KUTOKA hatua za mwanzoni hadi sasa tunapoizungumzia robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, zimebaki timu nane huku tukitarajia kushuhudia vita ya wakubwa pekee.
Vita hiyo ya wakubwa inazihusisha timu za Ligi Kuu Bara pekee baada ya mchujo mkali kupita kuanzia hatua za awali, 64 bora, 32 bora na 16 bora ambayo imehitimishwa wikiendi iliyopita.
Baada ya kushuhudia timu nane zikijikatia tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali itakayochezwa Mei 16 na 17 mwaka huu, kifuatacho ni kusubiri ratiba yake itakuwaje.
Timu nane zilizofuzu hatua ya robo fainali, ni Mashujaa iliichapa Geita Gold kwa penalti 4-2, baada ya suluhu (0-0) dakika 90, ikifuatiwa na JKT Tanzania iliyokata tiketi hiyo kwa kuichapa Mbuni FC ya Arusha mabao 3-0.
Coastal Union chini ya benchi jipya la ufundi linaloongozwa na Fikiri Elias, aliyerithi mikoba ya Mohamed Muya, imefuzu baada ya kuifunga Pamba Jiji bao 1-0, huku Yanga ikiichapa TMA ya Arusha 1-0.
Timu nyingine zilizofuzu ni Simba iliyoigeuzia kibao Dodoma Jiji na kutoka nyuma ya bao 1-0, hadi ushindi wa mabao 3-1, huku Singida Black Stars, ikiitembezea kichapo Mbeya City cha mabao 5-1, wakati TRA United ikiifunga Namungo mabao 2-0.
Azam FC ilihitimisha hesabu kwa kuifunga Fountain Gate mabao 4-0, ikiwa ni ushindi mkubwa kwa kikosi hicho tangu kimeshiriki michuano hiyo ya CRDB msimu wa 2025-2026.
Wakati timu nane zikifuzu kucheza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa kina kuhusu kile kilichojitokeza, rekodi mbalimbali zilizoandikwa na kinachosubiriwa kutokana na ushindani ulioanza kuonekana.
Ushindi wa bao 1-0 ilioupata Yanga, Aprili 11, 2026 dhidi ya TMA FC ya Arusha, lililofungwa na Maxi Mpia Nzengeli, umeifanya timu hiyo kufikisha mechi 27 za Kombe la CRDB bila ya kupoteza.
Mara ya mwisho Yanga kupoteza mechi katika michuano hiyo ilichapwa bao 1-0 na Simba, lililofungwa na Mganda, Taddeo Lwanga, katika fainali ya msimu wa 2020-2021, iliyopigwa Julai 25, 2021 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Tangu Julai 25, 2021 hadi Aprili 11, 2026, Yanga imefikisha siku 1,721, bila ya kupoteza, sawa na miaka minne, miezi nane na siku 17.
Mtihani uliopo kwa wapinzani ni jinsi watakavyoweza kuvunja rekodi ya Yanga ambao ni mabingwa mara nne mfululizo wa mashindano hayo, baada ya kuchukua taji hilo kuanzia msimu wa 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024 na 2024-2025.
Katika timu nane zilizofuzu hatua ya robo fainali, nne zinatafuta rekodi mpya ndani ya michuano hii, kwani hazijawahi kutwaa ubingwa huo, ambazo ni Mashujaa, Coastal Union, Singida Black Stars na TRA United.
Timu nne tu kati ya nane zilizochukua ubingwa huo ambazo zimefuzu robo fainali ni Yanga ambao ni mabingwa wa kihistoria tangu mwaka 1967, ikifuatiwa na Simba pia ambayo mara ya mwisho kuchukua taji hilo ni msimu wa 2020-2021.
Azam FC, inasaka pia taji hilo kwa mara ya pili, baada ya kulichukua msimu wa 2018-2019, ilipoichapa Lipuli FC ya Iringa bao 1-0, katika fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi.
JKT Tanzania ilichukua taji hilo mwaka 2002, ikijulikana kwa jina la JKT Ruvu, ambao ulikuwa ni wa mwisho kwa michuano hiyo kufanyika ikifahamika kama Kombe la FAT, kisha kurejea mwaka 2015 na kuitwa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na sasa ni Kombe la Shirikisho la CRDB.
Singida Black Stars iliyofika fainali msimu uliopita wa 2024-2025 na kukosa ubingwa baada ya kuchapwa na Yanga mabao 2-0, itakuwa na kibarua cha kupigania ubingwa huo kama ilivyo pia kwa JKT Tanzania iliyoishia hatua ya nusu fainali msimu uliopita baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Yanga.
Kwa mara ya kwanza msimu huu, hatutashuhudia timu kutoka Ligi ya Championship katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, baada ya miamba inayotamba kwa sasa, Geita Gold, Kagera Sugar, Mbeya Kwanza, Transit Camp na Polisi Tanzania kutolewa.
Katika hatua ya 16 bora, zilikuwa timu tatu za Championship, ikianza Geita Gold iliyochapwa na Mashujaa, kisha TMA FC kutoka Arusha ikichapwa na Yanga bao 1-0.
Mbuni ya Arusha, ilihitimisha safari ya vigogo wa Ligi ya Championship katika michuano hiyo kwa kuchapwa na JKT Tanzania mabao 3-0, ikiwa ni tofauti na msimu uliopita wa 2024-2025, ambapo mbili zilitinga hadi robo fainali.
Mbeya City ambayo kwa sasa inacheza Ligi Kuu Bara, msimu uliopita 2024-2025 ikiwa inashiriki Championship, ilifika robo fainali ya Kombe la CRDB, ikachapwa na Simba mabao 3-1, Aprili 13, 2025.
Timu nyingine ya Championship iliyofika robo fainali msimu wa 2024-2025 ni Stand United, nayo ilihitimisha safari yake baada ya kuchapwa na Yanga mabao 8-1, Aprili 15, 2025.
MABINGWA KUANZIA KOMBE LA FAT HADI CRDB
9 Yanga (1967, 1974, 1998, 2001, 2015-2016, 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024, 2024-2025)
4 Simba (1995, 2016-2017, 2019-2020, 2020-2021)
2 Mtibwa Sugar (2000, 2017-2018)
Tanzania Stars (1997, 1998)