Tume ya Oktoba 29, yaongezewa tena siku 21

Dar es Salaam. Baada ya kufanya kazi kwa takriban miezi minne, hatimaye Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya kabla na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 imeomba na kuongezewa tena muda wa siku nyingine 21 kukamilisha kazi.

Hiyo ni nyongeza ya pili ya muda kwa Tme hiyo, ambayo Februari 20, mwaka huu iliongezewa siku 42 za kukamilisha kazi yake, baada ya zile 90 ilizopewa kuifanya kazi hiyo kwa mujibu wa hadidu za rejea kutamatika.

Tume hiyo, iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuanza kazi Novemba 20, 2025, ilipewa siku 90 kuifanya kazi hiyo, zilizoisha Februari 20, mwaka huu.

Siku hizo hazikuitosha Tume kukamilisha kazi hiyo, ikaomba na kuongezewa nyingine 42, ambazo zilikamilika Aprili 3, 2026.

Hizo nazo hazikutosha na sasa imepewa nyingine 21 na kutakiwa kukamilisha kazi hiyo kabla au ifikapo Aprili 24, 2026.

Tume hiyo yenye wajumbe tisa ikiongozwa na Mweyekiti, Jaji Mkuu mstaafu Othman Chande, iliundwa kufanya uchunguzi wa maandamano yaliyozaa vurugu siku ya uchaguzi na baada. Matukio hayo yalisababisha vifo, uharibifu wa miundombinu ya umma na mali za watu binafsi.

Taarifa ya kuongezwa kwa muda huo wa siku 21, imetolewa Aprili 4, 2026 katika Gazeti la Serikali namba NSSN 0856-0323, toleo la 2, ikimrejea Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Othman Chande.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, Tume  imeomba nyongeza hiyo ya muda ili kukamilisha uchambuzi wa ushahidi, taarifa na maoni yaliyopokelewa.

“Kutoa fursa kwa wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi kufanyia kazi baadhi ya vielelezo vipya vilivyowasilishwa,” imeandikwa katika sehemu ya maombi hayo yaliyochapishwa kwenye gazeti hilo.

Pia, kuiwezesha kukamilisha maandalizi ya ripoti itakayowasilishwa kwa Rais na kutoa fursa kwa Tume kuandaa tafsiri ya ripoti.

Hata hivyo, imeeleza  baada ya kuongezwa muda wa siku 42 za awali, wananchi waliendelea kujitokeza kwa wingi tofauti na ilivyotarajiwa.

Hiyo ikafanya Tume hiyo iendelee kupokea ushahidi, taarifa na maoni zaidi na kushindwa kukamilisha kazi yake ndani ya muda wa nyongeza uliotolewa, ndiyo maana imeomba tena.

“Umma unataarifiwa kuwa, mamlaka ya uteuzi imeridhia maombi ya muda wa ziada wa Tume kukamilisha kazi na imeongeza muda wa siku 21 na kuitaka ikamilishe kazi kabla au ifikapo Aprili 24, 2026,” imeeleza sehemu ya taarifa iliyochapishwa  kwenye gazeti hilo.

Katika maelezo yake, imeeleza Tume hiyo inawashukuru wananchi na wadau waliotoa ushirikiano wakati wa kufanya uchunguzi, kupitia njia mbalimbali ikiwemo kupiga simu, kutuma ujumbe, maoni kwa maandishi na waliowasiliana na Tume kwa njia za mitandao ya kijamii.