Dar es Salaam. Jamii imekumbushwa umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya kulinda utajiri sambamba na juhudi za kuujenga, ili kuhakikisha usalama wa kifedha wa muda mrefu.
Akizungumza katika kongamano la Women Shaping the Future 2026, lililoandaliwa na Shirika la Wakala (SRC) jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Meneja wa Bancassurance wa Alliance Life Assurance, Tumaini Pyanisa, amesema kuwa watu wengi hupuuza hatua muhimu ya kulinda mali zao na familia zao dhidi ya hatari zisizotarajiwa.
Amesema kuwa ingawa watu wengi wanafanikiwa kupata kipato, kuweka akiba na kuwekeza, bado huacha familia zao katika mazingira hatarishi kwa kukosa mipango ya ulinzi wa kifedha.
“Tunafanya kazi kwa bidii na kujenga kipato, lakini mara chache tunafikiria kulinda tulichokipata hadi pale tatizo linapotokea,” amesema.
Amefafanua kuwa hata watu wenye uwekezaji mzuri katika hati fungani za Serikali, hisa na amana za muda maalumu, wanaweza kukumbwa na changamoto kubwa iwapo hawana bima ya maisha, hasa panapotokea majanga kama ulemavu wa kudumu au kifo.
“Uwekezaji wako unakuza fedha zako, lakini haulindi maisha yako. Ikitokea jambo, familia yako itaendeleaje?” amehoji.
Akizungumzia utamaduni wa kusaidiana uliopo nchini, Pyanisa amekiri kuwa ni nguzo muhimu ya kijamii, lakini akaonya kuwa haupaswi kutegemewa kama suluhisho la kudumu la usalama wa kifedha.
“Jamii inaweza kusaidia kwa muda, lakini mustakabali wako wa kifedha unapaswa kutegemea maamuzi yako binafsi,” amesema.
Aidha, ameeleza kuwa kuna dhana potofu kuwa bima hupunguza uwezo wa kuwekeza, akisisitiza kuwa bidhaa za kisasa za kifedha, kama mipango ya endowment, zinawezesha mtu kuwekeza na kulinda maisha kwa wakati mmoja.
“Huweki tu akiba, bali pia unalinda mustakabali wako,” amefafanua.
Ameongeza kuwa hata taasisi za kifedha hulinda mali zao kupitia bima, hivyo ni muhimu kwa mtu binafsi kufanya hivyo pia.
“Kama taasisi zinalinda mali zao, kwa nini usilinde maisha yako ambayo ndiyo mali yako kubwa zaidi?” amehoji.
Kwa wale wanaohisi kuwa wamechelewa kuanza au hawana kipato kikubwa, Pyanisa amewashauri kuanza na kile walichonacho.
“Anza ulipo, hata kama ni kidogo. Uthabiti ni muhimu zaidi kuliko kiwango unachoanza nacho,” amesisitiza.
Ametoa wito kwa jamii kubadilisha mtazamo wa mafanikio ya kifedha, akisema kuwa mafanikio hayo hayapaswi kupimwa kwa kipato na uwekezaji pekee, bali pia kwa kiwango cha ulinzi na usalama wa kifedha. “Bima si uwekezaji tu, ni kulinda maisha,” amesema.
Kongamano hilo lililokuwa na kaulimbiu “Jenga Utajiri, Jenga Nguvu”, liliwakutanisha zaidi ya wanawake viongozi 200 kutoka taasisi mbalimbali. Washiriki walipata fursa ya kushiriki katika vipindi vya wataalamu, mijadala ya wazi, pamoja na warsha za ustawi wa kifedha, zilizolenga kubadili maarifa ya kifedha kuwa vitendo.
Katika kongamano hilo, Alliance Life Assurance iliendesha warsha maalumu iitwayo “Kulinda yenye thamani”, na Pyanisa aliwasilisha mada iliyolenga kuwahamasisha wanawake kujenga utajiri huku wakihakikisha wanajilinda kifedha.
