MZUMBE KUIMARISHA TAFITI NA UBUNIFU KWA KITUMIA AI

Na Farida Mangube, Morogoro

Chuo Kikuu Mzumbe kimezindua Kituo cha Tafiti na Ubunifu wa Akili Unde (CAIRI), hatua inayokuja wakati ambapo taifa linaongeza jitihada za kutumia teknolojia katika kuboresha elimu, tafiti na kukabiliana na changamoto za maendeleo.

Hafla hiyo imefanyika katika Kampasi Kuu ya Morogoro, ikiongozwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Petro, kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha. Hafla hiyo pia imehudhuriwa na wataalamu mbalimbali wa teknolojia, watafiti, washirika wa maendeleo kutoka Ubelgiji pamoja na wanafunzi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Hawa alisema dunia ipo katikati ya mapinduzi makubwa ya kiteknolojia yanayoendeshwa na AI hivyo vyuo vikuu haviwezi kubaki nyuma.

“Kituo hiki kitakuwa daraja kati ya maarifa, ubunifu na mahitaji halisi ya jamii,” alisema Prof. Hawa.

Alisema CAIRI itajikita katika tafiti zenye tija na ubunifu unaotekelezeka kwa ushirikiano kati ya serikali na sekta mbalimbali ili kuhakikisha teknolojia hiyo inaleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mratibu wa mradi huo, Dkt. Bokigwe Isagah, ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe, alisema lengo la mradi huo ni kufanya tafiti na bunifu zitakazowawezesha wanafunzi wa sayansi kutumia AI katika kutatua changamoto za jamii.

Alisema licha ya serikali kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu, bado kuna changamoto, hivyo chuo kimeona ni muhimu kutumia Akili Mnemba kama suluhisho la kusaidia kuboresha ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za kielimu katika jamii.

Mwakilishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Othman Mohamed, alisema uzinduzi wa kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati mpana wa taifa wa kuingia katika uchumi wa kidijitali.

“Akili Mnemba tayari inabadilisha dunia kuanzia elimu, afya, kilimo hadi usalama wa taifa. Tanzania haina budi kuwa sehemu ya mabadiliko hayo,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali inaendelea kuandaa mkakati wa kitaifa wa AI, sambamba na kuimarisha matumizi ya teknolojia hiyo katika sekta ya elimu kupitia uboreshaji wa miundombinu ya TEHAMA na kuweka miongozo ya matumizi sahihi ya teknolojia hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ubunifu, Utafiti na Maendeleo wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Evodius Kanyamyoga Marco, alisema uzinduzi wa CAIRI unaendana moja kwa moja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuijenga Tanzania kuwa uchumi unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia.

Alisema katika kipindi cha awali cha utekelezaji wa dira hiyo, serikali inaweka mkazo katika matumizi ya teknolojia kama kichocheo cha uzalishaji, ajira na ushindani wa kiuchumi.

“Hatuwezi kufikia malengo ya Dira 2050 bila kuwekeza kwa nguvu katika sayansi, teknolojia na ubunifu. Kituo hiki ni hatua ya vitendo kuelekea huko,” alisisitiza.

Mwalimu Debora Maliango kutoka Shule ya Msingi Mzumbe ameishukuru Wizara ya Elimu kupitia Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuanzisha mradi huo, akisema umeongeza hamasa ya wanafunzi kujifunza na kupunguza utoro shuleni.

Alisema tangu kuanza kutumika kwa Akili Mnemba katika somo la hisabati shuleni hapo mwaka 2024, imeisaidia kurahisisha ufundishaji kwa walimu na kuboresha ufaulu wa wanafunzi. Aidha, alieleza kuwa endapo utaendelezwa zaidi, mradi huo una uwezo wa kuleta mageuzi makubwa katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.

“Hapo awali ilikuwa vigumu kuwavutia watoto darasani, lakini sasa wana hamu ya kujifunza, wanashiriki zaidi, na hata utoro umepungua kwa kiasi kikubwa,” alisema.