani ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi bila shaka yoyote. Hivyo, ilitupilia mbali rufaa ya warufani na kuthibitisha hukumu ya kunyongwa hadi kufa iliyotolewa na Mahakama Kuu.