ACHANA na matokeo ya ushindi wa 3-2 waliopupata Mbeya City dhidi ya KMC, uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya umesema timu hiyo itarejesha makali yake licha ya kutoanza vyema Ligi Kuu Bara msimu huu.
Mbeya City inamilikiwa na Halmashauri hiyo na haikuwa na mwanzo mzuri kwenye ligi na kuweka presha kwa mashabiki kuikatia tamaa wakiitabiria kurejea Championship.
Hata hivyo, Aprili 2 mwaka huu, ikitumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara, iliishindilia KMC mabao 3-2 na kuchumpa nafasi ya 12 kwa pointi 16 baada ya michezo 17.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Justice Kijazi, amesema Ligi Kuu ina ushindani, lakini uongozi wa timu hiyo upo imara na timu yao ni bora.
Amesema Mbeya City ipo Ligi Kuu kwa ajili ya ushindani na inao uwezo wa kufanya hivyo, akisisitiza uongozi umejipanga kuirejesha katika ubora wake kuhakikisha inawapa kile mashabiki wanachotaka.
“Mashabiki waondoe wasiwasi, Mbeya City ni timu bora na inao uwezo wa kutoa ushindani, tumejipanga kiutawala kuirejeshea kiwango chake ili kutetea kile wanachopenda wadau jijini Mbeya,” amesema Kijazi.
Mmoja wa mashabiki wa timu hiyo, Charles Mwakyokile, amesema ushindi katika mchezo dhidi ya KMC umerejesha ari na matumaini kwao wakiamini City inaweza kunusurika kushuka daraja.
Amesema benchi la ufundi linapaswa kufanyia kazi makosa sehemu ya ushambuliaji na kutengeneza muunganiko ili kuondoa makosa binafsi kwa mchezaji mmoja mmoja.
“Bado matokeo si mazuri sana ukilinganisha na walio chini na juu yetu, lakini inatoa matumaini kiasi fulani ila kocha akazie sana straika kutumia nafasi wanazopata, kiujumla tunaiombea timu yetu,” amesema Mwakyokile
