Zanzibar. Wito wa uwazi umeendelea kutolewa huku wengi wakisubiri ripoti za kitabibu, matokeo ya uchunguzi wa maiti na uwezekano wa mamlaka kutoa maelezo ya kina kuhusu mlolongo wa matukio hadi kifo cha mhamasishaji wa mitandao ya kijamii, Ashlee Jenae.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Benedict Mapujira, aliiambia Mwananchi uchunguzi wa awali unaonesha Ashlee (31) raia wa Marekani, amejiua mwenyewe, akiwa visiwani humo kuvinjari na mpenzi wake.
Kwa mujibu wa maelezo ya polisi, tukio hilo lilitokea Aprili 9, 2026, Ashlee anadaiwa kujaribu kujinyonga kwa kutumia kipande cha nguo kutoka katika vazi lake ndani ya kabati la chumbani katika hoteli aliyofikia.
“Ushahidi tulionao hadi sasa unaonesha kuwa marehemu alitumia kipande cha nguo kutoka kwenye vazi lake na kujinyonga ndani ya kabati,” amesema Kamanda Mapujira.
Ameongeza taarifa ya awali iliripotiwa Kituo cha Polisi Nungwi kama tukio la jaribio la kujiua, si kifo kilichothibitishwa moja kwa moja.
“Kwa mujibu wa taarifa, mwanamke huyo alikuwa na mtalii mwenzake na baadaye iligundulika kuwa alikuwa akijaribu kujitoa uhai katika chumba alichokuwa amekodi.”
“Baada ya taarifa kufikishwa polisi, hakuwa amefariki. Aliokolewa na kupelekwa hospitalini, lakini siku iliyofuata, Aprili 10, alipoteza maisha,”amesema kamanda huyo.
Amefafanua kuwa mwili bado upo nchini ukisubiri uchunguzi zaidi kabla ya mipango ya kusafirishwa kurejeshwa kwao kufanyika.
Polisi pia, walieleza marehemu alikuwa akisafiri na mchumba wake ambapo kulikuwa na kutoelewana baina yao.
“Walikuwa na tofauti, na uongozi wa hoteli uliamua kuwatenganisha vyumba, kila mmoja akawa na chumba chake,” amesema.
Amekataa wito wa kuchukuliwa hatua dhidi ya mchumba huyo akisema hakuna msingi wa kisheria wa kumzuia.
“Alikutwa akijaribu kujinyonga akiwa chumbani kwake, sasa ungemchukulia hatua gani mwanaume?” amehoji.
Hata hivyo, kwa familia ya marehemu, hitimisho la polisi halijamaliza maswali yaliyopo.
Katika taarifa yao ya Aprili 12, 2026, familia ilieleza kuwa, safari ya Zanzibar ilikuwa kwa ajili ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na uchumba mpya.
“Ashly alikuwa kwenye moja ya safari za furaha zaidi maishani mwake,” ilieleza taarifa hiyo.
Familia ilisema alipatikana akiwa hajitambui na kuwahishwa hospitali, ambako alithibitishwa kufariki saa chache baadaye.
Walieleza kuwa, tukio hilo ni la ghafla na gumu kueleweka, huku wakilitaja kuwa la kutia shaka na kuonya dhidi ya taarifa zisizothibitishwa.
Marafiki pia, walihoji maelezo ya polisi, wakitaka majibu zaidi kuhusu kilichotokea.
Pamoja na kauli ya polisi, bado kuna mapungufu katika maelezo ya muda wa matukio, ikiwemo tofauti ya lini hasa kifo kilithibitishwa.
Pia, haijaelezwa kwa kina mazingira ya chumbani, nani alitoa taarifa ya awali na hatua zilizofuata.
Maswali mengine yanahusu muda wa mgogoro kati ya wawili hao na lini walitenganishwa vyumba.
Aidha, hakuna taarifa za kina za kitabibu au uchunguzi wa maiti zilizotolewa hadharani kuunga mkono taarifa za kujiua.
Kutokana na hali hiyo, wito wa uchunguzi wa kina na wa uwazi umeendelea kuongezeka, huku baadhi ya watu wakihusisha muda wa tukio na hali ya maisha yake kabla ya kifo.