Kocha Yanga aibuka na matatu hesabu za ubingwa Bara

YANGA ina hesabu zake za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tano mfululizo, lakini katika hilo, inakumbana na vikwazo mbalimbali ikiwemo majeraha ya nyota wake wa kikosi cha kwanza na baadhi wameanza kurudi akiwemo Ibrahim Bacca, lakini itaendelea kuwakosa Clement Mzize na Dickson Job hadi mwisho wa msimu.

Kabla ya mambo hayajaharibika zaidi, uongozi wa klabu hiyo ukatangaza, baada ya kufanya tathmini ya mzunguko wa kwanza, umebaini mbali na changamoto hizo, kuna shida katika mbinu za ufundishaji, ndipo ikamrudisha Abdihamid Moalin aliyekuja kusaidiana na Kocha Mkuu, Pedro Goncalves.

Tangu kutua kwa Moallin ambaye alikuwepo kikosini hapo msimu uliopita wakati Yanga ikishinda Kombe la Muungano, Kombe la FA na Ligi Kuu Bara, timu hiyo imerudi katika njia ya ushindi ikiifunga Tanzania Prisons 3-0, kabla ya hapo ilitoka sare tatu mfululizo dhidi ya Azam (0-0), TRA United (0-0) na Mtibwa Sugar (1-1), matokeo yaliyohatarisha mbio zao za kuwania ubingwa.

Akizungumza na Mwanaspoti siku chache baada ya kurejea Yanga, Moalin amesema majukumu yake makubwa ni kumsaidia Goncalves na hatua ya kwanza watasaidiana kusimamisha matokeo ya sare yaliyowaandama kwenye mechi za karibuni yasijirudie tena kipindi hiki wanapowania ubingwa.

Kocha huyo amesema anaamini Goncalves ni kocha mzuri sambamba na wenzake aliowakuta na jambo lingine katika jukumu lao litakuwa kuunganisha nguvu kama benchi la ufundi na kufanya kazi kwa umoja, huku pia wakiwa na jukumu la kuwasaidia wachezaji kuimarika ili kurudi njia ya ushindi.

“Mimi sitaki kuongea sana, unajua hii Yanga ni timu kubwa hapa Tanzania na Afrika, uwepo wetu hapa tunatakiwa kushirikiana kusimamisha matokeo ya kuangusha pointi, hiki siyo ambacho mashabiki wanakitaka wala kukivumilia,” amesema Moalin.

“Nilikuwa hapa asilimia kubwa ya wachezaji nawajua vizuri, nitakuwa msaidizi wa kocha mkuu kushauriana namna gani ya kuwaimarisha zaidi wachezaji ili waweze kurudi kwenye kushinda mechi.

“Bahati nzuri sana timu haijapoteza mchezo wowote kitu ambacho kinaleta presha ni matokeo ya sare, hili tunatakiwa kuunganisha nguvu kuliondoa na timu iweze kuwa na matokeo ambayo yatarudisha imani kwenda kutetea ubingwa wetu.”

Aidha Moalin aliongeza, bado Yanga ina kikosi bora na kama wachezaji watarejea kutoka kwenye majeruhi, timu hiyo itarudi kwenye njia ya kuendeleza vipigo kwa timu pinzani.

“Kila mchezaji ambaye alikuwa bora msimu uliopita bado yupo hapa, tatizo ni baadhi ya wachezaji kuwa majeruhi, nadhani ni suala la muda wakipona timu itarudi njia yake ya kuendelea kushinda.”

Msimu uliopita baada ya kuondoka kwa kocha Sead Ramovic, Moalin aliiongoza Yanga kushinda mechi moja ya ligi kwa mabao 6-1 dhidi ya KenGold ambayo ilishuka daraja mara baada ya msimu huo kumalizika.