Sintofahamu mwili wa kichanga kutoonekana mochwari ya Mawenzi

Moshi. Hali ya sintofahamu imeibuka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi, baada ya familia ya Edward Modest, mkazi wa Njiapanda, Himo, Wilaya ya Moshi mkoani hapa kufika katika hospitali hiyo kuchukua mwili wa mtoto wao aliyefariki dunia Aprili 10, 2026 na kuukosa katika chumba cha kuhifadhi maiti.

Mtoto huyo, Doreen Edward ambaye alizaliwa Januari 6, 2026 alifariki dunia Aprili 10, 2026 katika hospitali hiyo aliyokuwa amelazwa akisumbiliwa na tatizo la kubanwa na kifua.

Mwananchi limefika katika hospitali hiyo na kuutafuta uongozi ambao umeomba kupewa muda kufuatilia kujua ni nini ambacho kimetokea.

Mama mzazi wa mtoto huyo (marehemu) Neema Paulo (35) akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Aprili 13, 2026 nje ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi.

Familia hiyo ambayo tayari imefanya maandalizi ya maziko ya mtoto wao leo Aprili 13, 2026 imebaki katika hali ya sintofahamu huku wakishikwa na butwaa kwa kuukosa mwili wa mtoto huyo ambapo hadi kufika jioni hii hawajajua hatima ya mazishi yake.

Aidha, familia hiyo imedai ilifika hospitalini hapo saa nne asubuhi kwa ajili ya kuchukua mwili wa mtoto huyo lakini walipofika katika chumba cha kuhifadhia maiti hawakuupata mwili huo.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Neema Paulo (35) amesema alifika hospitalini hapo Aprili 9, 2026 na mtoto wake aliyekuwa amezidiwa akitokea kituo cha afya Himo ambapo alilazwa na ilipofika Aprili 10, 2026, mwanaye alifariki dunia.

“Mtoto wangu alikuwa anaumwa nikamleta hapa Mawenzi (hospitali) Alhamisi, nikitokea hospitali ya Himo ambapo kule nilikaa siku mbili. Siku ya tatu nikapewa rufaa ya kuja hospitali ya Mawenzi, nikapokelewa hapa, mtoto akaanza kupewa matibabu. Kuamkia Ijumaa, saa 5 asubuhi, mtoto akawa amefariki dunia,” amesema mama wa mtoto huyo.

Mama mzazi wa mtoto huyo (marehemu) Neema Paulo (35) akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Aprili 13, 2026 nje ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi.

Amesema baada ya mtoto huyo kufariki, taratibu za kuhifadhi mwili ziliendelea na yeye kuelekea nyumbani kwa ajili ya taratibu za maziko.

“Kesho yake, Jumamosi, tulikuja hapa Mawenzi kufanya malipo ya wodini ambayo tulikuwa tukidaiwa pamoja na malipo mengine kwa ajili ya utaratibu wa kuja kuchukua mwili Jumatatu (leo).

Amesema: “Cha kushangaza, leo tumekuja kuchukua mwili, tumefanya taratibu zote za malipo, lakini tumeenda mochwari mwili wa mtoto wetu hauonekani, tukiuliza uongozi wa hospitali wanatuambia bado tusubiri wanatafuta, mpaka sasa tupo hapa tunasubiri,” amesema.

Aidha, amesema katika chumba cha kuhifadhia maiti wameonyeshwa mwili wa mtoto ambaye si wao na kwa mtazamo anaonekana ni mkubwa na mpaka sasa hawajui nini hatima yao maana uongozi wa hospitali haujatoa majibu ya wapi ulipo mwili wa mtoto wao.

Kwa upande wake, baba wa mtoto huyo, Edward Modest amesema licha ya kusubiri kwa muda mrefu hawataondoka hospitalini hapo mpaka watakapokabidhiwa mwili wa mtoto wao na si vinginevyo.

“Yaani tunakuja kuchukua mwili wa mtoto tunaambiwa hauonekani, yaani hatuelewi kabisa, hatuelewi tunachotaka ni mwili wa mtoto tukazike,” amesema baba wa mtoto huyo.

Naye, mmoja wa majirani wa familia hiyo ambaye yupo hospitalini hapo, Mary Njau amesema wapo hospitalini hapo kwa zaidi ya saa saba kusubiri majibu ya uongozi wa hospitali kuhusu wapi mwili wa mtoto huyo ulipo, lakini bado kimya kimetawa.

“Tumekuja asubuhi hapa hospitalini na tumepewa kibali cha maziko, lakini sasa ni zaidi ya saa saba hakuna mwili tunaopewa wala majibu yanayoeleweka, mpaka sasa hatujui nini cha kufanya, tunaomba serikali itusaidie tupate mwili wa mtoto wetu tukazike, maana tulishachimba na kaburi,” amesema jirani huyo.