Serikali yaeleza dhamira yake kusukuma mtangamano wa EAC

Arusha. Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Joseph Ntakirutimana amemtwisha mzigo wa kushughulikia changamoto zinazolikabili Bunge hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, James Ole Millya katika vikao vya Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa sababu zimekuwepo kwa muda mrefu.

Amesema hayo leo Jumatatu, Aprili 13, 2026 wakati wa kikao maalumu cha Bunge la tano baada ya Naibu Waziri huyo kula kiapo cha utii kwa Bunge hilo, kwenye mkutano unaofanyika makao makuu ya jumuiya hiyo jijini Arusha  kwa njia ya mtandao.

“Mheshimiwa Ole Millya sio mgeni katika Bunge la tano, tulikua naye akiwa mbunge mwenzetu, aliamua kugombea ubunge kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana na kushinda, kisha kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa wizara inayoshughulikia EAC, tunaamini unazifahamu changamoto zinazotukabili na kwenye vikao vya baraza vya mawaziri mtazifanyia kazi,” amesema Ntakirutimana.

Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Joseph Ntakirutimana akiongeza kikao cha bunge maalumu jijini Arusha.

Ameongeza kuwa Bunge hilo linajivunia hatua aliyofikia Ole Millya na litampa ushirikiano unaostahili ili atekeleze majukumu yake katika nafasi ya kuwa mjumbe kwenye Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki, chombo chenye uamuzi wa kisera katika kusimamia jumuiya hiyo.

Katika hotuba yake baada ya kuapishwa, Ole Millya amesema Tanzania ikiwa mwanachama mwaminifu wa EAC itaendelea kutekeleza wajibu wake mkuu wa kusukuma juhudi za mtangamano ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.

Amesema Waziri wa Mambo Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Thabit Kombo anaamini ushirikiano wa nchi wanachama ni nguzo muhimu katika kukuza malengo ya kuanzishwa kwa EAC.

“Mtakumbuka kabla kushika nafasi hii nilikua mbunge wa Bunge hili ambalo nilifurahi kufanya kazi pamoja nanyi, nimefurahi kurudi tena na ninaahidi nitajitolea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha tunakua na jumuiya bora.

“Ninatambua umuhimu wa Bunge hili maalumu, nina ahidi kutimizia wajibu wangu wa kuhakikisha Eala inakua chombo cha kusimamia ajenda ya mtangamano,” amesema Ole Millya.

Ameongeza kuwa shughuli za Eala zinategemea michango kutoka nchi wanachama na hivi karibuni vikao vya Bunge hilo havikufanyika kutokana na ukata wa kifedha, hatua inayosababishwa na nchi wanachama kutokuwasilisha michango ya fedha kwa wakati ili kuwezesha shughuli za EAC kufanyika.

Wakati huohuo, mbunge wa Eala kutoka Sudan Kusini, Ayason Kennedy ameomba Bunge hilo kuzingatia hali ngumu ya wabunge wanayopitia ya kutolipwa mishahara kwa kipindi cha miezi sita, hatua inayokwamisha utendaji kazi wao.

“Tunafahamu nchi wanachama ambazo hazitoi michango yao zinakwamisha shughuli za Bunge na jumuiya kwa ujumla, wapo wabunge walichukua mikopo benki wakitegemea mishahara yao itumike kulipa mikopo. Kadiri siku zinavyoendelea bila kulipwa, riba zinaongezeka,” amesema Kennedy.

Akijibu hoja hiyo, Spika Ntakirutimana amesema Tume ya Uongozi ya Bunge hilo imejadili kwa kina hoja hiyo ambayo iliwasilishwa kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri kinachoshughulikia fedha na utawala na kutoa mapendekezo ambayo yatafanyiwa kazi na baraza la mawaziri.