Dar es Salaam. Licha ya Serikali kusisitiza taasisi zenye watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi ya kupikia, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2024/25 imebaini mwamko bado ni mdogo.
Lengo la Serikali kusisitiza nishati safi kwenye Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) ni kuhakikisha asilimia 80 ya matumizi hayo ifikapo 2034, ili kusaidia utunzaji wa mazingira na kulinda afya ya jamii.
Hata hivyo, ripoti ya CAG ya ukaguzi ulioishia Juni 30, 2025, imebaini bado kuna shule 2,072 katika halmashauri 26 zenye wanafunzi zaidi ya 100, ambazo zinaendelea kutumia kuni au mkaa kwa maandalizi ya chakula cha wanafunzi, kinyume na mkakati wa nchi ulivyoelekeza.
Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni Aprili 10, 2026, jijini Dodoma, hali hiyo imesababishwa na uhaba wa rasilimali fedha katika shule, unaozuia uwezo wa kununua na kufunga majiko ya kisasa.
“Matumizi ya kuni na mkaa yana madhara makubwa kwa mazingira, afya, jamii na uchumi, ikiwa ni pamoja na ukataji wa miti, mabadiliko ya tabianchi, magonjwa ya njia ya hewa, na uchafuzi wa hewa ndani ya majengo unaoleta athari kwa afya,” imeeleza ripoti hiyo.
Ripoti hiyo hiyo imefafanua kuwa kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191, kinasema kuwa Waziri (anayehusika na mazingira) atakuwa na jukumu la jumla katika masuala yanayohusu mazingira na atawajibika kuandaa miongozo ya sera inayohitajika kwa ajili ya kuendeleza, kulinda na kusimamia mazingira endelevu nchini.
Machi 24, 2023, kupitia Gazeti la Serikali, ilitolewa agizo la kupiga marufuku matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi zote za umma na binafsi zinazopika chakula kwa watu zaidi ya 100 kwa siku, mchakato huo ulianza kutekelezwa Januari 31, 2024.
Hivyo, Ofisi ya CAG imependekeza Wizara ya Nishati na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuweka mipango inayohakikisha shule zinatumia nishati safi wakati wa kuandaa chakula.
“Msaada wa kifedha na uwekezaji katika miundombinu unapaswa kupewa kipaumbele ili kurahisisha matumizi ya nishati safi, hususani katika maeneo ya vijijini zaidi.
“Serikali inapaswa kuongeza uhamasishaji na kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji ili kuhakikisha utekelezaji wa sera za nishati safi shuleni unafanyika kwa ufanisi,” imeeleza.
