Babati. Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara limewakamata watu 19 kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo ulawiti na kujihusisha na dawa za kulevya, kutokana na operesheni, doria na misako iliyofanyika mwezi uliopita.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani, ameeelza hayo leo Aprili 13, 2026 mjini Babati, Manyara, alipozungumzia matukio yaliyotokea katika maeneo mbalimbali mkoani humo.
Kamanda Makarani ameeleza kwamba operesheni hizo zililenga kuzuia na kubaini uhalifu ili kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku kwa amani na utulivu.
Amesema watuhumiwa watatu wamekamatwa wakiwa na vitu mbalimbali vya wizi, ikiwemo pikipiki tatu aina ya King Boss na King Lion zisizo na namba za usajili, pamoja na vifaa vingine.
Amesema watuhumiwa wengine watatu wamekamatwa wakiwa na kilogramu 2.16 za bangi na misokoto 95, huku wawili wakikamatwa na lita 25 za pombe haramu aina ya gongo.
Katika hatua nyingine, amesema madereva wawili wamekamatwa kwa kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa na kusababisha ajali.
Kamanda Makarani ameeleza ajali hiyo ilisababisha majeruhi na vifo, huku watuhumiwa wawili wakikamatwa wakiwa na nyara za Serikali, zikiwemo wanyamapori mbalimbali.
“Vilevile, watuhumiwa watano walikamatwa kwa kosa la kujeruhi, mmoja kwa kulawiti mwanafunzi, na mwingine kwa kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire bila kibali,” amesema Kamanda Makarani.
Ametoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu na kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kudhibiti uhalifu, hususan biashara ya dawa za kulevya.
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Manyara wamepongeza jitihada za polisi kushirikisha jamii katika kupiga vita uhalifu.
Mkazi wa kata ya Bonga, Hanzuruni Swaleh, ameeleza polisi kupitia dhana ya polisi jamii na ulinzi shirikishi imekuwa chachu ya kupambana na uhalifu.
“Sasa hivi hata ukitoa taarifa za uhalifu katika vituo vya polisi hautangazwi, inakuwa siri na motisha kwa jamii kutoa taarifa za uhalifu kwani wao ndiyo wanaoishi nao na wanawatambua,” amesema.
