Tunashindwaje kuanzisha karakana za madawati?

Katika kipindi ambacho Taifa linaendelea kujivunia mafanikio katika sekta mbalimbali za maendeleo, bado kuna doa lisilofutika katika sekta ya elimu; uhaba wa madawati shuleni.

Hivi karibuni baada ya kushuhudia ukubwa wa changamoto hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda aliagiza halmashauri zote mkoani humo kuanzisha karakana maalum za kutengeneza madawati.

Hii ni hatua ya kimapinduzi inayolenga kutibu tatizo sugu kwa suluhisho la kudumu. Ni wazo linalopaswa kuigwa kitaifa, kwa sababu tatizo la uhaba wa madawati si la Mwanza pekee, bali ni changamoto inayokumba shule nyingi kote Tanzania.

Kwa miaka mingi, shule za msingi na sekondari nchini zimekuwa zikikabiliwa na uhaba mkubwa wa madawati.

Ongezeko la wanafunzi linalotokana na sera ya elimu bila malipo limekuwa jambo jema na la kupongezwa, lakini maandalizi ya miundombinu hayakwenda sambamba na kasi ya uandikishaji.

Matokeo yake, madarasa yamejaa wanafunzi kupita kiasi huku madawati yakibaki haba.

Katika baadhi ya maeneo ya vijijini, wanafunzi wamekuwa wakikaa chini sakafuni, wengine juu ya mawe au magogo ya miti.

Picha hizi zimekuwa zikisambaa mara kwa mara na kuzua mjadala mpana katika jamii. Inasikitisha kuona kwamba katika nchi iliyojaaliwa rasilimali nyingi za misitu na miti, bado shule zinakosa madawati ya kutosha.

Tatizo hili si la leo. Limekuwepo kwa miongo kadhaa, likirithiwa kutoka awamu moja ya uongozi hadi nyingine. Kila mara kumekuwa na kampeni za muda mfupi za uchangishaji au misaada kutoka kwa kampuni na wahisani, lakini jitihada hizo zimekuwa za kuzima moto badala ya kuleta suluhisho la kudumu. Ni aibu kwamba katika karne ya 21, wanafunzi bado wanakaa chini wakati wa kujifunza.

Kimsingi, tatizo haliko katika ukosefu wa uwezo, bali katika ukosefu wa ubunifu na mipango thabiti ya ndani. Halmashauri nyingi zina mafundi seremala, zina majengo yanayoweza kubadilishwa kuwa karakana, na zina uwezo wa kununua malighafi za kutengeneza madawati.

Hata hivyo, mara nyingi kumekuwepo na mtazamo wa kusubiri msaada kutoka nje badala ya kujitegemea.

Inapotokea kiongozi anashtushwa na hali halisi na kuchukua hatua ya haraka, hapo ndipo mabadiliko ya kweli huanza. RC Mtanda alipoona idadi ya wanafunzi wasiokuwa na madawati, hakuridhika na taarifa za makaratasi pekee.

Hatua yake ya kuagiza kila halmashauri kuanzisha karakana za kutengeneza madawati ni ushahidi wa uongozi unaojali na unaotafuta suluhisho la kudumu.

Karakana hizi zinaweza kuwa chanzo cha ajira kwa vijana wa eneo husika, zikaongeza ujuzi wa ufundi seremala, na wakati huo huo zikahakikisha kila shule inapata madawati ya kutosha kwa wakati.

Zaidi ya hayo, kuanzishwa kwa karakana kunapunguza gharama za ununuzi wa madawati kutoka kwa wazabuni wa mbali.

Badala ya kusubiri zabuni, kusaini mikataba na kusubiri miezi kadhaa, halmashauri zinaweza kuzalisha madawati yao wenyewe kulingana na mahitaji halisi ya shule zao.

Hili ni wazo linaloweza kupanuliwa zaidi. Mbali na madawati, karakana hizo zinaweza kutengeneza meza za walimu, makabati, viti na hata kufanya matengenezo ya miundombinu ya shule. Kwa kufanya hivyo, halmashauri zitakuwa zimejenga mfumo endelevu wa uzalishaji na matengenezo.

Ni wakati sasa wa kugeuza wazo hili kuwa sera ya kitaifa. Kila wilaya au halmashauri nchini inapaswa kuwa na kitengo maalum cha kutengeneza madawati na samani za shule. Hili si jambo lisilowezekana; ni suala la uamuzi na vipaumbele.

Ni aibu kila siku kusubiri misaada ya madawati kutoka kwa kampuni na wahisani kana kwamba taifa halina uwezo wa kujitegemea.

Misaada ni muhimu pale panapohitajika, lakini haipaswi kuwa suluhisho la kudumu kwa tatizo la msingi kama hili.

Katika nchi yenye rasilimali ya kutosha ya miti na nguvu kazi ya vijana, kushindwa kutengeneza madawati ya kutosha ni ishara ya uzembe au kukosa mipango madhubuti.

Tunapaswa kujifunza kwamba maendeleo ya kweli yanatokana na kujitegemea.

Serikali kuu inaweza kuweka mwongozo wa kitaifa unaotaka kila halmashauri kuanzisha karakana ndani ya kipindi fulani maalum.

Aidha, vyuo vya ufundi vinaweza kushirikishwa kutoa mafunzo kwa mafundi watakaofanya kazi katika karakana hizo. Ushirikiano kati ya sekta ya elimu na ile ya ufundi unaweza kuleta mapinduzi makubwa.

Kwa kufanya hivyo, tatizo la madawati litakuwa historia. Wanafunzi watasoma katika mazingira bora, watapata motisha zaidi, na matokeo ya kitaaluma yataimarika. Heshima ya taifa katika sekta ya elimu itaongezeka.

Kwa hakika, kongole kwa RC Mtanda kwa kuthubutu kufikiria tofauti na kuchukua hatua. Wazo la karakana za madawati si tu suluhisho la Mwanza, bali ni mwanga unaoweza kuangaza taifa zima.

Ni wakati sasa wa kuacha visingizio na kuchukua hatua madhubuti kwa sababu katika karne ya 21, hakuna sababu ya mwanafunzi wa Tanzania kukaa chini wakati akijifunza.

Kwa hali ilivyo, uanzishaji wa karakana za utengenezaji wa madawati katika ngazi za halmashauri si pendekezo la kawaida bali ni wito wa mabadiliko ya kimfumo katika usimamizi wa elimu nchini.

Ni dhahiri kuwa changamoto ya upungufu wa madawati imekuwepo kwa muda mrefu, lakini suluhisho lake halihitaji miujiza, bali linahitaji uamuzi, ubunifu na uthubutu wa viongozi wetu wa ndani.

Halmashauri zina mamlaka, rasilimali na ukaribu na jamii; kinachohitajika ni kuunganisha nguvu hizi na kuzigeuza kuwa matokeo yanayoonekana.

Kila siku tunayoichelewesha hatua hii, tunachelewesha pia ndoto za maelfu ya wanafunzi wanaolazimika kujifunza katika mazingira yasiyostahili. Hili si suala la miundombinu pekee, bali ni suala la haki na usawa katika elimu.

Mtoto anayekaa chini darasani ananyimwa fursa sawa ya kujifunza ukilinganisha na anayekaa kwenye dawati. Hivyo basi, hatua ya kuanzisha karakana hizi ni hatua ya kurejesha heshima na hadhi ya mwanafunzi wa Kitanzania.

Ni wajibu wa kila mdau kuanzia viongozi wa serikali za mitaa, wabunge, walimu hadi wazazi, kuona umuhimu wa wazo hili na kulisukuma kwa nguvu zote.

Mabadiliko haya hayawezi kusubiri tena mipango ya muda mrefu isiyo na utekelezaji; yanahitaji hatua za haraka na zenye matokeo ya moja kwa moja. Historia itawahukumu kwa matendo yao wale wenye uwezo wa kufanya mabadiliko lakini wakasita kuchukua hatua.

Kwa hiyo, wakati wa majadiliano umepita; huu ni wakati wa utekelezaji. Tukiamua kwa dhati, tunaweza kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anapata dawati, na kwa kufanya hivyo, tunajenga msingi imara wa elimu bora na taifa lenye maarifa, usawa na maendeleo endelevu.