Urithi utakaokumbukwa kwa Karume | Mwananchi

Dar es Salaam. Leo ni miongo mitano na miaka minne tangu alipotwaliwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, huku wadau wa siasa wakimkumbuka kwa misingi aliyoiasisi, ambayo baadhi wanadai imeachwa.

Karume alifariki dunia Aprili 7, 1972, baada ya kupigwa risasi Kisiwandui, Unguja, visiwani Zanzibar, zilipokuwa ofisi za Makao Makuu ya Chama cha Afro Shiraz.

Wadau wa siasa wameukumbuka uongozi wake, wakiutaja kuwa uliojenga misingi ya umoja na mshikamano, huku wengine wakisema mtindo wake wa kujenga ustawi wa jamii ni kama umelegalega kwa sasa.

Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Paul Kimiti, amesema Karume alisimamia umoja na mshikamano wa wananchi, akihimiza watu kuishi kama ndugu, hali iliyorahisisha kufikiwa kwa Muungano.

Amesema msingi wa umoja aliouweka Karume unapaswa kuendelezwa na jamii, kwani una uwezo wa kulipeleka Taifa mbele zaidi kuliko migawanyiko, huku akionya dhidi ya kauli zinazoibua tofauti za Uzanzibar na Utanganyika.

“Maneno ya Uzanzibar na Utanganyika hayana tija katika jamii yetu. Katika dunia ya leo hakuna sababu ya kubaguana. Karume na Julius Nyerere walifanya kazi kubwa ya kutuunganisha, hivyo ni wajibu wetu kuenzi na kulinda tunu hiyo,” amesema.

Mchambuzi wa siasa za Zanzibar, Ali Makame, amesema kuwa wakati wa utawala wake, Karume aliweka mbele ustawi wa wananchi kwa kuhakikisha hali zao za maisha zinaboreshwa. Alianza kwa kuboresha makazi, ambapo wananchi walijengewa nyumba bora mijini na vijijini.

Amesema Karume alikuwa kiongozi aliyeacha alama zisizofutika, kwa kuwa sera zake zilikuwa zinagusa moja kwa moja maisha ya wananchi. Pia, alianzisha mfumo wa kuwalipa pensheni wazee wote bila kujali kama walikuwa watumishi wa umma au la.

“Pamoja na kuwa na kiwango kidogo cha elimu, alikuwa na hekima nyingi na ubunifu mkubwa katika kufanya mambo yaliyogusa maisha ya wananchi,” amesema.

Mchambuzi wa masuala ya sera za jamii, Profesa Ibrahimu Tambu, amesema msingi wa utawala wa Karume ulikuwa ni sera za ustawi wa jamii zilizogusa moja kwa moja maisha ya wananchi wa kawaida.

Ametaja elimu bure, huduma za afya bure na makazi bora kuwa zilikuwa nguzo zilizojengwa katika kipindi chake, akilenga kupunguza pengo la kijamii mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ingawa sera hizo zilikuwa na nguvu wakati wa Karume, amesema sehemu ya mfumo huo imepungua au kubadilika kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na kisera.

“Kwa mfano, baadhi ya huduma ambazo zilikuwa bure, kwa sasa zinachangiwa na wananchi, hali inayozua mjadala kuhusu urithi wa ustawi wa jamii aliouasisi hayati Karume,” amesema.

Amesema Karume aliweka msingi wa mfumo wa pensheni kwa wazee, hatua iliyolenga kuhakikisha heshima kwa watu waliotumikia jamii.

Hata hivyo, amesema mfumo huo umepitia mabadiliko ya kiutendaji na changamoto za kifedha katika miaka ya baadaye.

Kwa upande wa mchambuzi wa siasa, Dk Salma Mbarouk, amesema Karume alijenga uchumi wa Zanzibar kwa kulipa kipaumbele zao la karafuu, ambalo lilikuwa uti wa mgongo wa mapato ya Taifa hilo.

Katika kipindi chake, amesema karafuu ilitumika kama nyenzo kuu ya kupata fedha za kigeni na kuiwezesha Serikali kugharamia huduma za kijamii.

Hata hivyo, amesema kuwa utegemezi mkubwa wa zao moja uliacha changamoto ya muda mrefu, hasa baada ya bei za soko la dunia kubadilika na uzalishaji kupungua kwa miaka iliyofuata.

“Hili ni moja ya maeneo ambayo yangehitaji kuendelezwa kwa mseto zaidi wa uchumi,” amesema.

Amesema Karume pia alikuwa na msimamo mkali dhidi ya mikopo ya nje, akiamini katika kujitegemea kiuchumi.

Msimamo huo, Dk Salma amesema, ulisaidia kuimarisha uhuru wa fedha wa wakati huo, lakini pia uliweka changamoto ya upatikanaji wa mtaji wa maendeleo ya muda mrefu.