Global Publishers
April 6, 2026
0 Comments
Klabu ya Singida Black Stars imetangaza kuvunja benchi zima la ufundi lililokuwa chini ya kocha Othmen Najar kuanzia Aprili 5, 2026, kufuatia matokeo mabaya ya hivi karibuni.
Hatua hiyo imekuja muda mfupi baada ya timu hiyo kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa TRA United katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid Stadium.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na uongozi wa klabu hiyo, uamuzi huo umechukuliwa kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu katika mechi za karibuni, hali iliyozua wasiwasi kwa mashabiki na wadau wa soka.
Uongozi wa Singida Black Stars umeeleza kuwa utatoa taarifa zaidi kuhusu benchi la ufundi la muda (mpito) litakalosimamia timu hiyo wakati maandalizi ya michezo ijayo yakiendelea.
Hatua hii inaashiria mabadiliko makubwa ndani ya klabu hiyo, huku mashabiki wakisubiri kuona nani atakayekabidhiwa jukumu la kuinusuru timu hiyo katika kipindi hiki kigumu.
