▪︎ Asisitiza Vijana kuomba udahili na ufadhili*
▪︎ Asisitiza Uwazi na Ushindani*
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ametangaza rasmi kutolewa kwa ufadhili kupitia Samia Scholarship Exender AI/DS wa masomo ya Uzamili (Masters) katika Sayansi ya Data, Akili Unde na fani zinazohusiana.
Akizungumza Aprili 13, 2026 jijini Dar es Salaam amesema kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika kuandaa rasilimali watu wenye uwezo wa kushindana kimataifa katika sayansi na teknolojia na kuwashawishi vijana wenye vigezo kuomba udahili na ufadhili.
Prof. Mkenda ameeleza kuwa Samia Scholarship extended DS/AI+ ilianza kufadhili wanafunzi wa shahada ya kwanza waliobobea katika sayansi, uhandisi, tiba na hisabati, ambapo tayari wanafunzi 16 wamepelekwa nchini Afrika Kusini na wengine 34 watakwenda nchini Ireland.
Ameongeza kuwa ufadhili wa sasa unalenga kuongeza idadi ya vijana wa kitanzania wenye ujuzi na taaluma katika maeneo hayo.
“Ufadhali huu ni kwa waombaji watakaosoma shahada ya Uzamili katika Taasisi ya Indian Institute of Technology (IIT) Madras – Kampasi ya Zanzibar,” amesisitiza Prof. Mkenda
Waziri Mkenda amesema kuwa masharti ni ya wazi ambapo mwombaji awe Mtanzania, mwenye umri usiozidi miaka 35, awe na daraja la kwanza katika masomo ya sayansi ya kidato cha sita, GPA ya angalau 3.8 katika shahada ya kwanza, na awe amepata udahili katika IIT Madras, Zanzibar.
Amesisitiza kuwa hatua ya kwanza ni kuomba udahili chuoni kabla ya Aprili 15, kisha kuwasilisha maombi ya ufadhili kuanzia Juni 1 hadi Juni 30 na kwamba Kamati huru itapitia maombi kwa uwazi na ushindani, kuhakikisha wanafunzi bora zaidi wanapata nafasi.