Mwamko wa wazazi unavyofifisha utoaji chakula shuleni

Dar es Salaam. Wakati changamoto ya watoto kushindwa kupata chakula shuleni ikizidi kuathiri ujifunzaji, hali hiyo imetajwa kuchangiwa na mwamko duni wa wazazi.

Mmoja wa walimu kutoka mkoani Kigoma, akizungumza hivi karibuni na Mwananchi, amesema licha ya ushirikishwaji, bado utayari ni mdogo.

“Tumejaribu kufanya vikao mara mbili kuwashirikisha wazazi kuchangia chakula, hatujafanikiwa. Wengi wanasema hilo ni jukumu la Serikali. Hata ukijaribu kuwashawishi, wanadhani unaenda kinyume na maagizo ya Serikali,” amesema mwalimu huyo.

Amesema ni wakati sasa wa Serikali kusimama hadharani na kutoa tamko kwa wazazi, ili wajue kuwa kuchangia chakula shuleni ni jukumu lao kwa ajili ya kuunga mkono sera ya elimu bure.

Kutokana na kutambua changamoto hiyo, Uwezo Tanzania ilikuja na kampeni ijulikanayo kama “Kikombe cha Ndoto”, inayolenga kuhamasisha utoaji wa uji wa lishe shuleni, ili kuboresha umakini, afya na mahudhurio ya wanafunzi. Kampeni hiyo inalenga kutatua njaa ya darasani, ili watoto wajifunze vyema na kutimiza ndoto zao.

Mkurugenzi wa Shirika la Uwezo Tanzania, Baraka Mgohamwenda, amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubaini kuwa baadhi ya watoto hawapati mlo shuleni hata nyumbani, jambo linalopunguza umakini darasani.

“Ili kutatua changamoto hiyo tunahitaji wadau ambao siyo wazazi tu, bali taasisi binafsi au mtu mmoja mmoja anayeweza kuchangia kuja pamoja,” amesema. Hiyo ni kwa sababu wanaamini kuwa tatizo la kijamii linamalizwa kwa kufanya jitihada zinazojumuisha wadau na kutembea pamoja.

Ripoti ya Uwezo Tanzania ya mwaka 2019, iliyozingatia uelewa wa wazazi juu ya kuchangia chakula shuleni, ilionesha kuwa ni asilimia 50 pekee ya wazazi walitambua hili kuwa jukumu lao.

Ripoti hiyo, ambayo ndiyo ya mwisho kutolewa kuangazia suala hili, pia ilibainisha kuwa asilimia 38 ya wazazi walisema hawana uhakika kuwa jukumu hilo ni lao au la Serikali, huku asilimia 12 wakidai kuwa jukumu hilo ni la Pamoja.

Akizungumzia suala hili, mdau wa elimu Nicodemus Shauri amesema wazazi wengi hawana utayari.

“Baadhi ya wazazi hawana mwamko wa elimu, baadhi wanatamani watoto wao wasiendelee na shule, lakini sheria inawabana. Mzazi kama huyu ni ngumu kumshawishi alipe chakula cha mtoto,” amesema Shauri.

Ametoa mfano wa baadhi ya wazazi wa Mkoa wa Mtwara, katika moja ya tafiti walizowahi kufanya walikuwa wakiwalazimisha watoto wao kujifelisha katika mitihani yao.

“Sasa mzazi ambaye anamlazimisha mtoto kufeli, unadhani atakuwa tayari kutoa kulipa michango tofauti shuleni, ikiwemo chakula?” amehoji.

Mtwara iliyotajwa na Shauri ni moja ya maeneo yanayonufaika kupitia Mradi wa Afya na Lishe Shuleni. Mpango huo kinara unatekelezwa na World Food Programme, kwa kushirikiana na Serikali, na kuungwa mkono na Ubalozi wa Canada.

Programu hiyo inalenga kuboresha lishe na matokeo ya elimu kwa wanafunzi 65,000 katika shule 116 za msingi na sekondari katika mikoa ya Mtwara na Lindi, pamoja na wilaya ya Tandahimba, ikiwa mojawapo ya wanufaika.

“Mlo wa shuleni ni muhimu kwa kujifunza vizuri. Chakula chenye lishe bora huongeza umakini, mahudhurio na ufaulu, hasa kwa wanafunzi kutoka kaya zilizo hatarini. Kwa kupunguza njaa, tunaimarisha ujifunzaji na ustawi kwa ujumla,” amesema Ismaili Saidi, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nahnyanga, wilayani Tandahimba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Ushirikiano wa Canada katika Ubalozi wa Canada nchini Tanzania, Carol Mundel, amesema umuhimu wa ushirikiano huo, akieleza kuwa kusaidia mipango ya chakula shuleni kunahakikisha watoto wanajifunza wakiwa na tumbo lililoshiba, huku wakijenga jamii zenye afya bora.