Simba Vs Dodoma Jiji kupigwa Sheikh Amri Abeid

Mchezo wa hatua ya 16 bora wa Kombe la Shirikisho la CRDB baina ya Simba na Dodoma Jiji, Jumapili Aprili 12, 2026 utachezwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha badala ya Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

Uamuzi wa mechi hiyo kupelekwa Arusha umetokana na maombi ya Simba ya kupeleka mchezo huo katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid badala ya Meja Jenerali Isamuhyo kutokana na kubanwa na ratiba ya ligi.

Kabla ya mchezo huo, itacheza na TRA United uwanjani hapo Aprili 9, 2026 na Aprili 15, 2026 itakuwa na mechi nyingine hapo dhidi ya Fointain Gate.

Ikiwa mechi hiyo dhidi ya Dodoma Jiji FC ingechezwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Simba ingelazimika kurudi Dar es Salaam baada ya kukabiliana na TRA United kisha kurejea tena Arusha kucheza na Fountain Gate baada ya kumaliza kibarua cha Kombe la Shirikisho la CRDB.

Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto ameithibitishia Mwananchi Digital kuwa mechi hiyo itachezwa Arusha.

“TFF ilipokea maombi ya timu mwenyeji wa mchezo huo ambayo ni Simba ikiomba uchezwe katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na baada ya kufanyia tathmini maombi yao, ni rasmi mechi hiyo itachezwa Arusha badala ya Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo,” amesema Kizuguto.

Simba itaikabili Dodoma Jiji ikiwa na kumbukumbu ya mchezo wa mwisho baina yao ambao ulikuwa ni wa Ligi Kuu ambao ulichezwa katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kumalizika kwa sare tasa.