Sare ya New King yaishtua Kipanga 

KOCHA wa Kipanga, Khamis Makame ‘Kocha Meki’ amesema bado timu hiyo ina kazi ya kurekebisha upungufu uliojitokeza kwenye mechi dhidi ya New King iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Mechi hiyo ilichezwa Aprili 10, 2026 kwenye Uwanja wa Mao B, kisiwani Unguja na kocha huyo amesema sababu ya kupata sare hiyo ni wachezaji kupoteza umakini baada ya kwenda mapumziko wakiongoza 1-0.

Amesema, licha ya matokeo hayo jambo kubwa analolichukua ni kumalizika salama kwa mechi hiyo bila ya kuumia kwa mchezaji yeyote.

“Jambo ambalo nashukuru ni kumaliza mechi bila ya kuwa na majeruhi kwani afya ya wachezaji ni kipaumbele kikubwa kwa timu,” amesema.

Hata hivyo, amesema wachezaji walipoteza umakini kwa baadhi ya vipindi vya mechi, hali iliyowapa nafasi wapinzani wao kurudi mchezoni na kusawazisha mabao hayo.

Amesema katika mchezo huo, amebaini timu inashindwa kurudi kwenye muunganiko kwa haraka kujibu mashambulizi wanapopoteza mpira, huku akiahidi kulifanyia kazi tatizo hilo kwenye uwanja wa mazoezi.

Aliongezea, licha ya sare hiyo, timu bado inaendelea vizuri katika ligi huku akibainisha hawajakata tamaa kwenye harakati za kujiweka katika nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo.

“Vijana wanaendelea kuimarika na viwango vyao vinaongezeka, tunaamini tukirekebisha makosa haya tutapata matokeo mazuri zaidi katika michezo ijayo,” alisisitiza.

Kwa sasa Kipanga ipo nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 36, huku KVZ ikiongoza na pointi 43, baada ya mzunguko wa 22 kumalizika.