Dar es Salaam. Wakati pazia la shindano la wazo bora la kiuchumi lililopewa jina la ‘Vijana Uchumi Challenge’ likiwa limefunguliwa, vigezo vya kushiriki vimewekwa wazi, huku mshindi akitarajiwa kulamba Sh30 milioni.
Hatua hii inakuja ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, kutangaza uwepo wa shindano hilo na kuteua kamati ya watu wanane watakaosimamia maandalizi ya kufanyika kwake, na vijana 100 wataingia katika mchujo wa awali kabla ya kupatikana mshindi wa kwanza hadi watatu.
Ujio wa shindano hilo, kwa mujibu wa Waziri Nanauka, ni kupata mawazo mbadala kutoka kwa vijana kuhusu namna gani nchi inaweza kukabiliana na hali ya uchumi kunapotokea misukosuko mbalimbali duniani, ikiwemo vita.
Huku swali kuu kwa washiriki likiwa: ‘Linapotokea tishio la uchumi wa dunia kushuka kutokana na misukosuko ya kimataifa, ikiwemo vita, ushindani wa kiuchumi na teknolojia, ni changamoto zipi zinazoweza kuikumba Tanzania na nini kifanyike ili uchumi wa Tanzania uendelee kuimarika?’
Kutokana na hilo, mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya shindano hilo, Joseph Malekela, leo Jumatatu, Aprili 13, 2026, ameeleza sifa wanazopaswa kuwa nazo washiriki, vigezo vya wazo husika pamoja na zawadi zitakazotolewa kwa washindi.
Malekela amezitaja sifa hizo kuwa mshiriki anapaswa kuwa kijana mwenye umri kati ya miaka 15–35 na awe Mtanzania.
“Sifa nyingine ni kushiriki kama mtu mmoja na siyo kikundi, huku wazo atakaloandika liwe na maneno yasiyozidi 300 au video isiyozidi dakika tatu, na uwasilishaji wa mawazo hayo utaanza leo hadi Aprili 30, 2026,” amesema.
Kuhusu vigezo vya wazo, Malekela amesema linapaswa kuwa la kibunifu na upekee, na mshiriki awe na uelewa wa muktadha wa uchumi wa kitaifa na kimataifa.
“Pia katika hili, wazo liwe linalotekelezeka, linaloeleza athari kwa uchumi wetu na liwe na uwezo wa kuleta fursa, ikiwemo za ajira kwa vijana,” amesema.
Vigezo vingine ni uendelevu wa wazo ambao utakuwa wa kudumu na kuleta fikra chanya, pamoja na kuwa na mpangilio mzuri na rahisi kueleweka.
Kwa upande wa zawadi, Malekela amesema mshindi wa kwanza atapata Sh30 milioni, wa pili Sh15 milioni na wa tatu Sh5 milioni.
Kwa wale kumi bora, mbali na zawadi, watafaidika na mafunzo ambayo hutolewa na wizara, na ili shindano hili lisiwe la mara moja, watapata vyeti kutambua mchango wao wa mawazo.
Kwa watakaoingia kumi bora, kila mmoja atapata Sh1 milioni, huku washiriki 30 watafaidika na mafunzo ambayo hutolewa na Wizara.
Wakati kwa washiriki 100 watakaokuwa wameingia katika mchujo, watapatiwa vyeti vya kutambua mchango wao wa mawazo.