Wadau wafunguka mfungwa aliyepewa vifaa kuanza maisha uraiani

Dar es Salaam. Hatua ya Rashid Shemndorwa, aliyetumikia kifungo cha miaka 15 jela, kukabidhiwa vifaa vya kuanza maisha uraiani imeibua mjadala kuhusu namna bora ya kuwasaidia wafungwa wanapotoka gerezani, huku wadau wakisisitiza kuwajengea maisha mapya ni njia sahihi ya kuwazuia kurudia makosa.

Shemndorwa, aliyefungwa katika Gereza la Njombe mkoani Njombe, alitoka gerezani Aprili 2, 2026 baada ya kumaliza kifungo chake, akikabidhiwa vifaa vya ujenzi na cheti cha taaluma ya ujenzi aliyoipata gerezani.

Kwa mujibu wa wadau, ili kuwe na mwendelezo wa hilo, Serikali inapaswa kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya kuwawezesha wafungwa wanaorudi uraiani, wasijikute wanakosa cha kufanya na kurudia makosa.

Hata hivyo, utaratibu kama huo ndio unaotumika katika baadhi ya mataifa, wafungwa husomeshwa na kutoka na taaluma. Hata wanapotoka mara nyingi wanapewa mitaji itakayowawezesha kuishi uraiani bila kurudia makosa.

Ilivyokuwa kwa Shemndorwa

Akizungumzia kilichotokea kwa Shemndorwa, Msemaji wa Jeshi la Magereza Tanzania, Elizabeth Mbezi, amesema mfungwa huyo alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 15 katika Gereza la Njombe, mkoani Njombe.

Kile alichokabidhiwa, amesema alinunuliwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Jeremiah Katungu, baada ya kuombwa na mfungwa huyo.

“Kamishna Jenerali alifanya ziara katika gereza hilo na mfungwa aliomba aonane naye binafsi kwa ajili ya kumweleza shida yake. Alilichukulia kwa uzito akamnunulia vifaa hivyo,” amesema.

Ukiacha huyo aliyenunuliwa na Kamishna Jenerali, Elizabeth amesema magereza ina utaratibu wa kuihusisha jamii na wadau kuwasaidia wafungwa wakaishi vema watakaporudi uraiani.

Amesema wanafanya hivyo, kwa kutambua kuwa, Serikali pekee haitafanikiwa kukidhi mahitaji ya wafungwa wote wanaorudi uraiani.

Kuhusu cheti alichokabidhiwa, amesema wafungwa wanapokuwa magerezani kuna programu mbalimbali za urekebishaji wanazofunzwa.

Amesema zipo zile programu wanazofunzwa akiwa palepale gerezani na wengine wanapelekwa katika vyuo kwa ajili ya kupata taaluma.

“Kwa hiyo mfungwa anapotoka pale anakabidhiwa cheti na Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), kwa kuwa tuna ubia na vyuo hivyo.”

Amesema vyeti wanavyopewa ni uthibitisho kuwa, amejifunza kile anachokwenda kufanyia kazi na ana sifa zote za kufanya kazi hiyo pale anapotoka gerezani na kurudi uraiani.

“Tunawapa vyeti hivyo ili kuthibitisha taaluma walizozipata gerezani na kufuta mitazamo ya jamii kuhusu tabia zao za nyuma zilizosababisha wakafungwa,” amesema.

Akizungumzia hilo, mmoja wa watu waliowahi kukaa gerezani kwa miaka tisa, Tumaini Mabula, amesema mara nyingi magerezani wanafanya kazi ambazo ukiziendeleza baada ya kutoka zinabadilisha maisha.

Lakini, ameeleza tatizo ni mtaji au vifaa vya kuifanya kazi hiyo, kwa sababu wengi wanatoka na ujuzi, lakini hawawezeshwi kwenda kuutumia.

“Sasa fikiria umetoka na ujuzi wa ufundi seremala, ukienda kuomba kazi maeneo rasmi watataka cheti, hakukuwa na vyeti. Ukitaka uanze mwenyewe huna mtaji, lakini hili la sasa litasaidia,” amesema.

Amesema utaratibu huo wa magereza, utabadili mtazamo kuhusu jela, kutoka kuwa eneo la kuadhibiwa na wakati mwingine kukufanya uwe sugu, hadi kuwa eneo la kukurekebisha na kukupa mbinu mbadala za kuishi utakapotoka.

“Hii itasaidia hata wale ambao mara nyingi wanarudia makosa na kufungwa kila wakati, watapungua. Kwa sababu mtu anafungwa, akitoka hana cha kufanya anarudia kosa ili akafungwe tena. Lakini ukimpa mradi hawezi kurudia kosa,” amesema Mabula.

Akizungumzia hilo, Mtaalamu wa Sheria za Jinai na Haki za Binadamu, Dk Amina Mwakyusa, amesisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa kitaifa wa uwezeshaji wa wafungwa wanaotoka magerezani.

Amesema tafiti za kimataifa zinaonyesha zaidi ya asilimia 60 ya wafungwa wanaorudia makosa hufanya hivyo kutokana na ukosefu wa kipato halali baada ya kutoka gerezani.

“Mfuko huo unaweza kutoa mikopo midogo, vifaa vya kazi au ruzuku kwa wafungwa waliopata ujuzi wakiwa magerezani. Serikali ikishirikiana na sekta binafsi inaweza kuunda mfuko huu na kuuwekea utaratibu wa uwajibikaji ili kuhakikisha fedha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” amesema.

Amependekeza marekebisho ya sheria ili kutambua rasmi vyeti vinavyotolewa magerezani kama sehemu ya mfumo wa elimu ya Taifa.

Kwa upande wa mchambuzi wa sheria na marekebisho ya jinai, Joseph Mdoe, amesema suluhisho la kudumu lipo katika kuimarisha mfumo wa uangalizi wa mahakama na ufuatiliaji wa wale wanaotoka kabla ya muda wa adhabu kuisha, yaani (probation and parole).

Kwa tafsiri yake, probation ni hali ambayo mtu anayepatikana na kosa haruhusiwi kwenda gerezani moja kwa moja, bali anaachiwa aishi uraiani chini ya masharti maalumu na uangalizi.

Kuhusu Parole, amesema ni pale mfungwa anaachiwa kutoka gerezani kabla ya kumaliza kifungo chake, kwa sababu ameonyesha mwenendo mzuri, lakini bado anakuwa chini ya uangalizi na masharti maalumu.

Amesema mfumo huo ukiboreshwa utaruhusu wafungwa wanaoonyesha nidhamu nzuri kuanza kuunganishwa na jamii hata kabla ya kumaliza vifungo vyao.

“Hii huwasaidia kujenga mtandao wa kijamii na kiuchumi mapema, tofauti na kutoka ghafla bila maandalizi,” amesema.

Ametaka kuwepo kwa sheria inayowalazimisha waajiri wakubwa kutenga asilimia ya nafasi za ajira kwa watu waliotoka magerezani.

Aidha, Mdoe amegusia umuhimu wa kuondoa rekodi za makosa madogo baada ya muda fulani, kwani mara nyingi zinakuwa kikwazo kwa ajira na mikopo.

“Mtu aliyemaliza kutumikia adhabu yake anapaswa kupewa nafasi ya kuanza upya bila kubeba mzigo wa makosa ya zamani maisha yake yote,” amesema.