Unguja. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amewaapisha wakuu wa wilaya aliowateua hivi karibuni huku wateule hao wakitaja vipaumbele vyao kwenye maeneo yao ya kazi.
Hafla ya kuwaapisha viongozi hao imefanyika leo Aprili 13, 2026 Ikulu Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, viongozi wa chama na vikosi vya ulinzi na usalama.
Walioapishwa ni pamoja Dk Said Haji Mrisho, Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja, Lailah Burhan Ngozi, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A Unguja na Ali Abdalla Said Natepe, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B.
Wengine ni Riziki Daniel Yussuf, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini Unguja na Zuhura Mgeni Othman, Mkuu wa Wilaya ya Chakechake, Pemba.
Wakizungumza baada ya kula kiapo, viongozi hao wamempongeza Rais wa Zanzibar kwa kuonyesha uaminifu wake kwao kuwapa nyadhifa hizo, ambazo ni kubwa kwa ajili ya kumsaidia kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na kufikia malengo yake.
Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, Lailah Burhan Ngozi amesema atahakikisha anakwenda kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni ambazo zimewekwa, akiamini kwa kushirikiana na watumishi wenzake watakwenda kufanikisha malengo yaliyokusudiwa katika wilaya hiyo.
Lailah amesema kwa vile ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na ilani ya chama ilikuwa inaelekeza nini Serikali ifanye hivyo, anahisi mtihani aliowatungia wenzake amepewa kuufanyia kazi na kuyatekeleza yote ambayo yamelekezwa katika wilaya husika.
“Ule mtihani niliowatungia wengine sasa naenda na mimi kuufanyia kazi, lakini kikubwa ni ushirikiano katika hili,” amesema.
Kwa upande wa migogoro ya ardhi, amesema jambo hilo haliepukiki hivyo atahakikisha anakwenda kulifanyia kazi kwa kusikiliza pande zote mbili kwani ndio itakuwa suluhisho.
Naye, Dk Said Haji Mrisho, Mkuu wa Wilaya ya Mjini, amesema atahakikisha anakisimamia kiapo alichokula na yale yote mazuri yaliyofanywa na viongozi waliopita atayasimamia na yale ambayo hayajafikiwa atahakikisha yanakamilika kwa ufanisi na wakati.
Ameahidi kuwa ataendelea kushirikiana na ngazi zote ili kuhakikisha wilaya hiyo inaendelea kuwa salama na kuangalia vyanzo vyote ikiwemo kuupanga na kusimamia suala la usafi wa mji.
“Tunakwenda kusimamia Baraza la Manispaa kuhakikisha wanasimamia majukumu yao, pia kuangalia vyanzo vya mapato ambavyo vitakuwa ni nguvu ya kusimamia usafi kwani usafi ni fedha,” amesema.
Hata hivyo, amesema katika kusimamia suala la usafi wataangalia utaratibu wa kutafuta kampuni zenye uwezo ili kuzisimamia ziweze kufanya usafi katika mji, kwani ndio kitovu kikuu cha utalii wa Zanzibar.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chakechake Pemba, Zuhura Mgeni Othman ameahidi kuifanyia kazi wilaya hiyo kwa kushirikiana na jamii na watendaji wengine ili kuhakikisha wilaya hiyo inaendelea kuwa mikono salama, na kufikia lengo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Mwinyi la maendeleo anayoendelea kuyapeleka katika wilaya hiyo.
Akizungumzia lengo la Rais Mwinyi kuifungua Pemba kiuchumi, amesema kutokana na nguvu kubwa zilizoelekezwa katika kisiwa hicho utalii utaimarika kwa kasi, hasa kutokana na utanuzi wa kiwanja cha ndege na ujenzi wa barabara.
Ali Abdalla Natepe ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B, amesema anafahamu kuwa ofisi ya mkuu wa wilaya inaongozwa kwa mujibu wa sheria na katiba na hivyo ndivyo vitakavyomuongoza katika utekelezaji wa majukumu yake.
Amesema Wilaya ya Magharibi B inakuwa kwa kasi na wilaya ya pili kimjini na inakabiliwa na changamoto nyingi, hivyo watahakikisha wanashirikiana pamoja katika kuzipatia ufumbuzi wake kwani kwenye maendeleo lazima changamoto zijitokeze.
Ameahidi kwamba atahakikisha anashirikiana na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi katika kutatua changamoto za ardhi zilizopo katika wilaya hiyo na kuona ardhi inatumika vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wa suala la usafi, amesema Baraza la Manispaa ndio wenye jukumu hilo hivyo akiwa kama msimamizi wao basi atahakikisha anawasimamia na kuona wanatatua changamoto zote ambazo zinazojitokeza.
“Jukumu langu ni kuhakikisha nashirikiana na waliopo kusimamia suala la usafi ili kuhakikisha wilaya inakuwa safi na kufikia malengo wanayotarajia.”