Tanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limewakamata watu wawili wanaodaiwa kuhusika na mtandao wa utapeli wa mtandaoni uliowalaghai vijana 87 kwa ahadi za kupata utajiri wa haraka kupitia kampuni isiyo halali.
Taarifa hiyo imetolewa jana Aprili 5,2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, ambapo amewataja waliokamatwa ni Mohammed Idrisa (24), mkazi wa Masiwani, na Fidolini Rashidi (21), mkazi wa Mbugani.
Amesema watuhumiwa hao wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi huku uchunguzi wa kina ukiendelea kubaini mtandao mzima wa uhalifu huo.
Mchunguzi amesema watuhumiwa hao walikuwa wakisimamia shughuli za kampuni iliyojitambulisha kwa jina la Champions E-Commerce Education, ambayo ilijitangaza kutoa mafunzo ya biashara ya mtandaoni yenye mafanikio ya haraka kifedha.
“Vijana waliokuwa wanavutiwa na ofa hizo walitakiwa kulipa kati ya Sh600,000 hadi Sh4,000,000 kama mtaji wa kuanzia pamoja na gharama za mafunzo,” alisema Mchunguzi.
Ameongeza kuwa, licha ya ahadi hizo kuvutia vijana wengi, walijikuta wameingia kwenye mtego wa utapeli uliopangwa kwa ustadi, wakipoteza fedha zao bila kupata faida waliyoahidiwa.
Mchunguzi amesema katika operesheni maalumu iliyofanywa na polisi, vijana hao 87 walikutwa wakiishi katika mazingira yasiyoridhisha, huku wakiendelea kupewa mafunzo yanayodaiwa kuwajengea uwezo wa kufanya biashara hizo mtandaoni.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mbinu zilizotumika zilihusisha matumizi ya mitandao ya kijamii na lugha ya Kishawishi iliyolenga hasa vijana wanaotafuta njia za haraka za kuboresha maisha yao kiuchumi.
Kamanda Mchunguzi amewatahadharisha wananchi kuwa makini na uwekezaji unaoahidi faida kubwa kwa muda mfupi bila kuwa na uthibitisho wa uhalali wake.
“Ni muhimu kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kujiunga na kampuni au mpango wowote wa uwekezaji. Matapeli wanazidi kubuni mbinu mpya za kuwahadaa wananchi,” alisisitiza.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini wahusika wengine wa mtandao huo, huku likiahidi kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaothibitika kuhusika.
