Dar es Salaam. Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kinondoni, Mrakibu Msaidizi wa Zimamoto, Jacob Chacha, amewahimiza Watanzania kuzingatia matakwa ya kisheria kwa kuomba ukaguzi wa majengo yao ili kujikinga na majanga ya moto.
Ametoa wito huo wakati anazungumza na Mwananchi leo, Aprili 6, 2026, jijini Dar es Salaam kufuatia tukio la moto lililodhibitiwa na jeshi hilo katika jengo la ghorofa sita la Orchid Apartment lililopo Masaki, ambapo vyumba viwili vya juu viliteketea.
Amesema jeshi hilo linafanya ukaguzi wa tahadhari na kinga dhidi ya moto kwa kuzingatia Sheria ya Zimamoto na Uokoaji ya mwaka 2007 pamoja na kanuni zake za mwaka 2008, sambamba na Sheria ya Majengo ya mwaka 2015, ambazo zinaelekeza namna ya kuhakikisha majengo yanakuwa salama.
“Nawaomba wananchi kutimiza matakwa ya kisheria kwa kuomba ukaguzi wa majengo yao. Jukumu la kulinda majengo si la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pekee, bali ni la wananchi wote,” amesema.
Ameshauri umuhimu wa kuwa na utaratibu wa mara kwa mara wa ukaguzi wa majengo na kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa zimamoto wanapotekeleza majukumu yao.
“Baada ya ukaguzi, jeshi huwa linatoa ripoti zenye ushauri wa kitaalamu ambao wamiliki wa majengo wanapaswa kuuzingatia ili kuimarisha usalama na kupunguza hatari ya majanga ya moto,” amesema.
Tukio la Orchid Apartment
Katika tukio hilo ambalo halikusababisha madhara kwa binadamu, isipokuwa hasara ya mali zilizokuwa ndani ya vyumba hivyo, Kamanda Chacha amesema lilitokea leo saa 11:28 alfajiri.
“Baada ya Jeshi la Zimamoto kupata taarifa na kufika eneo la tukio, moto ulikuwa bado unawaka kwa kutumia mitambo yetu pamoja na askari, tulianza juhudi za kuuzima moto huo.”
“Tulikuta jengo hili la ghorofa lenye wapangaji, ambapo chumba kimoja kilichopo ghorofa ya sita kilikuwa kinateketea kwa moto.
Katika tukio hilo, ambalo pia lilitembelewa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kujionea hali ilivyokuwa, Kamanda Chacha amesema uchunguzi wa awali umebaini chanzo ni hitilafu ya kwenye kiyoyozi.
Amesema hitilafu hiyo ilisababisha cheche zilizoangukia kwenye godoro na kusababisha moto kusambaa ndani ya chumba hicho.
Amesema kabla ya jeshi kufika, wapangaji wa eneo hilo walijaribu kuuzima moto huo lakini walishindwa kuudhibiti hadi Jeshi la Zimamoto lilipofika na kufanikiwa kuuzima.
