Paroko alivyonusurika kifo madhabahuni, mshambuliaji auawa

Dar es Salaam/Mwanza. Paroko wa Parokia ya Kagunguli, wilayani Ukerewe, amenusurika kuuawa akiwa madhabahuni baada ya kijana kuvamia ibada ya Misa Takatifu ya Pasaka akiwa na panga.

Tukio hilo la kushtua lilitokea wakati wa misa, na mshambuliaji huyo aliwajeruhi waumini wawili, akiwemo mwanakwaya na mwenyekiti wa parokia, kabla ya kuzuiwa na wananchi waliokuwapo eneo la tukio.

Kwa mujibu wa mashuhuda, kijana huyo aliingia ghafla kanisani na kuanza kushambulia bila ya onyo, hali iliyozua taharuki miongoni mwa waumini waliokuwa wakishiriki misa hiyo.

Hata hivyo, wananchi, kwa kushirikiana na baadhi ya waumini, walifanikiwa kumdhibiti mshambuliaji huyo, ambaye baadaye aliuawa katika tukio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Aprili 5, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, kijana aliyefanya shambulio hilo ametambuliwa kuwa ni mkazi wa Kijiji cha Kagunguli, anayejulikana kwa jina la Renatus Silivester (38), maarufu Pacome.

Amesema tukio hilo, ambalo linaendelea kufanyiwa uchunguzi, lilitokea Jumapili ya Pasaka, saa 1:30 asubuhi, na mtuhumiwa aliingia kanisani kupitia mlango wa upande wa kulia akiwa amebeba mfuko na kuelekea moja kwa moja madhabahuni.

Kamanda Mutafungwa ameeleza kuwa hatua zaidi za kisheria na kiuchunguzi zinaendelea kuchukuliwa, ili kubaini chanzo na mazingira ya tukio hilo.

Tukio hilo linaongeza katika orodha ya matukio ya mashambulizi dhidi ya viongozi wa dini nchini na kuzua wasiwasi kuhusu usalama katika maeneo ya ibada, hususan wakati wa mikusanyiko mikubwa ya waumini.

Julai 2023, Paroko wa Parokia ya Karatu, mkoani Arusha, Pamphili Nada, aliuawa baada ya kushambuliwa na mtu anayesadikiwa kuwa na changamoto ya afya ya akili.

Mtuhumiwa huyo, Romani Leonard (30), ambaye naye aliuawa na wananchi, kabla ya kutekeleza shambulio hilo, aliingia kanisani kwa madai ya kutaka kusali.

Aidha, Aprili 30, 2025, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padre Charles Kitima, alishambuliwa kwa kitu butu kichwani akiwa nyumbani kwake Kurasini, Dar es Salaam, huku mtu mmoja alishikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.

Taarifa ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ya Mei mosi, 2025, ilieleza kuwa mtu mmoja anashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na shambulio dhidi ya Padri Kitima, huku jeshi hilo likieleza kuwa linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Kupitia taarifa yake kwa umma, Kamanda Mutafungwa amesema mwenyekiti wa parokia hiyo, Costantine Bituro (65), alimshtukia kijana huyo kutokana na mienendo yake na kumtoa nje ya kanisa.

“Wakati wakiendelea kumhoji, alitoa panga na kuwajeruhi watu wawili. Kutokana na kitendo hicho, kundi la waumini na wananchi waliokuwa nje ya kanisa walimdhibiti mtuhumiwa kwa kumpiga kwa silaha za jadi na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, waliojeruhiwa kwenye tukio hilo ni Bituro, alijeruhiwa kichwani na kwenye mikono yote na Aloyce Christopher (57), mwanakwaya, alijeruhiwa mkono wa kushoto.

Amesema majeruhi wote wamepelekwa Hospitali ya Kanda Bugando, jijini Mwanza, kwa matibabu zaidi na hali zao zinaendelea kuimarika.

“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo na kufuatilia hali ya majeruhi waliopelekwa hospitali,” amesema Mutafungwa.

Kuhusu mtuhumiwa, Kamanda Mutafungwa amesema wakati akikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe kwa matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata, alifariki dunia kabla ya kufikishwa hospitalini.