Mwanza. Fikiria hali hii: mke anapata mshahara mkubwa kuliko mume. Je, hiyo ni baraka kwa familia au mwanzo wa migogoro?
Kwa miaka ya hivi karibuni, mada hii imezua mjadala mkubwa, hasa kufuatia kazi za kitafiti zinazodai kuwa ndoa ambazo mwanamke ndiye mtoa kipato mkuu, zinaweza kuwa na hatari kubwa ya kuvunjika.
Hata hivyo, je, ni kweli kwamba pesa za mwanamke zinaweza kubomoa ndoa au ni mitazamo ya jamii, heshima na mawasiliano ndizo zinazoamua hatma ya uhusiano?
Watafiti kutoka Chama cha Kijamii cha Marekani (American Sociological Association), pamoja na watafiti wa Chuo Kikuu cha Chicago cha nchini gumi, wanaeleza kuwa katika baadhi ya mazingira hasa zamani, ndoa ambazo mwanamke alikuwa na kipato kikubwa zilionekana kuwa na ongezeko la hatari ya talaka kwa takribani asilimia 30 hadi 40.
Hata hivyo, watafiti wanasisitiza kuwa takwimu hizi hazimaanishi kuwa kipato pekee ndicho chanzo cha migogoro.
Katika muktadha wa Tanzania, mtaalamu wa saikolojia na uhusiano, Said Kasege, anaeleza kuwa mabadiliko ya kiuchumi kwa mwanamke, yanaweza kubadilisha mizani ya nguvu ndani ya ndoa.
“Ongezeko la talaka baada ya mwanamke kujikwamua kiuchumi linahitaji kutazamwa kwa jicho la kina, si kwa hisia pekee. Mabadiliko haya hubadilisha sana mizani ya nguvu ndani ya ndoa,” anasema.
Anafafanua kuwa hapo zamani utegemezi wa kifedha ulimfanya mwanamke kuvumilia changamoto nyingi.
Lakini anasema anapopata uwezo wa kujitegemea, uvumilivu huo hupungua si kwa kiburi, bali kwa sababu ya kuongezeka kwa mambo ya kujiuliza.
“Mwanamke anaanza kujiuliza: Je, ninaheshimiwa? Je, nina furaha kweli? Ikiwa hapati majibu ya kuridhisha, uhuru wa kifedha unakuwa kama mlango wa kutokea,” anaeleza.
Kwa mtazamo wa kisaikolojia, kujitegemea kifedha kunabadilisha namna mtu anavyojiona. Mwanamke anapokuwa na uwezo wa kujitegemea, huongeza hali ya kujithamini na kujiamini katika kufanya uamuzi.
Hii ina maana kuwa mambo ambayo hapo awali angeyavumilia, sasa anaweza kuyakataa.
“Kwa upande wa kijamii, Tanzania bado inaathiriwa na mfumo dume, ambapo majukumu ya kifamilia yanaelekezwa kwa misingi ya kijinsi. Mwanamke anapofanikiwa kiuchumi, baadhi ya wanaume huona kama mamlaka yao inapungua, anasema Kasege na nyongeza:
“Hali hii inaweza kusababisha migogoro ya mara kwa mara, ukosefu wa mawasiliano yenye afya, na hatimaye kuvunjika kwa ndoa.”
Kwa upande wa wanawake, baadhi wanakiri kuwa hali hiyo ipo katika maisha halisi, hasa pale mwanamke anapokuwa na uwezo wa kujihudumia.
“Ni kweli baadhi ya ndoa huvunjika kwa sababu ya kipato kikubwa cha mwanamke, hasa kama alipitia mateso kabla ya kuwa na kipato ndani ya uhusiano. Akishapata uwezo wa kujitegemea, haoni sababu ya kubaki kwenye ndoa inayomuumiza,” anaeleza Theresia Mashaka, mkazi wa jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa Roby Jacobs, hali hiyo inaonyesha kuwa mara nyingi kipato si tatizo lenyewe, bali ni kichocheo cha uamuzi ambayo tayari ulikuwa unacheleweshwa na hofu ya utegemezi.
Kwa upande wa wanaume, hali hii huonekana kwa mtazamo tofauti. Wanaeleza kuwa wakati mwingine si mwanamke mwenye kipato ndiye anayevunja ndoa pekee, bali pia namna hisia za mwanaume zinavyomwongoza.
“Wakati mwingine si suala la wanawake kuwa na kiburi kama watu wanavyosema, bali pia wanaume kujihisi wanadharaurika pale wake zao wanapopata pesa zaidi yao. Hapo ndipo migogoro huanza,” anasema Sadick Kwilasa.
Anasema katika jamii nyingi za Kiafrika, mwanaume amezoea kuonekana kama kichwa cha familia na mtoa huduma mkuu. Hivyo, hali inapobadilika, inaweza kuleta mgongano wa kihisia na hata kupunguza kujiamini kwa baadhi ya wanaume.
Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa mafanikio ya kifedha mara nyingi hufichua matatizo yaliyokuwepo tayari, kama vile ukosefu wa mawasiliano, kutoaminiana au heshima ndogo ndani ya ndoa.
Kwa maneno mengine, fedha si chanzo cha migogoro, bali ni kioo kinachoonyesha hali halisi ya uhusiano.
“Mfano halisi unaweza kuonekana katika wanandoa ambao walikuwa na changamoto kabla ya mabadiliko ya kipato. Mwanamke anapopata mafanikio ya kifedha, huanza kuona uwezekano wa maisha bora zaidi… ikiwa ndoa haina msingi wa heshima na ushirikiano, anaweza kuchagua kuondoka,” anaeleza Kasege, ambaye pia ni mwandishi wa vitabu vya saikolojia.
Mshauri wa masuala ya kijamii na ndoa, Mzee Haruna, anasema mabadiliko ya kizazi yana mchango mkubwa katika suala hilo, kwa kuwa wanawake wa sasa wana elimu zaidi, wanafahamu haki zao na wanathamini afya ya akili, hivyo kuwa na viwango vipya vya ndoa ukilinganisha na vizazi vya zamani.
“Katika ndoa za zamani, uvumilivu ulikuwa msingi mkubwa, hata pale ambapo kulikuwa na matatizo. Lakini katika dunia ya leo, watu wengi wanatafuta ndoa yenye furaha, usawa na ukuaji wa pamoja. Hivyo, ikiwa ndoa haitoi vitu hivi, uwezekano wa kuvunjika huongezeka, hasa pale ambapo hakuna utegemezi wa kifedha,” anaeleza.
Anasema ni muhimu kutambua kuwa kuna ndoa nyingi zinazofanikiwa licha ya tofauti ya kipato, na kwamba wanandoa wanaoweka mbele mawasiliano, kuheshimiana na kushirikiana katika uamuzi hujenga msingi imara wa uhusiano.
“Katika mazingira haya, kipato kikubwa cha mwanamke hakileti mgogoro, bali huimarisha familia,” anasema na kusisitiza:
“Wanandoa wanaofanikiwa mara nyingi huwa na mtazamo wa kuona mafanikio ya mmoja kama mafanikio ya wote. Hawaoni ushindani, bali ushirikiano. Hii inasaidia kupunguza migogoro inayoweza kusababishwa na tofauti za kipato.”
Wataalamu hao wanasema suluhisho la changamoto za talaka halipo katika kuzuia mwanamke kufanikiwa kiuchumi; badala yake, linapatikana katika kubadilisha mitazamo ya kijamii na kujenga uhusiano wenye usawa.
Wanasema ndoa ya kisasa inahitaji ushirikiano, si ushindani; mawasiliano ya wazi, si ukimya; na heshima ya pande zote, si mamlaka ya upande mmoja.
