Peter Lwasa aahidi makubwa Pamba Jiji

KIUNGO mshambuliaji wa Pamba Jiji, Peter Lwasa ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao manane akiwa Kagera Sugar, amesema hajawa na mwendelezo mzuri wa kufumania nyavu msimu huu kutokana na kutocheza mechi mfululizo.

Huu ni msimu wa kwanza kwa kiungo huyo raia wa Uganda kuitumikia Pamba Jiji ya Mwanza akisajiliwa kutokea Kagera Sugar iliyoshuka daraja msimu wa 2024-2025 na sasa inashiriki Ligi ya Championship.

Akizungumza na Mwanaspoti, Lwasa amesema mabao yake matatu na asisti tatu alizohusika nazo msimu huu, sio rekodi nzuri sana kwa upande wake na takwimu hizo zinaonyesha hajafanya vizuri kutokana na kutokuwa na muendelezo mzuri wa kucheza mechi.

“Nimefunga magoli matatu na kutoa asisti tatu hadi sasa, lakini siyo kweli niko kwenye kiwango cha juu, kwa sababu nimeshindwa kucheza mechi nyingi mfululizo,” amesema Lwasa.

Amefafanua pamoja na hilo, wanapambana kwa ajili ya mafanikio ya timu ambayo ndio kipaumbele zaidi kuliko malengo ya mchezaji mmoja.

“Nadhani ni kuhusu utendaji wa timu, ambao kwa sasa unazingatia malengo ya timu kuliko malengo binafsi ya mchezaji mmoja mmoja,” amesema.

Ameongeza kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia malengo ya timu, ataweza kurudi kwenye kiwango cha kufunga na kufikia malengo yake binafsi.

“Tunaendelea kufanya kazi kwa ajili ya timu, na kwa njia hiyo, naamini nitafanikiwa na kurudi kwenye kiwango changu cha kufunga magoli,” amesema nyota huyo