Global Publishers
April 13, 2026
0 Comments
Jeshi la Marekani kupitia U.S. Central Command (CENTCOM) limetoa onyo kali kwa meli zote zinazosafiri katika eneo la Ghuba ya Uajemi, likisema kuwa yeyote atakayekiuka zuio la baharini dhidi ya Iran atakabiliwa na hatua za kijeshi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, meli yoyote itakayojaribu kuingia au kutoka katika eneo lililowekewa zuio bila kibali rasmi itazuiliwa, kuelekezwa upya au hata kukamatwa.
“Chombo chochote cha majini kinachoingia au kutoka katika eneo lililowekewa zuio bila idhini kinakabiliwa na kuzuiwa, au kukamatwa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Maafisa wawili wa Marekani wameeleza kuwa taarifa hiyo ilitolewa rasmi kwa mabaharia kabla ya kuanza kutekelezwa kwa zuio hilo, ikiwa ni tahadhari kwa vyombo vyote vya usafiri wa majini vinavyofanya kazi katika ukanda huo.

Hata hivyo, CENTCOM imefafanua kuwa zuio hilo halitazuia safari halali za kimataifa kupitia Strait of Hormuz kwa meli zisizohusiana na Iran.
Aidha, imesisitiza kuwa misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula, dawa na mahitaji mengine muhimu itaruhusiwa kupita, lakini itafanyiwa ukaguzi maalum kabla ya kuendelea na safari.
Zuio hilo linatajwa kuhusisha ukanda wote wa pwani ya Iran, hatua inayoongeza mvutano wa kisiasa na kijeshi katika eneo hilo muhimu kwa biashara ya mafuta duniani.
Hatua hiyo ya Marekani inaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kuishinikiza Iran, huku wadau wa kimataifa wakifuatilia kwa karibu athari zake katika usalama wa usafirishaji wa baharini na uchumi wa dunia.
