Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikipitia kipindi muhimu cha mijadala ya kitaifa, wadau mbalimbali wameibua wasiwasi juu ya mwelekeo wa mijadala hiyo, wakieleza kuwa kumekuwa na kupotea kwa kipaumbele katika masuala ya msingi yanayogusa maisha ya wananchi.
Kwa sasa, nchi ipo katika hatua muhimu ya kujadili na kutafuta suluhu ya kupaa kwa gharama za mafuta, bajeti ya Serikali sambamba na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo imeibua hoja kadhaa za kiutendaji.
Aidha, matarajio ya ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29, 2025 nayo yameendelea kuwa sehemu ya ajenda inayosubiriwa kwa hamu, hasa baada ya muda wake wa kuwasilisha ripoti hiyo ukitimia.
Hata hivyo, katikati ya masuala hayo mazito yanayohitaji mjadala wa kitaifa, umeibuka mjadala mitandaoni na katika jamii unaohusu uvumi wa watu kupotea viungo vyao vya siri kwa madai ya ushirikina. Pamoja na uvumi huo, pia zimesambaa taarifa kuhusu mbuzi anayedaiwa kuwa na jinsia mbili mkoani Geita.
Mijadala hiyo imechukua nafasi kubwa katika majukwaa ya kijamii na hata baadhi ya vyombo vya habari kwa siku za hivi karibuni.
Akizungumzia hali hiyo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Conrad Masabo, ameeleza kuwa ni muhimu kwa jamii kuelekeza nguvu katika mijadala yenye tija.
Amebainisha kuwa jamii kujikita katika mijadala ya uvumi inapoteza nafasi ya kujadili mambo muhimu ya maendeleo ya jamii na Taifa.
Dk Masabo ameonya kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuwa na umakini zaidi, ili kuepuka kupotosha mwelekeo wa mjadala wa Taifa kwa kuweka kipaumbele katika masuala yasiyo na tija kwa jamii.
“Hizi habari, mara watu wamepoteza nyeti zao, mara mbuzi ana jinsia mbili—mbuzi mwenyewe anaoneshwa kwenye picha ni mkubwa kabisa, kumbe alikuwepo tu muda mrefu, hazina tija kwa jamii, hazipaswi kupewa nafasi ya kuhamisha mijadala ya msingi ya maendeleo ya Taifa,” amesema.
Kwa upande wake, Wakili Alloyce Komba ameona kuwa mjadala wa sasa unahitaji kurejea kwenye masuala ya uwajibikaji na uchumi, akisikitishwa na hali ya sasa inayoendelea kujadili masuala ya uvumi yanayohusishwa na imani za kishirikina.
Ameeleza kuwa ripoti ya CAG imebeba hoja nzito zinazohitaji mjadala mpana, huku akisisitiza kuwa jamii inapaswa kufuatilia kwa karibu mijadala ya bajeti ili kuelewa mwelekeo wa matumizi ya rasilimali za umma, badala ya kujadili uvumi usio na tija kwa Taifa.
“Nasikitika sana, nilitegemea nione jamii ikijadili mambo haya kwa upana, lakini badala yake masuala ya ajabu haya, mara mbuzi ana jinsia mbili, mara nini, ndiyo yanapewa nafasi kubwa kuhamisha mijadala yenye tija,” amesema.
Kwa upande wake, mdau wa haki za binadamu, Dk Ananilea Nkya, ameeleza kuwa mijadala isiyo na tija inaweza kuathiri namna jamii inavyoshughulikia changamoto zake kuu na kuendeleza maumivu kwa jamii.
Amesisitiza umuhimu wa kuwa na mjadala unaolenga mahitaji halisi ya wananchi badala ya kushughulikia matukio yasiyo na mchango katika maendeleo ya Taifa.
“Haya yanayosemwa huko yote ni upuuzi tu. Wazungu wana usemi wao kuwa wakati mwingine mambo ya kijinga huibuliwa ili kuhamisha jamii kwenye mjadala wa jambo la msingi. Hata haya yanaondoa mijadala ya kusaidia nchi kusonga mbele.
“Nchi yetu ina changamoto nyingi, ikiwemo gharama za mafuta kupaa. Haya yanayoendelea ni upuuzi; mijadala ingenikita kutafuta majawabu ya tatizo la mafuta,” amesema.
Dk Nkya amesisitiza kuwa kuendelea kwa mijadala ya namna hiyo katika mitandao ya kijamii huikosesha Serikali na wananchi nafasi ya kufuatilia na kupata majawabu ya matatizo mbalimbali yanayoikumba jamii.
Ametaja suluhisho kuwa ni elimu ya jamii na uwazi, akieleza kuwa ni muhimu kukuza utamaduni wa kukubali ukweli na kujadili matatizo halisi ya wananchi, akionya kuwa bila kufanya hivyo, jamii itaendelea kuhamishwa kutoka kwenye ajenda muhimu na kushindwa kupata suluhisho la changamoto zinazoikabili.
Wakati wadau wakitoa wito huo, tayari Jeshi la Polisi limetoa ufafanuzi, likikanusha uvumi unaosambaa na kuzua taharuki kuhusu matukio ya kupotea kwa viungo vya siri na kuitaka jamii kuacha kusambaza taarifa zisizo na uhakika.
Katika taarifa yake ya Aprili 4, 2026, Jeshi hilo liliweka wazi kuwa hakuna ukweli wala uthibitisho katika madai hayo yanayozushwa na kuzagaa kwenye mitandao ya kijamii na kujadiliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini.
Aidha, wadau wanabainisha kuwa changamoto kubwa katika hali hiyo siyo tu kupotea kwa ajenda muhimu, bali ni namna jamii inavyojikita kujadili na kufuatilia ajenda hizo ambazo hazina maslahi.
