Songwe. Serikali imetoa siku 14 kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (Tarura) Wilaya ya Ileje mkoani Songwe kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa daraja la Mto Luswiswi, ili kuruhusu wanafunzi kuendelea na masomo.
Daraja hilo lililopo Kijiji cha Bwenda linadaiwa kukatika kufuatia mvua zilizonyesha na kusababisha Shule ya Msingi Bwenda kufungwa na kukata mawasiliano na shughuli za uchumi baina ya vijiji vitano vilivyopo wilayani humo.
Pia imeelezwa kuwa kutokana na changamoto ya daraja hilo kutishia usalama kwa wananchi, imesababisha baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kuhamia shule za jirani ili kunusuru maisha yao.
Muonekano wa daraja la mto Luswiswi ambalo lilikatika kufuatia mvua zilizonyesha na kusababisha kukatika kwa mawasiliano na kufungwa Shule ya Msingi Bwenda wilayani Ileje ili kunusuru maisha ya wanafunzi. Daraja hilo linatarajia kuanza kujengwa na kukamilika ndani ya siku 14. Picha na Sadam Sadick
Wakizungumza jana, Aprili 12, 2026 wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, baadhi ya wananchi wamesema daraja hilo limekuwa kero kwa watumiaji, wakimuomba kusaidia kulijenga ili kuruhusu matumizi kuendelea.
Iman Mtafya, mkazi wa kijiji hicho, amesema kwa sasa wanafunzi wameshindwa kupita katika daraja hilo huku wengine wakitimkia shule nyingine, akiomba Serikali kuwajengea hata la dharura ili kuruhusu mawasiliano.
“Tunaomba hata tupate daraja la muda kwa ajili ya wanafunzi, tusaidieni watoto waende shule, wengine wamehamia shule za jirani na mawasiliano yamekatika eneo hili, hiki ndicho kilio chetu,” amesema Mtafya ambaye ni Katibu wa CCM Kata ya Rubanda.
Naye Anangisye Kasebele amesema wanaishukuru Serikali kwa kufika kijijini hapo kushuhudia changamoto zao, akieleza kuwa wanajivunia kuwa na mbunge ambaye amekuwa na wananchi muda wote.
“Tunatoa shukrani kwa Serikali namna inavyofika kwa wananchi kusikiliza na kutatua kero zetu, tunazo changamoto ya miundombinu ya madaraja kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha,” amesema Kasebele.
Akizungumza na wananchi hao, Naibu Waziri Kasekenya amewataka Tarura wilayani humo kuhakikisha ndani ya siku 14 daraja hilo linatengenezwa ili kuruhusu wanafunzi kuendelea na masomo.
Hata hivyo, ametumia nafasi hiyo kuwapa pole wananchi wa jimbo hilo kwa changamoto za barabara na daraja hilo, akieleza kuwa kutokana na tatizo hilo mawasiliano yamekatika, hivyo lazima juhudi za makusudi zifanyike.
Muonekano wa daraja la mto Luswiswi ambalo lilikatika kufuatia mvua zilizonyesha na kusababisha kukatika kwa mawasiliano na kufungwa Shule ya Msingi Bwenda wilayani Ileje ili kunusuru maisha ya wanafunzi. Daraja hilo linatarajia kuanza kujengwa na kukamilika ndani ya siku 14. Picha na Sadam Sadick
“Tuna mambo mawili ya kufanya kwa daraja hili, tutafanya usanifu japo inachukua muda mrefu, hivyo kwa kuwa wanafunzi lazima waende shule na mawasiliano yarejee, lazima tujenge la dharura ambalo litaweza kutumika kwa wananchi na vyombo vya moto.
“Tumekubaliana hiyo kazi ianze mara moja, meneja wa Tarura yupo hapa, tumemkabidhi mkandarasi aanze kazi haraka, tunategemea isizidi wiki mbili iwe imekamilika ili shughuli ziweze kuendelea,” amesema Kasekenya.
Mhandisi huyo na Mbunge wa Ileje ameishukuru Serikali kwa kukubali ombi lake la kujenga daraja hilo, akieleza kuwa anaamini kazi itafanyika na kukamilika kwa wakati, akieleza kuwa Rais ametoa kibali hivyo wananchi waendelee kuiamini Serikali.
“Niishukuru Serikali kwa ujumla kuanzia Rais, Tamisemi na Tarura kwa kuruhusu shughuli hii, tunataka watu wavuke kwa amani, watoto waendelee na masomo, hatutaki kupoteza maisha ya mtoto hata mmoja, mkandarasi siku 14 kazi imalizike,” amesema Naibu huyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Tarura wilayani humo, Mhandisi Lugano Mwambingu amesema wanaamini ndani ya siku 14 kazi itakuwa imeisha na kuruhusu wanafunzi kuendelea na masomo na mawasiliano kurejea.
“Hii ni kazi ya dharura, bado hatujafanya tathmini kujua gharama ya mradi, lakini tutasimamia vyema kuhakikisha ndani ya siku 14 mkandarasi anamaliza kazi hii ili wanafunzi waendelee na shule ambayo inadaiwa kufungwa,” amesema meneja huyo.
