MWENGE WA UHURU 2026 WATEMBELEA MIRADI YENYE THAMANI YA SH.BILIONI 51.8 ILALA

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MWENGE wa Uhuru mwaka 2026 umeweka mawe umekagua  miradi saba katika Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam ikiwemo ya afya,elimu, Uwezeshaji wananchi ,barabara na maendeleo ya jamii ambayo imegharimu Sh.bilioni 51.8.

Katika mwenge wa uhuru 2026 kauli mbiu yake inasema “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo” ambapo maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Ilala wamejitokeza kwa wingi kushuhudia mwenge huo wakati ukitembelea miradi hiyo.

Akizungumza baada ya kutembelea,kukaguwa na kuweka mawe ya msingi katika miradi hiyo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 Kitaifa Wazo Mwang’onda amepongeza ujenzi wa miradi hiyo sambamba na kutoa baadhi ya maelekezo kwa viongozi wa Wilaya hiyo ikiwemo kuongeza matanki katika mradi wa kisima cha maji Mchikichini.

Mwenge wa Uhuru ulianza kwa kutembelea mradi mkubwa wa kitega uchumi cha DDC Kariakoo unaojulikana kama DDC Kariakoo One Stop Business Complex wenye thamani ya shilingi bilioni 36.7 ambapo mradi huo unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 4000.

Kwa mujibu wa taarifa ya mradi huo ni wa ubia kati ya Shirika la Maendeleo la Jiji la Dar es Salaam (DDC) na mwekezaji binafsi ambapo ujenzi huo umefikia asilimia 98 ya utekelezaji.

Ujenzi huo unahusisha jengo la ghorofa nane lenye zaidi ya maduka 1,016, ofisi, stoo na maeneo ya huduma mbalimbali ikiwemo benki na burudani.Mradi huo utawezesha  Shirika na Serikali kuongeza mapato ambapo kila mwaka itakuwa inapata  Sh. bilioni 2.500.

Mwenge wa uhuru pia uliweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Lindi yenye urefu wa kilomita 1.015 kwa kiwango cha lami ambayo ni sehemu ya maboresho ya barabara za Ilala CBD wenye thamani ya Sh. bilioni 23.5.

Mradi mwingine ni Kisima cha maji Ilala Mchikichini wenye thamani ya Sh. milioni 164.07 na kwa mujibu wa mradi huo unahusisha uchimbaji wa kisima kirefu cha mita 80, ujenzi wa mnara wa tanki la maji la lita 10,000 na usambazaji wa maji kwenye mtandao wa DAWASA.

Pia Mwenge ulikagua na kuweka jiwe la msingi Kituo cha Afya Mchikichini ambacho ujenzi wake utagharimu Sh.bilioni  7.45.Mradi huo ukikamilika unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 325,000 kutoka kata sita za Ilala na maeneo jirani, hivyo kupunguza msongamano wa wagonjwa katika vituo vingine vya afya.

Mradi mwingine uliotembelewa na Mwenge wa uhuru ni Shule ya Sekondari Kitunda Relini ambapo Mwenge uliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Kitunda Relini iliyojengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 4.21.Shule hiyo ya ghorofa itakuwa na madarasa 16, maabara nne za sayansi, maktaba na ofisi za walimu.

Wakati huo huo Mwenge wa Uhuru ulimalizia na mradi wa kituo cha Polisi Bonyokwa chenye thamani ya shilingi milioni 410.