Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya siku tatu kuhusu uwezekano wa mvua kubwa zitakazoweza kusababisha mafuriko ya katika baadhi ya mikoa ya Pwani, ikiwamo Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA leo Jumanne Aprili 7, 2026, imesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza kesho Jumatano hadi Ijumaa, zikihusisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Pwani pamoja na Jiji la Dar es Salaam, sambamba na visiwa vya Unguja na Pemba.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uwezekano wa kunyesha kwa mvua hizo pamoja na athari zake umeainishwa kuwa wa kiwango cha kati, lakini wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari zote muhimu.
“Kuanzia kesho hadi Ijumaa, mvua zinatarajiwa kunyesha katika maeneo tajwa. Uwezekano na athari zake zipo katika kiwango cha kati,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, TMA imeonya kuwa mvua hizo zinaweza kusababisha mafuriko ya maeneo katika baadhi ya sehemu na kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.
Wananchi, hususan wanaoishi maeneo ya pwani na visiwani, wametakiwa kuwa waangalifu zaidi kutokana na uwezekano wa ongezeko la kiwango cha mvua.
“Umma unashauriwa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuchukua tahadhari stahiki,” imeongeza taarifa hiyo.
TMA imeeleza itaendelea kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa na kutoa taarifa zaidi kadiri itakavyohitajika.
