Chipukizi yashikilia hatma ya New Stone

WAKATI New Stone Town ikiwa na hali mbaya katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), hivi sasa hatma yao ya kusalia katika ligi hiyo imeshikiliwa na Chipukizi.

Hiyo inatokana na hesabu zilivyo kwani New Stone inayoburuza mkia katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi tatu ikibakiwa na mechi nane, huku kituo kinachofuata ni dhidi ya Chipukizi inayopambana pia kutoka kwenye mstari wa kushuka daraja kwani kabla ya jana haijashuka dimbani, ilikuwa na pointi 25 ikiwa nafasi ya 12.

New Stone katika mechi nane zilizobaki ambazo ni sawa na pointi 24, endapo ikizikusanya zote hizo, itamaliza msimu na pointi 27 kutokana na sasa kuwa nazo tatu.

Pointi hizo 27 kwa sasa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar inazo Mafunzo iliyokuwa nafasi ya 11 kabla ya jana Chipukizi haijacheza dhidi ya Uhamiaji.

Kwa sasa timu nne ambazo zipo katika mstari wa kushuka daraja ni Polisi iliyopo nafasi ya 13 na pointi 25, Malindi ya 14 na pointi 24, huku Junguni ya 15 ikikusanya pointi 10, kisha New Stone ya mwisho na pointi tatu.

Ili New Stone iendelee kuwa na matumaini ya kupigania nafasi ya kubaki kwenye ligi katika mechi nane zilizosalia, inatakiwa kutopoteza wala kutoka sare dhidi ya Chipukizi zitakapokutana raundi ijayo ya 23, mechi iliyopangwa kuchezwa Aprili 19 mwaka huu.

Endapo ikipambana na kuambulia sare, maana yake itakuwa na nafasi ya kupigania pointi 21 katika mechi saba zijazo na kuifanya kuwa na uwezekano wa kumaliza na pointi 25 ambazo haziwezi kumtoa kwenye mstari mwekundu. Ikipoteza basi itakuwa na uwezo wa kumaliza na pointi 24 ambazo pia ni hatari kwake.

Wakati New Stone ikipiga hesabu hizo za ushindi, inatakiwa pia kuzidisha maombi wapinzani wake walio juu wapoteze mechi zote jambo ambalo siyo rahisi.

Ugumu zaidi unakuja kutokana na New Stone katika mechi 22 ilizocheza hadi sasa, imeshinda moja pekee dhidi ya Zimamoto, huku ikipoteza 21, haina sare.

Pia timu hiyo imeruhusu mabao mengi zaidi ambayo ni 63, yenyewe ikifunga 14 yakiwa pia ni amchache zaidi kulinganisha na timu zote shiriki katika ligi hiyo.

Tofauti hiyo ya mabao na wastani wa kupata ushindi sambamba na pointi ilizonazo, inazidi kuinyima nafasi New Stone ya kusalia katika ligi hiyo msimu ujao.

Ikumbukwe baada ya ligi hiyo kurejea Machi 28 mwaka huu iliposimama kwa takribani mwezi mmoja kupisha mfungo wa Ramadhan, imeshuhudiwa New Stone ikipoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Mlandege (5-2) na Polisi (3-1).