Shauri la Kikatiba la kufungwa Jamii Forums sasa mguu sawa

Dodoma. Jopo la majaji watatu wanaosikiliza shauri la kikatiba la kupinga kufungiwa leseni kwa mtandao wa Jamii Forums kwa siku 90, limetupa ombi la kuitwa ili kuulizwa maswali ya dodoso, Ofisa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Ofisa huyo, Philip Filikunjombe, ndiye aliyewasilisha kiapo kinzani kwa niaba ya mlalamikiwa wa pili, TCRA na wa tatu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) katika shauri hilo lililofunguliwa na msomaji wa Jamii Forums, Fortnatus Buyobe.

Katika shauri hilo la kikatiba linalosikilizwa na majaji watatu, Arnold Kirekiano, Dk Lilian Mongela na Hadija Kinyaka wa Mahakama Kuu, masjala Kuu Dodoma, Buyobe ameiunganisha kampuni ya Vapper Tech Limited inayomiliki Jamii Forums.

Vapper Tech Limited anayewakilishwa na wakili Peter Majanjala ni mlalamikiwa wa kwanza katika shauri hilo ambalo Buyobe anawakilishwa na wakili John Seka huku TCRA na AG akiwakilishwa na wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Webiro.

Uamuzi huo wa kuyatupa maombi ya kuitwa kwa Ofisa huyo wa TCRA ili kuulizwa maswali ya dodoso (Cross Examinations) na wakili Seka kwa niaba ya Buyobe, umetolewa Aprili 9,2026 na kuwekwa katika tovuti ya mahakama Aprili 10,2026.

Sababu za kudodoswa Ofisa wa TCRA

Machi 26,2026 wakati kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya mahakama kutoa amri mbalimbali, mleta shauri kupitia kwa wakili Seka, aliwasilisha ombi kwa Mahakama itoe amri kwa ofisa huyo kufika mahakamani ili kuulizwa maswali.

Maswali hayo yangehusu kiapo kinzani alichokiwasilisha kwa niaba ya TCRA na AG ambao ni walalamikiwa wa pili na wa tatu, ambapo wakili Seka aliegemea kanuni ya 15(3)(b) ya Kanuni za Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu (Bradea) iliyochapwa na GN namba 304 , akisema kiapo kina maelezo yanayojikanganya.

Wakili Seka alisisitiza kwamba kwa kuwa Mahakama itaendelea kupokea ushahidi wa pande mlalamikiwa wa pili na wa tatu kuhusu hati ya kiapo, kuruhusu kuulizwa maswali ya dodoso kutasaidia Mahakama hiyo kupata ushahidi wa wazi.

Mlalamikiwa wa kwanza, Vapper Tech Limited, kupitia kwa wakili Majanjala, waliunga mkono maombi hayo akisema hati ya kiapo ni mbadala wa ushahidi wa mdomo, maswali ya dodoso yanaruhusiwa kama haki ya msingi ya kusikilizwa.

Hata hivyo, wakili wa Serikali Mkuu, Webiro, anayewawakilisha walalamikiwa wa pili na wa tatu, alipinga ombi hilo akisema maombi hayo hayawezekani katika mazingira ambayo walalamikiwa hao wamewasilisha kiapo kinzani kortini.

Wakili Webiro alieleza kuwa kanuni ya 15(3(a) inataka ushahidi katika suala hili uwe kwa njia ya kiapo kwa kuongeza au mbadala ya ushahidi wa mdomo.

Aliongeza kuwa kanuni ya 15(3)(b) ya Kanuni hizo za Bardea inawahusu mashahidi ambao walikuwa hawajawasilisha hati za kiapo na mahakama inaona inafaa kuwaita kwa uamuzi wake ambao ushahidi wao utasaidia mahakama.

Wakili aliongeza kuwa kanuni ya 15(4) ya kanuni hizo inaruhusu kuhojiwa kwa shahidi kwa idhini ya mahakama iwapo shahidi ataitwa kutoa ushahidi.

Akijibu hoja za wakili Webiro, wakili Seka alitafsiri maana ya neno “witness” (shahidi) lililopo katika kanuni ya 15(3)(b) kuwa inajumuisha shahidi ambaye ametoa hati ya kiapo na yule ambaye hajatoa kiapo mbele ya mahakama.

Wakili alisema ingawa Kanuni ya 15(4 inapaswa kusoma na kanuni ya 15(3(b), kanuni ndogo ya 4 ya kanuni ya 15 inahusu shahidi aliyeitwa na mahakama yenyewe (suo motu), ndio wadaawa wanaruhusiwa au kuzuiwa kumdodosa.

Katika uamuzi wao, majaji hao walisema wamepitia kwa umakini kanuni ya 15(3)(a) na (b) ya Kanuni hizo, na kuona kuwa zinaipa mamlaka ama kupokea ushahidi kwa njia ya kiapo kama mbadala wa mdomo au ushahidi wa mdomo.

Pia, walisema Kanuni hiyo inaipa mahakama mamlaka ya kuita shahidi, kumpima na kuruhusu shahidi yeyote kuulizwa maswali ya dodoso kama itaona ushahidi wake unaweza kuisaidia mahakama kufikia uamuzi au hukumu ya haki.

Majaji hao walirejea vifungu vilivyonukuliwa na mawakili wa pande zote mbili lakini ikafikia hitimisho kuwa muombaji alitumia kimakosa kanuni hizo.

“Mwombaji ametumia kimakosa masharti ya kanuni ya 15(3)(b) kuitaka mahakama kumpa kibali cha kuhojiwa Filikunjombe ambaye amewasilisha hati yake ya kiapo cha mlalamikiwa wa pili na wa tatu, na ambayo ni sehemu ya ushahidi wao”.

Majaji hao walisema msingi wa Buyobe kuomba ofisa huyo kuitwa ili amuulize  maswali ya dodoso ni kutokana na kuwepo mkanganyiko wa maelezo katika kiapo kinzani alichowasilisha mahakamani kwa niaba ya mlalamikiwa wa pili na wa tatu.

“Lakini hata hivyo, muombaji hakufafanua au kutaja mkanganyiko huo wala hata kuonyesha ni aya ya ngapi ya kiapo kinzani yenye maelezo ya mkanganyiko,”walisema majaji hao katika uamuzi wao huo na kuongeza kusema kuwa:-

“Katika mazingira haya, hata kama mleta shauri alikuwa na haki ya kumuuliza maswali ya dodoso Bwana Filikunjombe, ameshindwa kuishawishi mahakama hii namna ushahidi ambao ungepatikana ungeisaidiaje mahakama kufikia haki.”

“Mbali na mleta maombi kushindwa kubaini utata unaodaiwa, usomaji wetu wa hati za kiapo na nyaraka zilizoambatanishwa nazo, unaonyesha utoshelevu wa kutuwezesha kuamua ipasavyo shauri bila ya kuhitaji udodosaji wa ziada”.

“Kulingana na uchunguzi wetu hapo juu, tunaona maombi ya mwombaji kumwita aliyeapa kiapo kinzani kwa niaba ya mlalamikiwa wa pili  na wa tatu ili kumuuliza maswali ya dodoso haina uhalali na haina maana hivyo yanakataliwa,” walisema.

Kutokana na aina ya maombi hayo, majaji hao waliamuru kila upande kubeba gharama zake na kutokana na uamuzi huo, sasa shauri la kikatiba limepangwa Mei 4,2026 kwa ajili ya pande zote za shauri hilo kuwasilisha mawasilisho ya mwisho.

Kiini cha shauri la kikatiba

Buyobe alieleza kuwa Septemba 6,2025, mlalamikiwa wa pili ambaye ni TCRA, alisitisha leseni ya Jamii Forums, kwa madai ya kukiuka sheria kwa kuchapisha maudhui yanayokwenda kinyume na tamaduni na desturi za nchi.

Habari hiyo kwa mujibu wa shauri hilo, TCRA ilidai maudhui hayo yaliathiri umoja wa kitaifa, amani, utulivu na kudhalilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, Buyobe ambaye ni mtumiaji aliyethibitishwa (verified user) wa Jamii Forums, alichukizwa na uamuzi huo, akisema unakiuka haki zake za kikatiba za kutafuta, kupokea na kutoa taarifa na imeathiri uhuru wake wa kutoa maoni.

Pia, anapinga Kanuni namba 9(a),(c),(e),(g) na (j) lakini pia kanuni za 12(a)(i), 15(A) pamoja na aya ya 3(a),9 na 10 ya Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni za mwaka 2020 kwani zinakiuka Katiba Ibara za 18(a)(b)(c)(d),20(1) na 29(1) za Katiba.

Nini anachokiomba mahakamani

Ni kutokana na hoja hizo, mlalamikaji anaiomba Mahakama hiyo itamke kuwa kusimamishwa kwa leseni ya Jamii Forums kulikofanywa na TCRA ni kinyume na haki za msingi na uhuru wa mlalamikaji zilizomo katika Katiba ya Tanzania.

Pia, anaiomba Mahakama itamke kuwa kusitishwa kwa leseni ya mlalamikiwa wa kwanza kutoa huduma za kihabari kulikofanywa na TCRA, kunakiuka haki za kimsingi kama zilivyoainishwa katika Ibara za 18(a)(b)(c)(d), 20(1) na 29(1) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mbali na maombi hayo, anaomba Mahakama itamke kuwa baadhi ya vifungu vya Kanuni ya 9,12,15 na 16 na GN namba 538 ya 2020, kwamba zinakiuka Ibara za 18(a),(b),(c)(d),20(1) na 29(1) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia, anaiomba Mahakama itoe tamko kuwa kusitishwa kwa leseni ya Jamii Forums kulikofanywa kulikiuka Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), kifungu cha 9 cha Mkataba wa Kiafrika wa Haki za Binadamu na Watu na Kifungu cha 19 cha Tamko la Kimataifa la Haki za Kibinadamu.