NGUVU YA PAMOJA YATAKIWA KATIKA MAFANIKIO YA DHANA YA AFYA MOJA – DKT. MANYATTA

Na, Mwandishi Wetu – Korogwe, Tanga

Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Afya Moja kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Salum Manyatta, amesema kuwa Mpango Mkakati wa Afya Moja umejikita kuhakikisha wananchi wananufaika kuanzia ngazi ya  Kaya hadi Taifa kupitia utekelezaji shirikishi wa sekta mbalimbali nchini ili kuhakikisha malengo yake yanafikiwa na kuwa na tija kwa jamii kwa ujumla.

Dkt. Manyatta ameyasema hayo Aprili 13, 2026 mkoani Tanga wakati wa kikao kazi cha wataalam cha kuandaa Mpango wa Mkoa wa Afya Moja kilichoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sehemu ya Afya Moja kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Serikali la CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani.

Amesema kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kuwajengea uwezo Watalamu ngazi ya mkoa kuhusu utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja na kuwawezesha kutengeneza Mpango wa Utekelezaji wa Afya Moja wa Mkoa ambacho kitafanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 13 hadi 17 Aprili 2026 katika Halmashauri ya Mji wa Korongwe, Mkoani Tanga.

Dkt. Manyatta ameeleza kuwa, lengo la dhana ya Afya Moja ni kupanua na kuimarisha ushirikiano baina ya sekta/taaluma mbalimbali katika hatua zote za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na hatari nyingine za afya zinazohitaji ushiriki wa sekta zaidi ya moja na taaluma mbalimbali.

“Ushirikiano huu pamoja na wadau wengine ikiwemo jamii, kimsingi unaongozwa na sekta/wizara za msingi (lead Ministries) ambazo ni Afya ya Binadamu, Wanyama (Mifugo na Wanyama Pori), Mazingira na Kilimo katika ngazi zote,” alifafanua Dkt. Manyatta.

Alifafanua kuwa, uwepo wa Mpango Mkakati ni muhimu kwani unatarajiwa kuweza kujibu na kutatua changamoto zilizopo katika Mkoa wa Tanga, hivyo utumike kama fursa ya kuhakikisha mkoa unakuwa na uelewa wa pamoja wa masuala ya Afya Moja kwa kuunganisha nguvu ya pamoja na kuweza kufanya kazi pamoja kwani hii ndiyo maana halisi ya dhana ya Afya Moja.

Naye Mwakilishi wa Katibu Tawala, ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Japhet Simeo amepongeza uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna inavyoendelea kutoa elimu ya masuala ya Afya Moja, na kueleza kuwa mkoa wa Tanga utanufaika kwa uwepo wa Mpango Mkakati wa Afya Moja na kusisitiza kuwa Tanga itautekeleza kwa vitendo na kufanya mkoa  huo kuwa wa mfano 

“….Ifike mahali tutoke katika mambo ya concept to Action, yaani kuwa na mipango na mikakati ya namna hii na kuitekeleza na hiyo ndiyo umuhimu wa dhana Afya Moja,” alisisitiza Dkt. Simeo

Kwa upande wake, Msimamizi wa  Afya Moja na Mratibu wa Mradi wa Usalama wa Afya Duniani unaotekelezwa na Shirika lisilo la Serikali la  CIHEB Tanzania Dkt. Irene Massawe amesema kuwa, ushirikiano uliopo utasaidia kufanikisha malengo yaliyopo kwa nguvu ya pamoja na kuhakikisha matarajio ya uwepo wa mpango huo yanafika hadi ngazi za chini.

Aliongezea kuwa, sekta husika zikiungana kwa pamoja katika kutekeleza dhana ya Afya Moja itasaidia kudhibiti vihatarishi vya afya ikiwemo magonjwa ya mlipuko hasa yale yanayoweza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, yakiwemo ya kimeta, kichaa cha mbwa kwani itarahisisha na kuleta ufanisi katika kukabiliana na changamoto hizo.

“Tunaamini kuwepo kwetu ndani ya siku tano hizi Korogwe kutazaa matunda kwa washiriki wote kisha kuyaleta haya katika utekelezaji wa kila siku na kuhakikisha tunaleta matokeo chanya  ya mipango hii,” alisema Dkt. Irene.

AWALI

Afya Moja ni Dhana ya Kimataifa iliyoridhiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (OIE), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Programu ya Kimataifa ya Mazingira (UNEP) kupitia “Global Health Security Agenda” (GHSA) na wadau wengine wa Afya duniani kote.

 Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (OIE) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) yamekuwa yakishirikiana duniani kote na kutoa wito kwa wataalamu wa sekta za Afya ya Binadamu, Wanyama na Mazingira kuongeza na kuimarisha ushirikiano na mawasiliano ili kuboresha ufanisi katika kukabiliana na tishio la magonjwa ya kuambukiza yanayoenea kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na yanayovuka mipaka; tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa na changamoto zingine zinazokabili afya ya jamii zinazohitaji nguvu ya pamoja.