Nyota Man United atia mkono Dodoma JIJI

TANZANIA inatarajiwa kupokea ugeni mzito siku chache zijazo baada ya kuthibitishwa ujio wa zaidi ya maskauti 10 kutoka Ulaya wakiwemo wawili kutoka Sweden huku nyota wa zamani wa Manchester United, Febian Brandy akifuatilia kwa karibu.

Brandy ambaye kituo chake huko Manchester, England kina vijana wawili wa Kitanzania, Gwakisa Mwakipesile na Calvin Mushi anatarajiwa kufuatilia kitachokuwa kinaendelea nchini  katika tukio la ‘AYE 2026 scouting series’ mahususi kwa ajili ya kutafuta vipaji vya soka.

Waswideni hao ni Tesfaye Berhane Nahom na Jamal Daniel samue. Tukio hilo linatarajiwa kufanyika Aprili 29 hadi Mei 2, 2026 Kwenye viwanja vya Don Bosco, Dodoma likiwa na kauli mbiu ya ‘Nyota Ajaye ni Wewe’ ikiwa ni mpango maalum kuhakikisha Tanzania inakuwa na wachezaji wengi wa kulipwa Ulaya kama ilivyo kwa mataifa ya Magharibi na Kaskazini mwa Afrika.

Taarifa kutoka kwa waandaaji zinaeleza maskauti hao zaidi ya 10 watatoka katika nchi mbalimbali za Ulaya, wakiwa na uzoefu wa kufanya kazi na akademi na klabu kubwa barani humo.

Kila mmoja atakuwa na jukumu la kuchambua vipaji hivyo kuanzia uwezo wa kiufundi, kasi ya mchezo, akili ya uwanjani, hadi uwezo wa mchezaji kuhimili presha ya mchezo wa ushindani.

Ujio huu unalenga kuleta mfumo wa kisasa wa ufuatiliaji wa vipaji Tanzania na mchezaji hatapimwa tu kwa kufunga mabao au kutoa pasi za mwisho, bali pia kwa mchango wake katika timu, nidhamu ya mchezo na uwezo wa kujifunza haraka.

Brandy ambaye anatajwa kuwa sehemu ya projekti hiyo, ana mtandao mpana wa kimataifa unaounganisha wachezaji chipukizi na maajenti pamoja na klabu mbalimbali za Ulaya, jambo linaloongeza uzito wa tukio hilo.

NYO 02

AYE 2026 Scouting Series imeelezwa ni hatua muhimu katika kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa ya soka la vijana, hasa katika mfumo wa kisasa wa utafutaji wa vipaji (modern scouting system).

Kwa miaka ya hivi karibuni, mataifa ya Afrika Magharibi na Kaskazini yamekuwa yakiongoza kwa kutoa wachezaji wengi wa kulipwa Ulaya kutokana na mifumo yao imara ya akademi na fursa za wachezaji hao kutazamwa.

Hata hivyo, mpango huu unalenga kubadilisha taswira hiyo kwa Afrika Mashariki, kwa kuifanya Tanzania kuwa moja ya vituo vipya vya kuzalisha vipaji vinavyoweza kushindana kimataifa.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa AYE, Gerald Muyimba anasema;

“Haya ndiyo yatakuwa maisha yetu, kila baada ya kipindi fulani tutaleta watu kwa ajili ya kuona  Tanzania ilivyobarikiwa kuwa na vipaji, hii siyo mara yetu ya kwanza ni muendelezo wa kuhakikisha tunakuwa na kina Mbwana Samatta wengine tena kwa wingi.”

Anasema: “Vijana ambao watapatikana watapata nafasi ya kwenda Ulaya katika mashindano ya timu vijana, hiyo itakuwa ni fursa nyingine kubwa zaidi kuonekana, naamini tutafanikisha hili ambalo linatunyima usingizi, kuifanya Tanzania kuwa na wachezaji wengi nje ya nchi.”

Kuhusu Brandy, Muyimba anasema: “Tunaamini siku moja atakuja nchini na kuwa sehemu ya jambo hili, hatutakuwa naye Dodoma lakini atashirikiana nasi kwa njia ya mtandao kwa sababu ni kati ya watu muhimu sana kwetu.”

Moja ya vipengele muhimu vya programu hii ni kutoa nafasi kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 18 ambao wataanza safari ya kupigania ndoto zao mapema wakiwa katika uangalizi maalum huko Ulaya.

Mmoja wa wadau wa soka la Tanzania, Antony Ngailo ambaye anaishi England aliwapokea wachezaji wawili wa Kitanzania, Gwakisa na Calvin kwa ajili ya uangalizi wa karibu kutokana na vijana hao kuwa chini ya umri wa miaka 18, ameongelea fursa hiyo.

“Najua ni suala la muda ila naamini siku moja Tanzania itakuwa moja ya mataifa makubwa sana ya mpira Afrika kwa sababu tunao vijana wengi wenye vipaji, nimeona vile ambavyo Gwakisa na Calvin wanachofanya na sina shaka kabisa baada ya miaka michache watakuwa msaada kwa taifa.”

“Natamani kuona vijana wengine sasa mfano wengine 10 wakiwa Hispania, watano labda wawe Italia, nane wawe Uholanzi, sita wawe Ufaransa sasa hawa wachezaji wakifikisha miaka 20 hadi 23 na Mungu akisaidia tukipata 10 hadi 13 ambao wameiva na wanacheza kwenye ngazi za juu kwenye mataifa yao tunaweza kuwa kama DR Congo, wameliheshimisha taifa lao kwa kuwa miongoni mwa nchi ambazo zimeenda Kombe la Dunia,” anasema.

NYO 01

Mpango huu pia unaunganishwa na mashindano makubwa ya kimataifa ya vijana kama Gothia Cup (Sweden), Dana Cup (Denmark) na Girona Cup (Hispania) ambayo ni miongoni mwa mashindano yenye heshima kubwa duniani katika soka la vijana. 

Mashindano hayo yamekuwa yakivutia timu na akademi kubwa kutoka duniani kote.

Miongoni mwa timu kubwa ambazo zimewahi kushiriki au kutuma vijana wao katika mashindano hayo ni pamoja na akademi za klabu kama FC Barcelona, Manchester United, Arsenal, Ajax, Bayern Munich na Paris Saint-Germain.

Kutokana na ushirikiano huu, vipaji vitakavyobainika Tanzania vitapata nafasi ya moja kwa moja ya kushiriki kwenye mashindano hayo, jambo litakalowapa uzoefu wa kimataifa, kujifunza nidhamu ya soka la kiwango cha juu na kuongeza nafasi za kusajiliwa na klabu kubwa za Ulaya.