Dar es Salaam. Utekelezaji wa Sera ya Elimu ya elimu na Mafunzo unaendelea kuchukua sura mpya nchini, huku Serikali ikijiandaa kukabiliana na changamoto ya ongezeko kubwa la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza ifikapo mwaka 2028.
Katika mwaka huo, Tanzania inatarajiwa kushuhudia madarasa mawili ya wanafunzi kutoka elimu ya msingi yakijiunga kwa pamoja na kidato cha kwanza, hali itakayoongeza idadi ya wanafunzi wanaohitaji nafasi katika shule za sekondari.
Kwa mujibu wa Serikali, maandalizi ya kukabiliana na hali hiyo tayari yameanza kwa kuimarisha miundombinu ya elimu katika maeneo mbalimbali nchini.
Lakini si uimarishaji wa mundombinu pekee, Serikali pia inaendelea na mchakato wa kuishirikisha sekta binafsi kuhakikisha hakuna mtoto atakayeachwa nyuma mwaka huo.
Akizungumza bungeni Aprili 2, 2026 Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba alisema Serikali tayari imeanza kufanya tathmini ya mahitaji ya miundombinu ya elimu katika ngazi za mikoa na halmashauri.
Alisema wakuu wa mikoa pamoja na timu za serikali za mitaa wamepewa maelekezo ya kufanya maoteo ya mahitaji ya madarasa na miundombinu mingine ya shule, ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa nafasi ya kuendelea na masomo.
Hatua hiyo inalenga kuweka takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga rasilimali na miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kabla ya mwaka 2028 kufika.
Alisema moja ya mikakati mikubwa inayotekelezwa na Serikali, ni kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya sekondari.
Wakati awali mpango ulikuwa kuhakikisha kila kata ina shule ya sekondari, sasa mwelekeo umebadilika na kulenga kuwa na shule ya sekondari katika kila kijiji.
“Kutokana na mpango huo, kila kijiji kinatarajiwa kuhitaji angalau madarasa matatu ya ziada ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi watakaojiunga na sekondari” alisema Dk Mwigulu.
Tathmini ya awali inaonyesha kuwa ili kufanikisha mpango huo, nchi itahitaji kujenga zaidi ya madarasa 23,200 pamoja na maabara mpya 9,300.
Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kugharimu takribani Sh1trilioni, fedha zitakazotumika katika ujenzi wa madarasa, maabara pamoja na miundombinu mingine muhimu katika shule za sekondari.
Katika maeneo ambayo hayakuwa na shule za sekondari hapo awali, Serikali imepanga kuongeza angalau madarasa matatu pamoja na maabara ili kuhakikisha wanafunzi wa maeneo hayo hawakosi fursa ya kuendelea na elimu.
Mkakati mwingine anasema ni ujenzi wa shule za muundo mpya zinazounganisha shule ya msingi na sekondari katika eneo moja.
“Mpaka sasa, zaidi ya shule 6,000 za aina hiyo tayari zimejengwa katika maeneo mbalimbali nchini. Shule hizo zinatarajiwa kusaidia kupunguza umbali ambao wanafunzi hulazimika kusafiri kwenda kupata elimu ya sekondari,”anasema.
Mbali na hilo, shule za sekondari zilizopo katika makao makuu ya kata pia zinatarajiwa kusaidia kupokea wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza katika mpango huo.
Ubia Serikali na sekta binafsi
Kwa upande mwingine, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi zimeanza kuchora ramani mpya ya ushirikiano katika elimu ya sekondari kupitia mpango wa ubia baina ya sekta ya umma na binafsi (PPP), hatua inayolenga kukabiliana na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, anasema pande hizo bado zinaendelea na majadiliano, ili kubaini mfumo utakaowezesha ushirikiano huo kutekelezwa kwa manufaa ya pande zote.
“Ni kweli tuko kwenye majadiliano, lakini bado hatujafikia uamuzi ni modeli ipi itatufaa ambayo itakuwa na manufaa kwa pande zote mbili. Tunafahamu kuna shule nyingi binafsi hazina wanafunzi, hivyo tunaona uwezekano wa kupeleka wanafunzi huko, lakini lazima tufikie mwafaka kwa kuangalia modeli sahihi ya kwenda nayo,” anasema alipoulizwa na Mwananchi hivi karibuni.
Kwa upande wake, Ofisa mtendaji mkuu wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali Tanzania (Tamongsco), Benjamin Nkonya, anasema mpango huo ni matokeo ya tathmini ya kina iliyofanywa kwa kushirikiana na wizara, baada ya kubaini kuwa idadi ya wanafunzi inaongezeka kwa kasi kuliko uwezo wa miundombinu ya shule za Serikali.
Akizungumza na Mwananchi, Nkonya alisema Tamongsco imeona ongezeko la wanafunzi wa sekondari litakalojitokeza mwaka 2028 na hivyo kuamua kushiriki kikamilifu kutafuta ufumbuzi.
“Kama sekta binafsi, tuliona hatuwezi kukaa pembeni. Ndiyo maana tumeamua kushirikiana na Serikali kuhakikisha elimu inayotolewa inaendelea kuwa bora,” anasema.
Anaeleza kuwa makubaliano hayo yameruhusu shule zisizo za Serikali kushiriki kupokea wanafunzi waliopaswa kujiunga na shule za Serikali kupitia mifumo minne ya mikataba, kila mmoja ukiwa na masharti yake kulingana na uwezo na makubaliano ya pande husika.
Kwa mujibu wa Nkonya, mfumo wa kwanza ni Serikali kuwapeleka wanafunzi katika shule binafsi na kulipia ada kamili kulingana na kiwango kitakachopangwa na bodi ya shule husika.
Mfumo huu unalenga shule zenye miundombinu tayari na uwezo wa kupokea wanafunzi wengi bila kuhitaji uwekezaji mkubwa wa awali.
Mfumo wa pili unahusisha Serikali kupeleka wanafunzi kwenye shule hizo huku ada ikilipwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na mzazi. Mfumo huu unalenga kuwapa wazazi nafasi ya kuchangia sehemu ya gharama ili kupunguza mzigo kwa Serikali.
Mfumo wa tatu unahusisha Serikali kukokotoa gharama za mwanafunzi kusoma katika shule husika, ambapo endapo mmiliki wa shule ataridhika na ukokotoaji huo, atasaini mkataba wa kushiriki mpango huo.
“Hapa tunataka uwazi na uhalisia wa gharama. Shule itakubali kwa hiari ikiwa itaona ina uwezo wa kuendana na kiwango kilichopangwa,” anasema.
Mfumo wa nne unahusisha shule binafsi kutoa majengo bila Serikali kulipa ada yoyote. Badala yake, Serikali italeta wanafunzi 30 kwa kila darasa pamoja na walimu, huku shule ikiendelea na udahili wake wa kawaida wa wanafunzi 15 wanaolipa ada.
Hivyo, darasa litakuwa na jumla ya wanafunzi 45, idadi inayolingana na viwango vinavyopendekezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).
Hata hivyo, Nkonya anasisitiza kuwa shule zitakazoshiriki mpango huo zitalazimika kuzingatia kwa umakini idadi ya wanafunzi zitakazowapokea ili kuepuka kuathiri ubora wa elimu.
Wadau wa elimu wamepokea mpango huo kwa hisia mseto, wengi wakiupongeza kama hatua ya ubunifu lakini wakitaka uangalizi wa karibu.
Mtaalamu wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Stella Mrema, anasema ubia wa Serikali na sekta binafsi, unaweza kusaidia kupunguza msongamano shuleni hasa ikiwa utasimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji.
“Sekta binafsi ina rasilimali na uzoefu wa kusimamia shule. Ushirikiano huu unaweza kuwa suluhisho, lakini lazima kuwe na mifumo imara ya ufuatiliaji ili kuhakikisha maslahi ya mtoto yanatangulizwa,” anasema.
Kwa upande wa wazazi, maoni yanatofautiana. Mkazi wa Temeke, Rashid Kiwelu, anasema mpango huo ni fursa kwa watoto kupata mazingira bora ya kujifunzia.
“Kama mtoto atasoma shule binafsi lakini Serikali inashirikiana, hiyo ni nafuu. Ila tunataka uhakika wa gharama zisizotuumiza,” anasema.
Naye mmiliki wa shule binafsi mkoani Morogoro, Neema Komba, anasema mpango huo unaweza kuimarisha uwekezaji katika elimu.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukijenga kwa tahadhari kwa hofu ya kutopata wanafunzi. Ushirikiano huu unatupa uhakika na motisha ya kuwekeza zaidi,” anasema.
