Mali zinavyowatoa roho wanandoa | Mwananchi

Canada. Kuna visa vinavyozidi kuongezeka ambapo wanandoa hutoana roho kisa mali. Japo tutakachojadili hapa si kipya, kuna mafunzo mapya tunaweza kutoa kutokana na ama uzoefu wetu au wenu.

Hivi karibuni,visa vya wanadoa kutoana uhai juu ya mali vimezidi kushamiri. Si kwamba havikuwepo, vilikuwapo ila siku hizi vimezidi. Hii ni kutokana na utandawazi na uelewa wa binadamu juu ya dhana nzima ya mali au utajiri.

Kwa wale wa kizazi chetu, yaani wa kuanzia miaka 50 kwenda juu, wimbi la mauaji baina ya wanandoa wakigombea mali ni jambo ambalo halikuzoeleka japo lilikuwapo si kwa kiwango cha sasa. Hata hivyo, kwa wengi waliokua wakati wa mfumo wa ujamaa, tulifundishwa kutopenda vitu bali utu.

Hata hivyo, hii haizuii zile jamii zinazojulikana kwa uovu huu ambazo ziliendelea na tamaa, unyama na uvivu wa kutafuta vya kutaka kuvuna wasipopanda. Kwanini kuuana kwa ajili ya mali kana kwamba mtaondoka nazo mtakapokufa?

 Ni ukatili na unyama kiasi gani kuuana kwa ajili ya vitu vinavyoweza kutafutwa vikapatikana? Kutokana na matukio mengi tuliyodurusu kwa muda kitambo, tuligundua kuwa hao wanaowaua wenzao ili wachukue mali peke yao, mara nyingi, huuishia gerezani kama siyo damu za waliowaua kuwataabisha.

 Kuna kisa kimoja cha kusikitisha kilichotokea nchini Marekani mwaka jana kwenye jimbo la Texas ambako mwanamke mmoja katili alimuua mumewe kwa kumpiga risasi tatu ili achukue mali zake.

 Pamoja na kujitahidi kuficha ushahidi ukiwamo mwili wa marehemu aliyetoweka, alikamatwa. Sasa anangojea haki ichukue mkondo wake akiwa korokoroni.

 Mama huyu unayeweza kumuita shetani, aliuficha mwili wa marehemu chini ya sehemu ya kuhifadhia takataka na kudai kuwa mume wake alikuwa nchi jirani akijirusha na kimwana wakati alishamnyongelea mbali. Baada ya majirani kutomuona mume, walipiga simu polisi ambao walikuja na kumhoji akatoa taarifa za kujichanganya na kuwafanya watafute hati ya upekuzi na kugundua mwili wa marehemu ukiwa umeishaoza baada ya kufichwa kwa miezi minne.

 Katika kufuatilia visa hivi vya kikatili na kinyama, tuligundua kuwa wengi wanaofanya unyama huu ni wavivu wa kutafuta, wakatili, wajinga, waroho na wapenda vya dezo.

 Kwanini unamuua mwenzio tena kwa mali alizotafuta mwenyewe kama kweli wahusika siyo kama chawa wapendao kunyonya wenzao? Hata chawa huwa hawawaui wale wanaowanyonya.

 Pamoja na udhaifu tajwa hapo juu, kesi nyingi za aina hii zinaonyesha kuwa kuna uwezekano wa ugonjwa wa akili unaowasumbua wauaji hawa ambao hawana tofauti na wauaji wengine.

Wapo wanaosema kuwa mauaji na ukatili huu ama husababishwa na chuki, hasira, visasi, uoga, na mengine mengi kama hayo yatokanayo ya kuachika au kuchelea kuachika.

 Katika baadhi ya jamii, yapo makabila yenye mchezo huu yatokanayo na mashindano na tamaa ya utajiri. Watu hawa huolewa kwa makusudi wakijua wanachopanga kufanya baadaye. Mara nyingi, huwalenga wenye nazo na siyo hohehahe. Katika jamii hizi mke au mume kumuua mwenzake kwa ajili ya tamaa ya utajiri wa haraka, ni jambo la kawaida.

Kitu kingine kilichojitokeza kwenye jinai na kadhia hii ni wahusika kuishia kutofaidi hizo mali japokuwa wapo wachache wanaofanikiwa. Hata hivyo, bado wanaonusurika huishi kwa matatizo yawe ya kiafya au kiakili kutokana na hisia za hatia waliyotenda.  

Japo hatujafanya utafiti wa kisayansi, kuna imani kuwa yeyote amwagaye damu ya mwenzake, damu hiyo itamuandama. Kuna ukweli katika hili. Wauaji wanaweza kuficha mateso wanayopata au kupitia, ukweli ni kwamba wanatesena kwa hatia hasa nyoyoni mwao.

Mwisho, badala ya jamii kuangalia na wengine kushabikia hata kushangilia hawa wale wenye uvivu wa kutafuta lakini wakawa na tamaa ya mali, inabidi ianze kuchukua hatua kama vile kupinga ujahili na unyama huu.

Ukitaka kujua ukweli wa haya tunayoandika, kama kuna yeyote aliyewahi kufanya hivi unayemjua au kumsoma, jikumbushe mwisho wake. Wengine wanaishi kwa kutegemea madawa ya usingizi na ulevi kutokana na mateso ya dhambi na ukatili waliowafanyia wenzao. Haiwezekani uue ambacho huwezi kukiumba uwe salama. Na kama utakuwa salama ni kwa muda.