Wafanyakazi wapendekeza haya kupunguza makali ya maisha

Dar es Salaam. Wakati gharama za maisha zikiendelea kupanda kutokana na ongezeko la bei ya mafuta, vyama vya wafanyakazi vimewataka waajiri na Serikali kuchukua hatua zitakazoleta unafuu kwa watumishi wao ili wamudu maisha katika nyakati ngumu.

Kwa mujibu wa wawakilishi hao wa wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi, ni muhimu waajiri wafikirie kutoa huduma za chakula ofisini na usafiri wa pamoja kwa wafanyakazi wao ili kuwapunguzia gharama za usafiri kutoka nyumbani kwenda ofisini.

Wamesema hatua hizo ni muhimu kwa sababu gharama za maisha zimeongezeka, huku mishahara ya wafanyakazi ikibaki bila mabadiliko na hivyo kuliacha kundi hilo katika hali ngumu.

Wafanyakazi wanakuja na mapendekezo hayo wakati ambao bei ya mafuta imepanda duniani kote kutokana na kuathirika kwa mnyororo wa ugavi wa nishati hiyo, kulikosababishwa na vita vya Mashariki ya Kati.

Vita hivyo, vinavyoyahusisha mataifa ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, vimesababisha kuharibika kwa miundombinu ya uzalishaji wa mafuta, na hata Mlango wa Bahari wa Hormuz unaopitisha takriban asilimia 20 ya nishati hiyo kufungwa.

Hata hivyo, tayari Hormuz imefunguliwa kwa wiki mbili, hatua iliyoambatana na kusitishwa kwa mapigano baada ya kuanza kwa mazungumzo kati ya Iran na Marekani, ambayo inaelezwa yamekwama.

Akizungumza na Mwananchi, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TAREWU), Michael Marere, amesema kupanda kwa bei ya mafuta kumeathiri huduma nyingi huku mishahara ya wafanyakazi ikibaki bila mabadiliko.

“Katika kipindi hiki, waajiri wanapaswa kuwasaidia wafanyakazi kupunguza gharama za maisha. Kwa mfano, kutumia usafiri wa pamoja au kuwa na huduma za chakula ofisini ili kupunguza gharama,” amesema.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude, amesema gharama za usafiri, chakula na huduma nyingine zimepanda, na mfanyakazi hawezi kuhimili mazingira ya sasa kwa mshahara alionao.

Amesema siku zote mwajiri amekuwa akitoa kiwango kidogo cha mshahara kwa mfanyakazi, hivyo maisha yanapobadilika ghafla ni maumivu kwa mfanyakazi.

“Wakati huu ni muhimu waajiri watangaze hali ya dharura, watoe ahueni ya maisha kwa watumishi wao walau kwa miezi kadhaa hali hii ipite kwanza,” amesema.

Mbali na hayo, Mkude amesema kwa kuwa Serikali ndiyo mlezi wa wananchi, iondoe sehemu ya kodi kwenye mishahara ya watumishi ili kuwaletea unafuu wakati huu.

“Serikali iangalie vyanzo vyake vingine vya mapato ili iondoe kodi iliyopo kwenye mishahara, hii itasaidia kama wafanyakazi hawataongezewa mishahara, watapata mshahara wao ukiwa mzima,” amesema.

‘Kodi katika mshahara ipunguzwe’

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Shule Binafsi Tanzania (TPTU), Julius Mabula, amesema ili kumsaidia mfanyakazi, Serikali ifanye mapitio ya haraka ya mishahara kwa kuzingatia mfumuko wa bei, na kuweka utaratibu wa kuongeza mishahara kila mwaka kulingana na hali ya uchumi.

“Pia, Serikali ipunguze PAYE kwa wafanyakazi wa kipato cha chini ili kuongeza uwezo wao wa kumudu maisha. Vilevile, imarishe mifumo ya udhibiti wa bei na kuhakikisha usambazaji wa vyakula muhimu unakuwa wa uhakika na wa bei nafuu,” amesema.

Kuhusu gharama za usafiri kupanda, amependekeza Serikali kutoa ruzuku kwa usafiri wa umma au kutoa motisha kwa waajiri kutoa posho ya usafiri kwa wafanyakazi wao.

Pia, amesema Serikali, kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ichukue hatua madhubuti za kudhibiti mfumuko wa bei kwa sera sahihi za fedha na uchumi.

Amesema badala ya kampuni kutoa kwa jamii (CSR), ni muhimu kuwasaidia kwa dharura watumishi wao katika kipindi hiki ambacho gharama za maisha zimepaa.

“Serikali ichukue hatua za haraka na za kimkakati kulinda ustawi wa mfanyakazi, kwani mfanyakazi ndiye mhimili wa uzalishaji na maendeleo ya Taifa. Bila kumjali mfanyakazi, uchumi wa nchi hauwezi kusimama imara,” amesema.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya, amesema athari za kupanda kwa bei ya mafuta ni za dunia nzima, si Tanzania pekee.

Amesema mafuta yanaathiri sekta nyingi, ikiwemo chakula na usafiri, ingawa katika sekta ya afya athari hazionekani kwa kiwango kikubwa kutokana na huduma zinazotolewa na Serikali.

“Sisi wafanyakazi tunalia kama wanavyolia wananchi wengine. Tunaiomba Serikali iangalie bei ya mafuta kwa sababu athari ni kubwa. Ikiwezekana, itumie akiba ya mafuta ili kupunguza makali ya hali hii,” amesema.

Pia, ameishauri Serikali kudhibiti wafanyabiashara ili wauze mafuta kwa kuzingatia bei waliyonunulia, badala ya kutumia bei mpya wakati bado wana akiba ya mafuta ya zamani.

Wafanyakazi ndio wanaumia zaidi

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za Utafiti, Taaluma na Mashirika (RAAWU) Taifa, Jane Mihanji, amesema kupanda kwa bei ya mafuta kunatokana na hali ya kimataifa, lakini bado wafanyakazi wanaumia zaidi.

“Wafanyakazi ndiyo walipakodi wakubwa kwa sababu kodi hukatwa moja kwa moja kwenye mishahara yao. Tunaiomba Serikali itafute namna ya kupunguza makali ya hali hii,” amesema.

Ameongeza kuwa hata watumiaji wa gesi katika vyombo vya moto wameathirika, huku gharama za vyakula na huduma nyingine zikizidi kupanda.

Pia, ametoa wito kwa mataifa yenye migogoro kurejea kwenye amani, akisema migogoro hiyo inaathiri hata nchi zisizohusika moja kwa moja.

“Niwaombe wafanyakazi waendelee kuwa watulivu wakati tukisubiri hatua za Serikali,” amesema.

Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani na Kilimo Tanzania (TPAWU), John Vaaye, amesema ongezeko la bei ya mafuta ni pigo kubwa hasa kwa wafanyakazi wa sekta binafsi vijijini.

“Tunapitia maumivu makali kutokana na kupanda kwa gharama za maisha huku vipato vyetu vikiwa vidogo. Serikali inapaswa kutafuta njia ya kutupunguzia mzigo huu,” amesema.

Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi, amesema ingawa ongezeko la mshahara ni vigumu kufanyika haraka, lakini sekta ya usafirishaji, ambayo gharama zake zinaongezeka, inaweza kuongeza mishahara kwa watumishi wake.

“Hata wale wanaofanya kazi viwandani, waajiri wanaweza kuwaongezea mishahara. Hatujui hali hii itadumu kwa muda gani, lakini kama itakuwa ya muda mrefu, ni muhimu waajiri kuongeza mishahara hasa kwa kuangalia kima cha chini,” amesema.

Mwanzoni mwa Aprili 2026, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, akiwasilisha bajeti ya mwaka 2026/2027 bungeni Dodoma, aligusia suala la kupanda kwa bei ya mafuta na kusema Serikali inaendelea kulifanyia kazi.

“Tumeona bei zimeanza kupanda. Tutahakikisha tunatafuta njia bora ya kukabiliana na hali hii ili wananchi waendelee kupata mafuta kwa bei nafuu na kudhibiti ongezeko la gharama za maisha,” alisema.

Aprili 7, 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dk James Mataragio, alisema taarifa rasmi itatolewa mara baada ya kukamilika kwa taratibu zinazohitajika.