Trump Awageukia Waandishi, Atishia Kuwapeleka Jela

Global Publishers
April 7, 2026
0 Comments

Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuwachukulia hatua kali, ikiwemo kuwafunga jela waandishi wa habari waliotoa taarifa za siri kuhusu operesheni ya kijeshi nchini Iran.

Kauli hiyo imekuja baada ya taarifa kuvuja zikidai kuwa kulikuwa na mwanajeshi wa pili wa Marekani aliyekwama ndani ya Iran kufuatia kudunguliwa kwa ndege ya kivita.

Akizungumza Ikulu, Trump alisema uvujaji huo uliweka maisha ya mwanajeshi hao hatarini na kufanya operesheni ya uokoaji kuwa ngumu zaidi.

“Hilo ni suala la usalama wa taifa. Tutawafuata waliotoa taarifa na tutachukua hatua kali,” alisema.

Kwa mujibu wa maelezo ya serikali ya Marekani, marubani wawili waliokuwa kwenye ndege hiyo waliokolewa katika operesheni mbili tofauti na hatari.

Rubani wa kwanza aliokolewa haraka, huku wa pili akikaa kwa zaidi ya siku moja ndani ya eneo la Iran kabla ya kuokolewa na vikosi vya Marekani.

Trump na maafisa wake wa ulinzi walisifu operesheni hiyo, wakisema ilikuwa miongoni mwa operesheni ngumu zaidi kuwahi kufanyika kijeshi.

Kauli ya Trump imeibua mjadala mkubwa kuhusu uhuru wa vyombo vya habari.

Jameel Jaffer, mkurugenzi wa taasisi ya haki ya kujieleza, alionya kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha kazi ya uandishi wa habari.

Alisema vyombo vya habari vina haki ya kikatiba kuchapisha taarifa muhimu kwa umma, na kulazimisha waandishi kufichua vyanzo vyao ni tishio kwa uhuru wa habari.

Baada ya ndege ya kijeshi ya Marekani kudunguliwa ndani ya Iran, mamlaka za Iran zilitoa kauli na hatua kadhaa muhimu hasa kuhusu kuwatafuta marubani waliokuwa ndani ya ndege hiyo.

Haya ndiyo yaliyosemwa na kufanywa na Iran:

  • Walithibitisha kudungua ndege ya Marekani
    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran viliripoti kuwa mifumo yao ya ulinzi wa anga ilifanikiwa kuidungua ndege hiyo ya kivita.
  • Walionesha mabaki ya ndege
    Picha na video zilionyeshwa zikidai kuonyesha vipande vya ndege hiyo iliyoanguka ndani ya ardhi ya Iran
  • Walianzisha msako wa marubani
    Vikosi vya kijeshi vya Iran vilianza operesheni ya kuwatafuta manusura wa ndege hiyo mara moja baada ya tukio
  • Raia waliombwa kusaidia kuwatafuta
    Serikali ilitoa wito kwa wananchi kuwa macho na kutoa taarifa endapo watabaini marubani wa Marekani waliokuwa wameanguka.
  • Ahadi ya zawadi ilitolewa
    Ripoti zinaeleza kuwa yeyote ambaye angefanikiwa kuwakamata marubani hao angepewa pongezi au zawadi maalum kutoka kwa mamlaka
  • Iran iliongeza shinikizo la kijeshi
    Wakati Marekani ikifanya operesheni ya uokoaji, vikosi vya Iran pia vilikuwa vikijaribu kuwafikia marubani hao kabla hawajaokolewa.