Rostam anunua kampuni inayoendesha mradi wa gesi Songo Songo

Dar es Salaam. Mfanyabiashara, Rostam Azizi kupitia kampuni yake ya Taifa Gas Tanzania Limited, kwa kushirikiana na Amber Energy Investment L.L.C-FZ, wameingia makubaliano ya kununua biashara ya gesi ya kampuni ya Orca Energy Group nchini Tanzania inayomiliki mradi wa Songo Songo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu, Aprili 13, 2026, Orca imesaini makubaliano ya mwisho ya ununuzi wa hisa (Share Purchase Agreement) na wanunuzi hao, ambapo itauza hisa zote za kampuni yake tanzu ya PanAfrican Energy Corporation (PAEM), inayomiliki shughuli zake zote za gesi nchini Tanzania.

Chini ya makubaliano hayo, Taifa Gas itanunua asilimia 49 ya hisa za PAEM huku Amber Energy ikichukua asilimia 51, hatua itakayokamilisha uhamisho wa umiliki wa mradi wa gesi wa Songo Songo kwenda kwa wawekezaji hao wapya.

Kulingana na taarifa hiyo Bodi ya Wakurugenzi ya Orca imeeleza uamuzi wa kujiondoa kwenye biashara ya Tanzania umetokana na tathImini ya muda mrefu ya hatari na changamoto zinazokabili shughuli zake nchini.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na migogoro inayoendelea, madai mbalimbali, pamoja na kutokuwa na uhakika wa hatIma ya kuongeza muda wa leseni ya maendeleo ya Songo Songo na mikataba ya kugawana uzalishaji (PSA).

Kutokana na hali hiyo, Orca iliona kuendelea kubaki nchini kungehitaji kuwa na akiba kubwa ya fedha ili kukabiliana na majukumu yasiyo na uhakika, ikiwa ni pamoja na uwekezaji mkubwa wa mitaji, gharama za maendeleo ya miradi, pamoja na kesi za kisheria na usuluhishi ambazo matokeo yake hayana uhakika na yanaweza kuchukua miaka mingi.

Kwa mantiki hiyo, bodi ya kampuni imeona kuwa kuuza biashara hiyo ni njia bora ya kulinda masilahi ya wanahisa wake na kuhifadhi fedha, sambamba na kutekeleza mkakati wake wa muda mrefu wa kupata thamani ya uwekezaji wake nchini Tanzania kwa njia iliyopangwa.

Akizungumzia makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Taifa Group, Rostam Azizi, amesema mkataba huo ni hatua muhimu kwa Tanzania na matumaini yake ni kuwa itachochea ushiriki mpana zaidi wa Watanzania katika sekta ya uchimbaji, huku akitoa wito kwa Serikali kuweka mifumo rafiki ya uwekezaji.

“Tumefanya kazi kwa bidii kwa miaka kadhaa kufanikisha jambo hili, na tunajivunia kwamba sasa Taifa Gas itakuwa na nafasi kubwa katika kuunda mustakabali wa sekta ya nishati ya nchi yetu,” amesema.

Ameongeza kuwa mradi wa Songo Songo una thamani kubwa kwa Tanzania, akisema umeleta thamani halisi kwa Tanzania, mapato ya Serikali, upatikanaji wa nishati ya ndani, ajira, maendeleo ya ujuzi, manunuzi ya ndani na uwekezaji wa muda mrefu.

“Kuongezeka kwa umiliki wa Watanzania kunapanua faida hizi, kunaimarisha uwezo wa viwanda na kuhakikisha faida zinabaki nchini, jambo linalounda utajiri kwa wote.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Orca, David Ross, amesema Mradi wa Songo Songo umekuwa hatua ya kihistoria kwa Tanzania na Orca huku akibainisha mambo kadhaa ambayo anayataja kuwa ni mchango wao katika maendeleo ya sekta ya gesi.

“Mradi huu umefungua enzi ya gesi asilia Tanzania, kusaidia uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi, usambazaji wa nishati kwa viwanda, na kujenga wataalamu wenye ujuzi mkubwa nchini,”

Hata hivyo Ross, alisisitiza kuwa muda umefika kwa mabadiliko na anaamini kuwa huu ni wakati sahihi wa kuhamisha mradi huu kwa utaratibu kwenda hatua inayofuata ya maendeleo yake.

“Kupitia Taifa na washirika wake, tunaona kundi lenye uzoefu wa uendeshaji, mwelekeo wa sekta na dhamira ya muda mrefu kwa Tanzania, litakaloweza kuendeleza mradi huu mbele zaidi,” amesema Ross.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Orca itauza hisa zake zote za PAEM kwa bei ya mfano ya dola 10 za Marekani, mbali na masharti mengine ya kimkakati na kibiashara yaliyokubaliwa.

Kabla ya kukamilika kwa mauzo hayo, Orca inaweza kulipwa madeni inayodai kutoka kwa kampuni zake tanzu, na pia inaweza kugawa gawio kwa wanahisa wake kulingana na masharti ya kifedha.

Aidha, Orca itapata asilimia 50 ya mapato yoyote ya ziada yatakayopatikana kati ya muda wa kusaini na kukamilika kwa makubaliano hayo.

Baada ya kukamilika kwa mauzo hayo, Orca haitakuwa tena na umiliki wowote katika biashara ya gesi nchini Tanzania, wala haitakuwa na wajibu wowote kuhusiana na matokeo ya baadaye ya leseni ya Songo Songo au migogoro yoyote na Serikali.

Aidha, kukamilika kwa makubaliano hayo kunategemea idhini kutoka kwa Tume ya Ushindani (FCC), Waziri mwenye dhamana nishati, wanahisa wa Orca, pamoja na mamlaka nyingine za udhibiti. Orca imeeleza kuwa itaitisha mkutano maalumu wa wanahisa wake ili kupiga kura kuidhinisha makubaliano hayo.

Kupitia kampuni yake tanzu ya PanAfrican Energy Tanzania Limited (PAET), Orca ilikuwa inamiliki haki zote za mradi wa gesi wa Songo Songo, ikiwa ni pamoja na mikataba ya uzalishaji, makubaliano ya masoko ya gesi na mali nyingine zinazohusiana na mradi huo.

Hata hivyo, kampuni imeeleza kuwa kwa kuzingatia hali ya mali hizo, thamani yake halisi kwa sasa ni ndogo kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo taarifa zote za kijiolojia zinamilikiwa na Serikali, na mali nyingi za kudumu zitarejea kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) baada ya leseni kuisha.